Kocha mkuu wa Simba sc, Mzambia Patrick Phiri (kulia)
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
SIMBA SC inajiandaa kuchuana na Polisi Morogoro
katika mechi ya raundi ya pili, ligi kuu
soka Tanzania bara itakayopigwa jumamosi uwanja wa Taifa, Dar es salaam.
Timu hizo mbili zitakutana zikiwa na matokeo tofauti
ya mechi za ufunguzi wikiendi iliyopita. Simba walitoka sare ya 2-2 na Coastal
Union uwanja wa Taifa, wakati Polisi Moro walitandikwa 3-1 na mabingwa watetezi
Azam fc katika uwanja wa Azam Complex.
Kocha Patrick Phiri hakuridhishwa na kiwango cha
timu yake na kuamua kwenda Visiwani Zanzibar tena kuwepa kambi ya maandalizi.
Simba kwasasa inaandamwa na majeruhi wengi. Jana
kipa namba moja Ivo Mapunda alivunjika kidole mazoezini na atakaa nje ya uwanja
kwa wiki nne.
Kuumia kwa Ivo ni pengo kwa kocha wa Simba ingawa
ataweza kumtumia kipa bora wa msimu uliopita, Hussein Sharif ‘Casillas’.
Mbali na Ivo, Mkenya Paul Kiongera naye ataikosa
mechi ya jumamosi. Bahati mbaya zaidi hata mechi ya watani wa jadi Oktoba 12
mwaka huu atakosekana kutonana na majeruhi sugu ya goti ambayo itamuweka nje ya
uwanja kwa takribani wiki sita au miezi miwili.
Mshambuliaji Elius Maguli naye alikuwa
anasumbuliwa na majeruhi, lakini kwasasa anaendelea vizuri na anaweza kucheza
jumamosi.
Amerudi?: Gerard Jonas Mkude amesumbuliwa na majeruhi ya muda mrefu
Kiungo wa ulinzi, Jonas Mkude naye anaendelea
kuimarika baada ya kukaa nje ya uwanjwa kwa muda mrefu akisumbuliwa na
majeruhi, lakini hajawahi kucheza chini ya Phiri. Kwa mazingira hayo dhahiri
kiungo huyu anahitaji kupata muda wa kurudisha kiwango chake.
Nyota mwingine, Haruna Chanongo atakaa nje ya
uwanja kwa siku 10 baada ya kuumia wikiendi iliyopita dhidi ya Coastal Union.
Beki wa kushoto, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ naye ana
majeruhi, hivyo hana uhakika wa kucheza mechi ijayo.
Kutokana na majeruhi yanayoiandama Simba, kocha
Phiri analazimika kufanya mabadiliko ya kikosi chake.
Ukiangalia kwa umakini unagundua kwa haraka kuwa baadhi
ya wachezaji walioumia ni wa kikosi cha kwanza, hivyo itaathiri timu kwa kiasi fulani.
Mchezaji wa kikosi cha kwanza ndiye chaguo la
kwanza kwa kocha. Inapotokea tatizo, analazimika kumpanga mbadala wake.
Ivo ni kipa namba moja, Casillas ni kipa namba
mbili. Phiri anapomkosa Ivo, analazimika kumtumia Casillas.
Lakini kama Ivo yuko fiti kwa asilimia 100,
Mzambia huyo hawezi kumuanzisha Casillas kirahisi.
Pengo?: Kipa Ivo Mapunda (kushoto) akisalimiana na waamuzi kwenye moja ya mechi ya Simba msimu uliopita
Nafasi ya Kiongera ina wachezaji wengi. Bado kuna
watu kama Emmanuel Okwi, Amissi Tambwe, Elius Maguli na Amri Kiemba ambao
wanaweza kuziba nafasi yake.
Safu ya ushambuliaji, Simba ina wachezaji wengi
wanaofanana majukumu, hivyo ni rahisi mwalimu kubadilisha kikosi chake.
Kukosekana kwa Chanongo, Ibrahim Twaha anaweza
kupata nafasi ya kucheza, lakini bado utakuwa mpango B wa Phiri. Asingeweza
kumchezesha Twaha wakati Chanongo yupo.
Pengo la Mkude, bado ni gumu kuliziba, Piere
Kwizera ameshindwa kukaribia uwezo wa kiungo huyo kijana.
Mechi iliyopita, Kwizera alijitahidi kupiga pasi
sahihi, lakini nyingi hazikwenda maeneo sahihi. Alikuwa pole pole kuanzisha
mashambulizi pale inapotakiwa na tatizo lilionekana wazi tofauti ambavyo
angecheza Mkude.
Simba wanakwenda kucheza na Polisi Morogoro,
kikosi kina majeruhi wengi, lakini wanaweza kupata matokeo kama watajipanga
vizuri.
Majeruhi ni suala la kawaida katika soka, lakini
athari yake ni kubwa na tunaona duniani kote timu zinavyohangaika pale zipoandamwa
na tatizo hilo.
Kutumia wachezaji wa mpango B huwa kuna madhara
kiufundi. Tumeona hata makocha wa Ulaya kama Arsene Wenger wanavyolalamika
wanapokuwa na majeruhi wengi kikosini.
Mchezaji wa ‘Plan B’ huwa halingani na mchezaji wa
‘Plan A’. Siku zote ‘Plan B’ huwa inafanywa kwa kulazimisha kwasababu hakuna
jinsi.
Paul Kiongera ni majeruhi
Phiri bila shaka anafanya kazi kubwa ya kuwafanya
wachezaji atakaowatumia wajiamini kwasababu itakuwa mechi ya presha kwao.
Wanahitaji kushinda ili kuendelea kuwajengea imani
mashabiki wao. Kinachotakiwa ni kuwapanga wachezaji kisaikolojia na waamini
wataweza.
Wachezaji wa Simba bila shaka wako fiti katika
utimamu wa mwili, ufundi na mbinu, lakini suala la saikolojia linatakiwa
kuangaliwa zaidi.
Kikubwa vijana wanatakiwa kukalishwa chini na
kuwapa mbinu zaidi ili wajiamini.
Ugumu wa mechi unakuja kutokana na namna Polisi
wanavyocheza. Walifungwa na Azam fc 3-1, lakini walionekana kuwa na hofu kubwa
hususani kipindi cha kwanza.
Wachezaji wa Polisi Moro walionekana wazi kutokuwa
makini, kutojiamini na wakawaruhusu Azam wacheza mpira katika eneo lao na
kushambuliwa zaidi.
Kadri dakika zilivyokuwa zinasonga mbele,
walionekana kubadilika na kujiamni. Kipindi cha pili walicheza vizuri,
walishambulia na kupata goli moja. Haikuwa kazi rahisi kwao kwasababu
walikutana na mabingwa watetezi.
Kocha Adolf Rishard ni mzoefu wa ligi kuu, lazima
amewatuliza vijana wake na kuwafanya wajiamini zaidi.
Simba watakutana na upinzani kwasababu tayari
Polisi Moro wamejua udhaifu wao, hivyo kocha Adolf ameendelea kuwafundisha nini
cha kufanya.
Lakini uwanja wa Taifa utakuwa mgumu zaidi kwa
Polisi kutokana na mazingira ya Simba kwa sasa. Timu imewavutia sana mashabiki
wake, wanajitokeza kwa wingi, hivyo presha itakuwa kubwa kwa wachezaji wa
Polisi.
Lakini kama Simba watawaacha wacheze mpira
hususani dakika za mwanzo (20-30) na kushindwa kuwafunga, basi mechi itaweza
kuwa ngumu kwao.
Mabao ya mapema huwa yanawaharibia wapinzani .
Kama Polisi watafungwa mapema zaidi
watashindwa kucheza mpira na itatakiwa kocha atumie maarifa kuwapanga upya,
lakini wakikaza dakika 20-30 za mwanzo, wataongeza kujiamini na mechi itakuwa
ngumu kwa Simba.
0 comments:
Post a Comment