Na Baraka Mpenja, Dar esl salaam
IMEELEZWA kuwa mshambuliaji wa Simba sc, Mkenya
Paul Kiongera Mungai leo amefanyiwa vipimo hospitali ya Taifa ya Muhimbili kufuatia
kuumia goti katika sare ya 2-2 dhidi ya Coastal Union, jumapili iliyopita
uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Katika vipimo vya awali, Kiongera amebainika kuwa
na majeruhi sugu ya goti kama ilivyowahi kuelezwa na mtandao huu siku za nyuma.
Kiongera anayekonga nyoyo za mashabiki wa Simba
alitokea benchi katika dakika ya 67 dhidi ya Wagosi wa Kaya, lakini dakika
mbili kabla ya mechi kuisha alitonesha goti lake kwa kugongana na kipa Shaaban
Hassan Kado, hivyo kulazimika kumpisha Amri Kiemba.
Baada ya kuumia, Kiongera alionekana kubadilika
katika lugha yake ya mwili ‘Body Language’ akionesha kuwa ameumia sana na
hataweza kurudi uwanjani kirahisi.
Kabla ya kusajiliwa majira ya kiangazi mwaka huu,
ripoti zilifafanua kuwa Kiongera ana majeruhi ya muda mrefu aliyopata wakati
anacheza Kenya, lakini kutokana na Simba kukosa mfumo wa kupima afya za
wachezaji kabla ya kuwasajili walijikuta wakimsainisha mkataba akiwa na ‘pancha’.
Imefahamika kuwa Kiongera anaweza kuwa nje ya
uwanja kwa wiki sita au miezi miwili na litakuwa pigo kwa Wanamsimbazi wanaovutiwa
na uchezaji wa Mkenya huyo.
Kwa maana hiyo Oktoba 12 mwaka huu kuna uwezekano
mkubwa nyota huyo akautazama mpambano wa watani wa jadi, Simba na Yanga akiwa jukwaani
na kuwaacha mashabiki wa Simba wakisikitika.
Mbali na Kiongera, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ ni
majeruhi pia, wakati Haruna Chanongo aliyeumia kwenye mechi dhidi ya Coastal
Union anaweza kurudi uwanjani muda wowote.
Wakati huo huo, Kiungo wa ulinzi aliyekaa nje ya
uwanja kwa muda mrefu sasa, Jonas Mkude ameimarika kiasi cha kusubiri maamuzi
ya kocha Patrick Phiri kumpanga katika mechi ijayo dhidi Polisi Morogoro,
Septemba 27 mwaka huu uwanja wa Taifa, Dar es salaam.
Mkude hajawahi kucheza chini ya kocha Phiri wala
kufanya mazoezi, kwahiyo Mzambia huyo ndiye mwenye maamuzi ya kumpanga au kumpa
mazoezi maalumu ili kuimarika zaidi.
Mechi iliyopita, Piere Kwizera alicheza nafasi ya
Mkude, lakini alionekana kutoimudu kwa asilimia kubwa na alikosa maamuzi sahihi
hasa katika upigaji wa pasi.
Alikuwa anachelewa kuanzisha ‘Movement’ pale
inapobidi na alikuwa anapiga pasi vizuri bila kukosea -kukosea, lakini nyingi
hazikuwa na madhara kwa Coastal Union.
0 comments:
Post a Comment