
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
YANGA kuifunga Simba katika mechi ya kirafiki, bonanza au mashindano ni
faida kubwa kwa kocha na wasaidizi wake, vivyo hivyo kwa upande wa pili.
Makocha wengi wa nyuma waliwahi kusifiwa na
kuonekana bora kwa kitendo cha kumuadhibu mtani wa jadi, na wale waliozichomesha
timu zao mbele ya mtani walitimuliwa kirahisi tu.
Hata wachezaji wanaofanya vizuri baina ya watani
wa jadi wanaonekana moto wa kuotea mbali kuliko wale wanaofanya vizuri kwenye
mechi dhidi ya timu nyingine.
Sahizi Simba na Yanga zipo chimbo kujiandaa na
ligi kuu msimu wa 2014/2015 unaotarajia kuanza kutimua vumbi septemba 20 mwaka
huu.
Yanga wataanza kampeni zao septemba 20 mwaka huu
uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro dhidi ya Mtibwa Sugar, wakati siku inayofuata
(septemba 21) Simba watakuwa uwanja wa Taifa kuivaa Coastal Union.
Mashabiki na viongozi wa timu hizi mbili
wanatambiana vikali mno kila mmoja akisema mtani atakiona cha moto.
Wanajangwani wanakwambia ‘Okwi mwisho Chalinze,
kila mtu mjini Jaja’. Wanamsimbazi nao wanatamba na urejeo wa Okwi wakisema
kipigo cha 5-0 kipo njiani.
Andrey Coutinho wa Yanga naye anatumika na
wanayanga kuichimba Mkwara Simba, huku nako kuna mtu anaitwa Paul Kiongera.
Juzi uwanja wa Taifa,Dar es salaa, Geilson Santos
Santana ‘Jaja’ alifunga mabao mawili katika ushindi wa Yanga wa 3-0 dhidi ya
Azam fc mechi ya Ngao ya Jamii kuashiria kupenuliwa kwa pazia la ligi kuu.
Baada ya kitendo hicho, Jaja aliteka jiji zima,
kila kona Jaja tu. Na wanayanga waliimba nyimbo na kumsifia sana Mbrazil huyo
licha ya siku za karibuni kuona hana uwezo.
Atawika ligi kuu?: Emmanuel Okwi (kushoto) akifanya vitu vyake dhidi ya Gor Mahia
Sasa wimbo ni Oktoba 12 mwaka huu ambapo timu hizo
zitakutana. Mashabiki wa Yanga wanatamba kuwa Jaja atawamaliza Simba, nao wa
Msimbazi wanatamba na nyota wao Pual Kiongera aliyefungwa mabao mawili katika
ushindi wa mabao 3-0, mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Gor Mahia, uwanja
wa Taifa, septemba 6 mwaka huu.
Mbali na Kiongera, Simba wanajivunia mfungaji bora
wa msimu uliopita, Mrundi, Amissi Tambwe.
Binafsi sioni kama tambo hizi zina maana yoyote
katika maendeleo ya mpira wa miguu wa nchi hii. Nadhani imechangiwa na mitazamo
mifupi ya mashabiki wengi wa soka na viongozi kwa ujumla.
Leo hii unamsikia kiongozi wa juu wa Yanga au
Simba akizungumzia namna wanavyojiandaa kumfunga mpinzani mabao 5-0 au 8-0.
Utani wa jadi ni muhimu katika soka, lakini
wenzetu wa ulaya wanakuwa na mipango ya mashindano makubwa zaidi ya ligi kuu.
Mashabiki wa Manchester United wanapenda sana
kuona timu yao inawafunga mahasimu wao Manchester City, ua Barcelona kwa Real
Madrid, lakini wakati huo huo wanapenda kuona timu zao zinafanikiwa UEFA.
Wenzetu wanathamini sana michuano kama UEFA na
huwa wanawekeza fedha na muda kujiandaa nayo. Ndio maana ukiwasikia makocha
wengi au viongozi, huwa wanasema msimu
huu utakuwa mgumu kwetu kwasababu tunakabiliwa na UEFA.

Jaja ni wimbo wa mjini kwasasa
Kama timu haichezi UEFA kama ilivyokuwa kwa
Liverpool msimu uliopita au Manchester United kwa msimu huu inapewa nafasi ya
kufanya vizuri zaidi.
Hapa unagundua kitu kimoja muhimu kuwa licha ya
Chelsea kumsajili Diego Costa ili aifunge Arsenal, Man United na timu nyinginezo,
lakini wanawaza zaidi kuzifunga timu nyingine za ulaya katika michuano ya UEFA.
Kwahiyo wenzetu wanajua fika kuwa kuna maana kubwa
kutwaa taji la UEFA kuliko ligi kuu, ingawa ni muhimu zaidi kutwaa kombe la
ligi kuu au kushika nafasi nzuri ili ushiriki UEFA.
Sisemi ligi kuu sio muhimu, kuna ulazima wa
kufanya vizuri na kupata nafasi ya kucheza michuano mikubwa.
Simba hawana michuano ya kimataifa mwakani. Nguvu
zote zinaelekezwa katika michuano hiyo ili kutwaa kombe na kupata nafasi ya
kucheza ligi ya mabingwa au kombe la shirikisho mwakani endapo watashika nafasi
ya pili.
Ni halali kwa Simba kuifikiria ligi kuu, lakini
sio kuifikiria Yanga tu. Kwasababu hawawezi kushinda kombe kwa kumfunga Mtani
pekee.
Yanga asiwe kichwani mwao muda wote, wafikirie
kuwa kuna Azam fc, Mbeya City fc, Kagera Sugar, Ruvu Shootingm Mtibwa Sugar na
nyinginezo.
Nadhani ule wakati wa kuweka mikakati ya mechi ya
mtani, kuificha timu na kwenda kwa wataalamu wa mambo yale ya kutambika,
umepitwa na wakati. Inatakiwa timu kuandaliwa kwa mechi zote 26.
Sidhani kama fikira za Patrick Phiri ziko sawasawa
na mashabiki wake wanaofikiria namna Okwi atakavyoifunga Yanga.
Malengo ya Phiri ni kushinda mechi zote kwasababu
itazidi kujenga wasifu wake hata akiondoka Tanzania. Huwezi kuajiriwa kwa CV ya
kumfunga Mtani, hapana! .

Kwa upande wa Yanga wakumbuke kuwa wana majukumu
mazito kuliko Simba. Watashiriki kombe la shirikisho na ligi kuu.
Nategemea kuona wanayanga wakitamba kuwa
tumemsajili Jaja, Al Ahly tukikutana nao watatukoma. Wanatakiwa kufikiria mbali
zaidi na kujenga heshima.
Mawazo ya kuifikiria Simba wakati utacheza kombe
la shirikisho, ni kukosa maono kabisa. Imefika
wakati timu zetu zitakazowakilisha nchi zifikirie mambo mawili kwa uzito wa
juu. Yaani Yanga wawaze Kombe la shirikisho na ligi kuu.
Waiandae timu kwa misingi hiyo na sio kuifikiria
Simba. Kama watafungwa na Simba, lakini wakafanya vizuri kombe la shirikisho,
kutakuwa na faida kubwa kimpira kuliko kuifunga Simba, halafu wanatolewa raundi
ya awali.
Leo hii kiongozi anaonekana wa maana kwasababu
amemfunga mtani. Tena hawana aibu kusema naangia madarakani kuwakomesha
mahasimu wetu.
Yaani unapigiwa kura eti ukamfunge mtann? Tuna malengo
ya kulisongesha soka letu?

Paul Kiongera anawakuna mashabiki wa Simba
Nakuwa na furaha sana ninapomsikia kiongozi
akisema tunaiandaa timu kwa michuano ya kimataifa, tunataka kuifikisha timu
anga za kimataifa, lakini nakereka sana ninaposikia mtu anasema tunaiandaa
timu, msimu huu Simba na Yanga hawatoki.
Mwisho wa siku wanazikamia mechi na kutoa sare,
lakini wakikutana na timu nyingene, wanachemsha. Wengine wanashuka daraja,
wengine wanashika nafasi za mkiani.
Kwa mfano Azam fc mwakani wanashiriki ligi ya
mabingwa. Haina maana kuingia katika siasa za kuifunga Simba au Yanga.
Wao wanatakiwa kufikiria timu pinzani za ligi ya
mabingwa, lakini kwa vile viongozi wamekosa maono, wanakesha kufikiria
kuzifunga Simba na Yanga.
Hatuwezi kuendelea kwa kushindana wenyewe. Unataka
Jaja aifunge Simba au Kiongera aifunge Yanga na si TP Mazembe?
Lazima tuachane na mambo ya kizamani. Kocha
asifukuzwe kwasababu amefungwa na mtani. Ni kitu cha kawaida, mbona Man United
hata kama watafungwa nje-ndani na Man City wanawaacha makocha?
Vipi kwa Real Madrid inapofungwa na Barcelona,
nje-ndani, makocha wanatimuliwa?, hapana! Wanaangalia michezo yote ya ligi.
Kama timu haijafanya vizuri, wanachukua maamuzi.
Najua Maximo anawaza mbali kuliko mashabiki na
viongozi wanaowaza kuifunga Simba. Naamini Phiri anawaza mbali zaidi ya
kuifunga Yanga.
Kufundisha mpira ni kazi yao. Anaweza kuajiriwa
popote pale, na ndio maana wanajitahidi kushinda makombe ili kujenga wasifu
utakaowasaidia mbeleni.
Mashabiki badala ya kuwasaidia kwa mipango mizuri,
tunafurahia wamfunge mtani tu, biashara imekwisha, tutafika?
Siku njema!
0 comments:
Post a Comment