Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
HABARI mbaya kwa mashabiki wa Simba sc ni kwamba
kipa namba moja wa klabu hiyo, Ivo Philip Mapunda amepata majeruhi
itakayomuweka nje ya uwanja kwa wiki nne.
Kocha msaidizi wa klabu hiyo, Seleman Abdallah
Matola ‘Veron’ amesema kuwa Ivo ameumia kidole chake leo katika mazoezi ya
klabu hiyo visiwani Zanzibar na daktari
wa timu amethibitisha.
Mapunda ataikosa mechi ya watani wa jadi oktoba 12
mwaka huu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Hata hivyo, Matola amesema kukosekana kwa Ivo sio
tatizo kubwa kwasababu wana makipa wengine kama Hussein Sharif ‘Casillas’ na
kipa Peter Manyika ambao wanaweza kufanya kazi vizuri.
Casillas na Manyika walisajiliwa majira ya
kiangazi mwaka huu baada ya mnyama kuachana na kipa Mghana Yaw Berko mwishoni
mwa msimu uliopita na kubaki na Ivo.
Majeruhi wanazidi kuongezeka Simba ambapo mpaka
sasa Jonas Mkude hayuko fiti kucheza kwa sasa ingawa ameshaanza mazoezi mepesi.
Mkenya Pual Kiongera naye aliumia mechi ya
jumapili iliyopita dhidi ya Coastal Union na taarifa zilizotoka jana ni kwamba
ana majeruhi sugu ya goti.
Ilifahamika kuwa Kiongera naye atakaa nje ya
uwanja kwa wiki sita au miezi miwili.
Naye beki wa kushoto Issa Rashid ‘Baba Ubaya’
anasumbuliwa na majeruhi na hana uhakika wa kucheza mechi ijayo.
Simba imejificha Zanzibar kujiandaa na mechi ijayo
ya ligi kuu dhidi ya Polisi Morogoro itayopigwa jumamosi (septemba 27 mwaka
huu) uwanja wa Taifa, Dar es salaam.
0 comments:
Post a Comment