Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
MBEYA CITY FC ni klabu inayosubiriwa kwa hamu
katika michuano ya ligi kuu kwasababu msimu uliopita ilitoa changamoto kubwa
kwa klabu za juu, Simba, Yanga na mabingwa Azam fc.
Katika mechi 26 za ligi kuu, timu hii inayonolewa na kocha Juma Mwambusi
ilifungwa mechi tatu tu ambapo ya Kwanza ilichapwa na Yanga 1-0 uwanja wa
taifa.
Mechi ya pili ilipoteza 2-0 dhidi ya Coastal Union
Uwanja wa CCM Mkwakwani Tanga na mechi ya tatu ikafungwa 2-1 na Azam fc uwanja
wa Sokoine Mbeya.
Ilipocheza na Azam fc uwanja wa Azam Complex,
mechi ya mzunguko wa kwanza, City ilitoka sare ya mabao 3-3. Wakati Yanga
walilazimisha sare ya 1-1 uwanja wa sokoine mzunguko wa kwanza sawa na Coastal
Union ambao walipata matokeo kama hayo katika uwanja huo mgumu kwa timu
pinzani.
Mbeya City walifanikiwa kushika nafasi ya tatu
nyuma ya Yanga na Azam fc ambao walitwaa ubingwa.
Lakini moja ya matukio ninayoyakumbuka vizuri kwa
timu hii ya Mbeya City ni jinsi mashabiki wa Mbeya walivyokuwa na mwamko wa
kuishangilia timu yao.
Walisafiri maeneo mengi ambayo City ilikwenda kucheza,
hakika walifanya jambo linalotarajiwa kuigwa na watu wa Mtwara kwa Ndanda fc na
Shinyanga kwa timu yao ya Stand United.
Wataendeleza?: Mashabiki wa Mbeya City fc waliwahi kupiga mawe gari la Tanzania Prisons
Ukiwafuatilia watu wa Mtwara na Shinyanga,
wanatamani sana kufikia mafanikio ya Mbeya City, na wana malengo ya kuzitupa
kule timu za Simba na Yanga.
Mashabiki wa Mbeya City wanafaa kuigwa kwa namna
wanavyoshangilia timu yao, lakini kuna mambo mawili wanatakiwa kutoigwa kabisa
kwasababu hayawezi kuiendeleza timu.
Mosi: kutokukubali
matokeo mabaya, mara nyingi mashabiki wa Mbeya City wanaonekana kuwa na
jaziba pale timu yao inapokosea. Wana amini kuwa haki ya kushinda iko upande
wao.
Niliwahi kushangaa siku moja ikishida 2-1 dhidi ya
Ruvu Shooting. Mashabiki walimzomea kocha Mwambusi wakati matokeo yakiwa sare
ya 1-1 mpaka dakika za lala salama kabla ya kufunga bao la ushindi. Kabla ya mechi
hiy, City ilitoka sare na Yanga, Kagera Sugar na Coastal Union.
Matokeo hayo yalionekana kuwakera mashabiki wake,
licha ya ukweli kuwa yalikuwa mazuri kimpira kwasababu timu ilikuwa ngeni na
ilikutana na timu ngumu zenye uzoefu na ligi kuu.
Mashabiki wa Mbeya City fc mara nyingi huwa wanakosa uvumilivu
Kwa watu wa mpira hawakushangaa matokeo kama hayo,
kwasababu kuna faida ya kupata pointi moja kuliko kupoteza kabisa. Timu ndio
kwanza inaanza, unamzomea mwalimu na wachezaji, kwanini?
Mpira hauko hivyo, hapa mashabiki wa Mbeya City
walifeli. Hivyo watu wa Mtwara na Shinyanga, mnatakiwa kuachana na tabia hii
kama mnataka kufanikiwa.
Pili; kujihusisha na vurugu. Mara kadhaa mashabiki
wa Mbeya City walijihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu kwenye mpira. Waliwahi
kurushia mawe basi la Yanga na kupasua vioo hatimaye kumjeruhi dereva uwanja wa
Sokoine.
Waliwahi kufanya vurugu kubwa kwenye mechi dhidi
ya Tanzania Prisons. Kiufupi wana rekodi ya utovu wa nidhamu na walishaigharimu
timu kwa tabia hii. Mara kadhaa City walitozwa faini na TFF.
Hata kwenye mechi ya majaribio ya tiketi za
kielekroniki baina ya Mbeya City na Prisons mwaka huu, kulitokea vurugu ambazo
hata wachezaji walishiriki, lakini Mwambusi aliwatetea na kudai wanaonewa.
Vurugu hazifai kwenye mchezo, watu wa Mtwara na
Shinyanga, hili hampaswi kuiga kabisa.
Lakini jambo jingine ni juzi (jumamosi)
walivyofungwa 4-1 na Vipers FC ya Uganda katika mechi ya kimataifa ya kirafiki.
Mashabiki walionekana kukerwa na matokeo na
waliowengi walitoka kabla ya mechi kumalizika na leongo likiwa ni kuashiria kutopenda
kilichotokea.
Vipers FC ni wazuri kuliko Mbeya City FC na mpira
ulionekana uwanjani, lakini mashabiki hawakuwa tayari kukubali kama timu
imezidiwa na badala yake wengine wakatoka kabla ya muda.
Yawezekana wengine walikuwa wanawahi usafiri, lakini
waliowengi, hususani wa Mbeya mjini walitoka kwasababu ya kukerwa na matokeo.
Haipaswi kuwe hivi katika mpira. Mara ngapi watu
wanafungwa, lakini wanashangilia mwanzo mwisho?, hili pia mashabiki wa Mbeya
City wamefeli.
Kuna haja ya kubadilika, watu wa Stand United na Ndanda msijifunze
tabia hizi tatu nilizozisema. Mpira hauko hivyo. Na ninyi wa Mbeya City
jifunzeni kukubali matokeo, la sivyo mtazidi kupotea katika njia.
Timu yenu ni nzuri, ina kocha mzuri, lakini kama
hamtafuta kasumba hii, basi hamtafika mbali kama mnavyodhani.
0 comments:
Post a Comment