Na Baraka Mpenja
WAGONGA nyundo wa Mbeya, Mbeya City fc
wametandikwa mabao 4-1 na Vipers FC (Zamani Bunamwaya) inayoshiriki ligi ya
Uganda katika mechi ya kimataifa ya kirafiki iliyomalizika jioni ya leo uwanja
wa Sokoine jijini Mbeya.
Vipers FC waliowasili leo asubuhi jijini humo
walitandaza soka safi na kuwazidi wenyeji wao karibia idara zote.
Hata hivyo taarifa kutoka kwa shuhuda wetu aliyekuwepo
uwanjani hapo, Mbeya City walijitahidi kugangamala, lakini walionekana kutokuwa
na ushindani wa ngazi ya kimataifa.
Mechi hiyo ni ya mwisho ya kujipima ubavu kwa
kocha Juma Mwambusi ambaye ana
changamoto ya kufanya vizuri katika msimu mpya wa ligi kuu Tanzania bara unaotarajia
kuanza kutimua vumbi septemba 20 mwaka huu.
Mwambusi aliyeibuka kuwa kocha bora msimu
uliopita, anasaidiwa na Suleiman Jabiri baada ya msaidizi wake Maka Mwalwisyi
kukataa kuongeza mkataba muda mfupi baada ya ligi kuu msimu uliopita kumalizika.
Maka kwasasa ni kocha mkuu wa klabu ya Panone FC
ya mkoani Kilimanjaro na inashiriki ligi daraja la kwanza.
Mbeya City msimu uliopita walimaliza katika nafasi
ya tatu nyuma ya Yanga na mabingwa Azam fc.
Wakali hao wanaovalia jezi za zambarao wataanza
kampeni ya ligi kuu msimu wa 2014/2015 kwa kuwakaribisha JKT Ruvu katika uwanja
wa Sokoine jijini Mbeya, septemba 20 mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment