JACOB MASAWE ni miongoni mwa wachezaji wa
kutegemewa katika kikosi cha Ndanda fc ya mkoani Mtwara chini ya kocha kijana,
Denis Kitambi.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Ndanda fc ikicheza
ugenini dhidi ya Stand United katika uwanja wa CCM Kambarage , Shinyanga, Jacob
alikuwa miongoni mwa wanandinga walioanza ligi kuu kwa kushindo wakitoa kipigo
cha 4-1 kwa wenyeji.
Jacob ambaye ni mdogo wa kocha wa sasa wa Stand
United, Emmanuel Masawe, hupendelea zaidi kucheza nafasi ya ushambuliaji wa
pembeni, namba 7 na 11, lakini katika mechi hiyo hakuonesha kiwango chake kama alivyozoeleka.
Msimu wa 2010/2011, Jacob alichaguliwa kuwa
mchezaji bora wa ligi kuu soka Tanzania bara na mtandao huu umeamua kufanya
mahojiano naye. Fuatilia mahojiano haya….
Mwandishi: Mwishoni mwa wiki kwenye mechi ya
ufunguzi wa ligi kuu Vodacom Tanzania bara kati ya timu yako ya Ndanda fc dhidi
ya Stand United katika uwanja wa Kambarage, ulikuwa unarejea nyumbani baada ya kuondoka
kwa muda, ulijisikiaje kucheza na timu
ambayo ina mazingira ya kinyumbani?
Masawe: Kweli nilijisikia amani sana, kwasababu
tangu nimeanza kucheza mpira ligi ligi kuu sijawahi kucheza uwanja wa nyumbani
wa CCM Kambarage.
Katika maisha yangu yote sijawahi kucheza mpira nje
ya timu ya kaka yangu (Emmanuel) , kwasababu yeye ndiye amenifundisha na kila
timu aliyokuwa akifundisha ilikuwa lazima niwepo. Mechi ya jumamosi ilikuwa ya
kihistoria katika maisha yangu.
Mwandishi: Ilikuwa ya kihistoria kwa maana gani
kwasababu wewe ni mzaliwa wa Shinyanga, umekuwa ukicheza mpira katika maeneo
hayo, hususani katikati ya mji, ni kitu gani kilikuzuia kucheza uwanja wa
Kambarage kabla?
Masawe: Tangu naingia kucheza ligi kuu, Shinyanga
haikuwa na timu yoyote ya ligi kuu na kaka yangu hakuwahi kufundisha timu
yoyote ya ligi kuu, kwahiyo nasema ni historia kukanyaga uwanja wa Kambarage.
Pia ni mara yangu ya kwanza kukutana na timu tofauti anayofundisha kaka yangu.
Mwandishi: Kabla ya mechi uliwahi kuwasiliana na
kaka yako?
Masawe: Sikuwahi kuwasiliana naye kuhusu mpira
wakati wa maandalizi zaidi ya kuwasiliana naye kuuliza mambo ya kifamilia,
lakini ilikuwa muda kidogo, siku tano au
sita kabla ya mechi hatukuwasiliana kabisa.
Mwandishi: Kabla ya kucheza Ndanda fc, ni timu
gani nyingine za ligi kuu umewahi kuzichezea?
Masawe: Timu yangu ya kwanza kucheza ligi kuu ni
Toto African, baada ya hapo nikaenda kucheza Africa Lyon na baadaye Mwadui fc.
Baada ya hapo nilisajiliwa na JKT Oljoro na sasa niko Ndanda fc.
Mwandishi: 2010/2011 ulikuwa mchezaji bora wa ligi
kuu ya Vodacom, ni kipi kilichosababisha ufikie mafanikio hayo na sasa hivi
huoni kama ni muda mwingine wa kuchukua tuzo hiyo kwa mara nyingine?
Masawe: Kikubwa kilichonifanya nichukue tuzo mwaka
2010/2011 ni nidhamu niliyokuwa nayo. Cha pili nilikuwa najituma sana hususani
nilipokuwa Toto African ambayo ilikuwa timu yangu ya kwanza na nilitamani sana
kucheza ligi kuu kabla.
Kwahiyo nikiwa Toto nilicheza kwa nguvu zangu zote
na akili zangu zote na ndio maana nikachaguliwa kuwa mchezaji bora. Hapa Ndanda
fc naamini nitafanikiwa kwasababu timu ina kila kitu na inabaki kwa mchezaji
kujituma.
Mwandishi: Wewe ukiwa uwanjani ni nafasi ipi unafurahia
kucheza?
Naifurahia sana nafasi ya mshambuliaji wa pembeni,
namba 7 na 11.
Mwandishi: Mchezaji gani anayekuvutia hapa
nyumbani na nje ya nchi?
Masawe: Hapa nyumbani anayenivutia sana ni Haruna
Moshi ‘Boban’ na nje ya nchi nampenda sana Lionel Messi.
Mwandishi: Unamzungumziaje Denis Kitambi, kocha wa
Ndanda fc na ana utofauti gani na makocha waliomtangulia?
Masawe: Kocha kitambi ni mwalimu ambaye yuko
karibu sana na wachezaji na anapokuwa kwenye mazoezi unajisikia vizuri.
Ule ukaribu unamfanya kila mchezaji kuwa makini
kusikiliza kile anachoelekeza. Tofauti na mazoezini, anacheka na kila mtu kwasababu ni kijana
mwenzetu, inakuwa kama mchezaji vile tofauti na walimu wengine.
Mwandishi: Mechi dhidi ya Stand United hukucheza
vizuri kama kawaida yako, ulikuwa na wasiwasi nini?
Masawe: Ni kweli kabisa sikucheza vizuri, lakini
kama nilivyokwambia ilikuwa mechi yangu ya kwanza kucheza katika uwanja wa CCM
Kambarage nikiwa na timu ya ligi kuu.
Pia ilikuwa
mara ya kwanza kucheza timu tofauti na kaka yangu, halafu nilikuwa nacheza
mbele ya familia yangu, rafiki zangu. kwahiyo nilikuwa na kitu kama kauoga
hivi, lakini nilitamani nifanye kitu bora na haikuwa hivyo. Huo ndio mpira na
nashukuru kwa kile nilichoonesha.
Mwandishi: Kama Mungu angekujaalia kufunga goli
ungeshangiliaje?
Masawe: Nisingeshangilia kwasababu mimi ni mmoja
wa waanzilishi wa Stand United. Tulipokuwa tunacheza ligi kuu, tukirudi
nyumbani tulikuwa na timu yetu ya mtaani iliyoitwa Fanta. Kwa bahati mbaya
ikafa na baada ya hapo kulikuwa na mashindano, tukaamua kuunda timu ya Stand
kwasababu marafiki zangu wengi wanafanya kazi Stand ya mabasi, kwahiyo tukaona
haina budi kuunda timu.
Nisingeshangilia kwasababu mimi ni mwanzilishi
wa Stand, halafu kuna kaka yangu.
Mwandishi: Asante sana Masawe nikutakie maisha
mema na Ndanda fc katika msimu huu wa ligi kuu.
Masawe: Nashukuru sana!
0 comments:
Post a Comment