Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' (wa kwanza kulia, waliosimama wima)
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
KUMKUBALI mpinzani wako pale anapokukaba koo katika
soka ni ushujaa mkubwa na inaonesha kuwa wewe ni mshindani wa kweli.
Kuna wachezaji, makocha, viongozi na mashabiki wa
soka huwa hawataki kuzungumza ukweli pale timu yao inapofungwa au kushinda.
Siku zote mtu anapenda kusifia chake, hata kama
timu yake ilicheza vibaya na kupata magoli, basi atasifia mno. Lakini itakuwa
ngumu kusikia akisema tulicheza vibaya ingawa tumeshinda.
Kibongo-Bongo, Simba na Yanga ndio habari ya
mjini. Mashabiki wa Yanga wanajasikia furaha sana pale wanapoona timu yao
inapata ushindi, hawajali sana namna inavyocheza.
Jana Yanga walichuana na Tanzania Prisons uwanja
wa Taifa na kushinda mabao 2-1.
Wakicheza pungufu kwa dakika 52, Prisons
walionesha kandanda safi na kuitia presha Yanga hususani kipindi cha pili.
Yanga walijitahidi kucheza vizuri sehemu ya kati
na mbele, lakini bado safu ya ulinzi iliyoongozwa na Juma Abdul, David Charles,
Nadir Haroub ‘Cannavaro, Kelvin Yondani/Rajab Zahir, iliendelea kuwa na ugonjwa
wa kujisahau.
Hata goli walilofungwa jana, Cannavaro na Yondani walizembea na kumuacha
Ibrahim Kasaka Hassan akiruka juu na kupiga kichwa huru kilichomshinda kipa
Deogratius Munish ‘Dida’.
Baada ya mechi mashabiki wa Yanga walifurahia
ushindi ikizingatiwa walitoka kwenye machungu ya kufungwa 2-0 na Mtibwa Sugar
uwanja wa Jamhuri.
Baadhi ya mashabiki walikiri wazi kabisa kwamba
wamepata pointi tatu, lakini hali ilikuwa tete kwa upande wa Yanga.
Ghafla wakati wakizungumza hayo, akatokea nahodha
wa Yanga na beki kisiki maarufu kama ‘Waziri wa Ulinzi’ wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Mzanzibar huyu alionesha wazi furaha yake baada ya
kuwaongoza wachezaji wenzake kupata ushindi mbele ya timu iliyokuwa bora.
Cannavaro alisema: “Kwanza ni matokeo mazuri.
Prisons ni timu nzuri na imeonesha kwamba ina uwezo. Tumecheza na kupata nafasi
nyingi, tumepata magoli na tunashukuru kwa kupata ushindi.”
“Siku zote timu ikiwa pungufu inacheza kwa bidii.
Wakipungua wanakuja mbele zaidi, na kwasababu na sisi tumeshinda tunalinda goli
letu. Walirejesha goli na tukaweza kupata goli la pili, ila Prisons ni timu
nzuri na tunashukuru kwamba tumepata ushindi na kusogea mpaka nafasi ya tano”.
“Bado tuna makosa madogo madogo, nadhani kwenye
mazoezi tutajirekebisha. Kwenye mechi dhidi ya JKT Ruvu tutaongeza nguvu zaidi”.
Yanga watashuka dimbani tena wikiendi ijayo
(Oktoba 5 mwaka huu) kumenyana na JKT Ruvu uwanja wa Taifa, Dar e salaam.
0 comments:
Post a Comment