Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
UWANJA wa Azam Complex unaomilikiwa na mabingwa
watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara, Azam fc umezidi kuwa mgumu kwa timu za
ligi kuu.
Timu pinzani zinapofika maeneo ya Chamazi zinaanza
kupata harufu ya kipigo kutoka kwa wenyeji wao.
Chamazi si sehemu salama kwa timu za ligi kuu
isipokuwa kwa Simba na Yanga ambao hawajawahi kucheza katika uwanja huo.
Azam fc wakiendelea kuutumia vyema uwanja wao wa
nyumbani, jana walishinda mabao 2-0 dhidi ya Ruvu Shooting ya Mkoani Pwani.
Kabla ya mechi hii, niliandika kupitia mtandao huu
nikisema Azam fc wataifunga Ruvu Shooting kwasababu mazingira ya Chamazi ni
rafiki kwao na wana kikosi kilichojaa. Nilisema sio rahisi kuifunga Azam katika
uwanja wake, hata rekodi zinaonesha hivyo.
Azam walikwenda kupumzika wakiwa mbele kwa bao 1-0
liliofungwa na Mrundi, Didier Kavumnagu katika dakika ya 40.
Kavumbagu alifunga goli hilo baada ya kuuwahi
mpira uliotemwa na mlinda mlango wa Ruvu Shooting, Abdallah Abdallah kufuatia
shuti la Kipre Tchetche aliyeunganisha krosi murua ya Shomari Salum Kapombe.
Lilikuwa bao jepesi kabisa kwa Didier, lakini
lilitosha kufikisha mabao 3 katika mechi mbili, baada ya kufunga mawili katika
ushindi wa 3-1 dhidi ya Polisi Morogoro katika mechi ya ufunguzi.
Dakika ya 50, Himid Mao Mkami alipiga krosi safi
iliyomaliziwa kiufundi na Didier Kavumbagu na kuiandikia Azam bao la pili.
Hilo lilikuwa bao la nne kwa Kavumbagu katika
mechi mbili na inaonekana safari hii amedhamiria kupata kiatu cha dhahabu
anachomiliki Amissi Tambwe wa Simba. Hata
hivyo, Kavumbagu alikosa baadhi ya nafasi kadhaa za kufunga.
Mabeki wa kati wa Ruvu Shooting, Salvatory Ntebe
na Hamisi Kasanga walishindwa kuhimili makali ya washambuliaji wa Azam fc na
mara nyingi waliruhusu mashambulizi langoni mwao.
Katika dakika ya 70, Salum Abubakary ‘Sure Boy’
alikaribia kufunga, lakini alikosa umakini wa kuunganisha krosi ya Kavumbagu na
dakika tano baadaye, Mrundi huyo alishindwa kufunga ‘Hat-trick’ ya kwanza msimu
huu kufuatia kutengenezewa mpira safi na Tchetche.
Kipre Balou, Mudathir Yahya walishika barabara
sehemu ya kati, huku Salum Abubakar aliyecheza nyuma ya Didier Kavumbagu
akifanya kazi nzuri.
Tchetche aliyeshambulia kutoka kushoto na Himid
Mao kutoka kulia, waliisaidia Azam kufika mara nyingi zaidi langoni kwa Shooting,
wakipiga krosi na kutoa pasi kwa washambuliaji wa kati.
Azam fc wamekuwa wakiutendea haki uwanja wa
nyumbani. Inafahamika kuwa kucheza nyumbani ni moja ya sababu ya kushinda
mechi.
Uwanja wa nyumbani huwa ni rafiki kwa wachezaji.
Wanakuwa huru na wanacheza mbele ya mashabiki wao wengi.
Azam fc haina mashabiki wengi kivile ukilinganisha
na Simba au Yanga, hata uwanja wa Chamazi huwa haujai. Lakini haiwapi shida
kufanya vizuri.
Lakini mbele ya mashabiki wao wachache huko
Chamazi, wamekuwa wakitandaza soka safi na kuiadhibu karibia kila timu
inayogusa uwanja wao.
Kwa bahati mbaya watu hawapati nafasi ya kuwaona
Azam fc hasa wanapocheza siku ambayo Simba au Yanga inacheza pia. Lakini hawa
vijana wanaonekana kuwa na mipango sahihi na morali kubwa ya ushindi.
Kwa asimilia kubwa wachezaji wa Azam wana utimamu
mzuri wa mwili, wako fiti kimbinu, kiufundi na kisaikolojia. Mazingira haya
yamewafanya wacheze mpira vizuri na kwa utulivu.
Kwa jinsi wanavyocheza mpira Chamazi, watu wengi
nikiwemo mimi ningetamani kuona Simba na Yanga wakigusa dimba hilo.
Naamini hali ingekuwa ngumu kwa wakongwe hao.
Wangehangaika kupata matokeo kama inavyowatokea kwenye baadhi ya viwanja kama
vile Sokoine Mbeya, Jamhuri Morogoro na Mkwakwani Tanga.
Kwa bahati mbaya zaidi wangekutana na timu bora
ikiwa nyumbani kwake. Lakini kwasababu haiwezekani ndio basi tena.
Simba na Yanga zina mashabiki wengi mno, uwanja wa
Chamazi unachukua watazamaji wachache, hivyo inalazimu mechi zote
zinazowakutanisha Azam dhidi ya Simba au Yanga kuchezwa uwanja wa Taifa.
Lakini sifa lazima ziwaendee Azam fc, wamekuwa
bora wanapocheza nyumbani kwao na ndivyo inatakiwa kuwa.
Usifanye makosa nyumbani, najua mpira umebadilika
siku hizi, timu inaweza kushinda nyumbani na ugenini, lakini bado uwanja wa
nyumbani una faida nyingi.
Hata ulaya, ni ngumu sana kushinda ugenini
kwasababu wenyeji wanakuwa na faida nyingi ikiwemo idadi ya mashabiki.
Kwa jinsi Azam walivyo na kikosi kikubwa,
wanavyojiamini nyumbani kwao, wataendelea kuzichapa timu za ligi kuu mpaka pale
zitakapojipanga kimbinu zaidi.
0 comments:
Post a Comment