
KLABU za Simba na Yanga zimekaa kwa muda mrefu
katika medani ya soka la Tanzania na kuwa kama ‘Tunu’ ya Taifa hili lenye
mipango mibovu katika misingi ya uendeshaji wa mpira wa miguu.
Licha ya klabu hizi mbili kuwa na umri wa miaka
zaidi ya 70 kwa sasa, bado hazijaweza kufanikiwa kwa ngazi ya kimataifa. Zimekuwa
‘Tia maji’ sana linapofika soka la ushindani.
Timu mpaka leo hazina hata viwanja vya mazoezi,
hazina mfumo mzuri wa uuzaji wa jezi, hazina akademi wala kitu chochote cha
maana.
Sio kwamba hazina wachezaji wazuri, mabenchi ya
ufundi na rasilimali, hapana! . Matatizo yao ni mengi, lakini kubwa ni kwenye
utawala.
Viongozi wao wengi wanaendesha mpira watakavyo
wao, wanaendesha kwa mahaba bila kujali ueledi. Kifupi, siasa imetawala na watu
wasiokuwa sahihi wanapewa mamlaka ya kufanya maamuzi ya kitaalamu klabuni.
Safari ndefu ya klabu hizi haijapata mafanikio
mpaka tunapozungumza leo hii. Kwa bahati mbaya sana, klabu nyingine zinaiga
siasa za Simba na Yanga.
Utawala mbovu unazitafuna klabu za Tanzania. Kwa
mfano timu nyingi za majeshi zinalalamikiwa na makocha wengi .
Tatizo linaloelezwa sana ni viongozi wasiokuwa na
utaalamu wa mpira kuingilia masuala ya kiufundi. Ni ajabu kuona katibu mkuu wa
timu, ambaye hajui lolote kuhusu mpira, anaingilia kazi ya kocha. Anataka
mchezaji fulani asajiliwe kwa matakwa yake, halafu mbaya zaidi analazimisha
acheze.
Migogoro mingi baina ya makocha na viongozi
inatokana na kuingiliana katika makujumu. Kocha anaweza kujikuta umepewa timu
yenye wachezaji asiowataka, kuna soka hapo?
Kumekuwa na ladha ya mabadiliko katika soka la Tanzania
hususani ngazi ya klabu, zimekuja timu zenye mapinduzi kama Mbeya City fc na
Azam fc.
Azam ni timu inayojadiliwa sana na imeaminiwa kuwa
ina malengo ya kuleta mabadiliko ya soka la Tanzania kuanzia ngazi ya mabenchi
ya ufundi, usajili wa wachezaji na utawala.
Hii ni timu iliyoanza vizuri na kuonekana
kuendeshwa vizuri, lakini dhahiri kuna dosari za ndani sana ambazo si rahisi
kuzijua.
Klabu inamilikiwa na watu wenye hela, na bahati
nzuri wana nia ya dhati kuleta mapinduzi ya soka. Wametoa mabilioni ya fedha
kujenga uwanja wa kisasa wenye vifaa vyote na wametoa mabilioni mengine
kudhamini ligi kuu.
Hapa unaona kabisa wamiliki wa Azam fc wana nia ya
kubadili soka la Tanzania na wanapenda sana klabu hii kuwa mfano. Wanataka
iendeshwe kitaalamu na kufikia ngazi za juu.

Wamiliki wa Azam kila wanaloshauriwa ni wepesi
kutekeleza, hawana longo-longo. Wakiambiwa mchezaji fulani anafaa, basi wanatoa
hela za kumsajili.
Lakini tatizo lipo pale pale, wale watawala
wanaoshauri mambo ya kiufundi, kweli wana ueledi wa soka? Jibu ni hapana!.
Waliowengi hawana utaalamu wowote na wanajifanyia mambo kwa vile wamepewa
nafasi tu.
Azam wana tatizo la kiutawala, hilo linajulikana
na ndio chanzo cha kufanya vibaya na wasipochukua maamuzi magumu, basi
watajikuta wanawekeza fedha nyingi, lakini wanaishia kushindana na Simba au
Yanga.
Kiukweli, Azam sio klabu ya ngazi hizo, kwasababu
imewekeza na kujijenga mno, hivyo inatakiwa kuwa na malengo ya mbali kama TP
Mazembe.
Binafsi, nawalaumu baadhi ya viongozi wa Azam kwa
kuliingilia benchi la ufundi na kulazimisha makocha wapange wachezaji fulani.
Jambo kama hili limezitafuna kwa kiasi kikubwa Simba na Yanga.
Kuna watu ambao wana uhusiano na wamiliki wa Azam,
hivyo wanatumia fursa hiyo kuingilia mipango ya benchi la ufundi wakati wao
hawana utaalamu wala ufundi wowote wa mpira na hawajawahi kucheza hata ‘chandimu’
zaidi ya kusoma kwenye mtandao.

Watu hawa wanajifanya wanajua mpira, kumbe hawajui
kabisa. Wanashinikiza wayapendayo wao na wamekuwa wakiwashauri vibaya wamiliki
wa timu.
Watu wanatumia
ufundi wa kuangalia mpira kwenye TV. Kwasababu tu wameona mpira unavyochezwa
uwanjani, wametafakari kwa mawazo yao na kuchanganya ya kwenye mtandao, wanajiona
kama wataalamu wa soka.
Mwisho wa siku wanatoa ushauri ‘bomu’ kabisa kwa
wamiliki wa timu na wamejikuta kuwa mstari wa mbele kuiharibu Azam inayopewa
heshima kubwa ya kubadili soka la nchi hii.
Watawala hawa wasiokuwa na ueledi, wamekuwa wakisajili
wachezaji wao, wanatoa mapendekezo kwa wenye timu, wakitaka wachezaji gani
wasajiliwe. Hatutaji majina, lakini itakapobidi tutawataja tu ili wajirekebishe
na wawaachie walimu watoe mawazo yao.
Azam wasitake kushindana na Simba au Yanga, kwasababu wao ni timu kubwa ambayo nchi nzima
inaiangalia kama ndiye mkombozi wa soka la Tanzania.
Wao wanatakiwa kusimamia na kuendesha mambo yao
kiueledi ili waonekane mfano wa kuigwa. Sasa hivi sio kwamba wana uwezo kuliko
timu nyingine, bali kinachowabeba ni msuli wa hela.
Wana timu ambayo inamilikiwa na matajiri. Kwa
bahati nzuri kila wanapoambiwa kitu wako radhi kutoa hela. Mfano mchezaji
waliyemsajili kutoka Mali, Ismail Diarra ni kuwadanganya ‘mabosi’ tu, nadhani kuna
kitu kingine katikati zaidi ya mpira.
Bahati mbaya zaidi watu hawa ni wachache tu,
wanaleta mambo ya Kiswahili kama ya Simba na Yanga, wakati Azam wanatakiwa kuwa
na mfumo wa kisasa.
Viwanda vya Bakhresa vinaendeshwa kwa kuajiri
wataalamu kutoka India, Italia. Kuajiri wataalamu hawa kutoka nje ni ueledi.
Kama wanaweza kufanya hivyo kwa viwanda, basi na timu
iwe vivyo hivyo, watafute wataalamu ili waiendeshe katika misingi ya taaluma
kama kweli wanataka iwe taasisi inayojitegemea.
Sisi tunafanya kazi kubwa zaidi kuwekeza katika
mabenchi ya ufundi, lakini tunasahau eneo lingine la upande wa utawala.
Kwa watu wanaotaka mabadiliko katika soka la
Tanzania wanawategemea Azam fc, lakini kuna watu wachache wanaharibu mambo kwa
kuendekeza maslahi binafsi na mahaba kwa baadhi ya mambo ya msingi.
Timu inaaminiwa na watu, inakwenda kucheza ligi ya
mabingwa na timu kama TP Mazembe, Esperance na nyingine. Kinachotakiwa ni
kujikita zaidi huko na sio kuangalia kuifunga Simba au Yanga. Kama wamefanikiwa
kuchukua ubingwa, basi wajipange zaidi kwa ajili ya ligi ya mabingwa.
Benchi la ufundi liko vizuri, lakini tatizo ni
mambo ya utawala. Wakiweza kurekebisha hilo, Azam itakuwa mfano wa kuigwa.
Kwa mfano mambo ya rushwa yamekuwa yakijitokeza.
Juzi walipofungwa na Yanga mabao 3-0 katika mchezo wa Ngao ya Jamii, kuna wachezaji
wamekuwa wakilalamikiwa chini kwa chini. Azam fc wasitafute mchawi, mchawi ni
wao wenyewe. Wamefungwa na Yanga kihalali.
Wanaanza sijui Sure boy, Kavumbagu, Mwadini wamechukua
hela, sio kweli. Wanatakiwa kuacha kuwafanya wachezaji kama kivuli cha
kukimbilia pale wanapofanya vibaya.
Ukitaka kujua kuwa viongozi ndio wenye matatizo,
kumbuka lile sakata la akina Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Said Mourad na kipa
Deogratius Munish ‘Dida’.
Walisema wachezaji hawa wamehujumu mechi moj dhidi
ya Simba sc. Wakaweka watu wa kuwachunguza na kupeleka kesi TAKUKURU, lakini
hawakupatikana na kosa hilo na mpaka leo wamebaki kuwa wachezaji wa kutegemewa.
Wachezaji hawakuwa na tatizo, wenye tatizo ni
viongozi. Kwahiyo kinachotakiwa kufanyika ni kujitathimini, kujitafakari,
halafu kujiongeza.
Katika kujitafakari; wanatakiwa kukaa chini upya,
kurejea mipango yao mama na kujikumbusha kuwa wana safari gani mbele yao.
Baada ya hapo wajitathimini ili wajue kama
wamefanikiwa japo hata kidogo katika mipango yao na wajue mapungufu yako wapi.
Kama wanaona kuna matatizo wanatakiwa kujipanga
upya. Cha msingi wabaini matatizo yako wapi na kuja kivingine.
Wakishajua matatizo yao, basi wajiongeze kwa maana
ya kufanya maamuzi magumu hususani katika suala la utawala linaloonekana kuwa
na matatizo. Hapa wamelundikana watu
wasiokuwa na ueledi na mpira na wanaaminiwa na wamiliki wa timu.
Hao ndio wachawi wa Azam fc. Kinachotakiwa ni
kutafakari kwa kina suala la utawala, watathimini mapungufu yao na kukubali
kutafuta watu wenye taalamu ya mpira hata kutoka nje.
Kama wamiliki watapata watu wenye taaluma katika
utawala wa mpira na kuwekeza hela kama walivyofanya kwenye miundombinu,
wachezaji na makocha, basi Azam itafika mbali.
Lakini kama wataendelea kuwakumbatia watu hawa
wachache wasiokuwa na taaluma, basi timu itajikuta iko pale pale na itaishi
miaka mingi kama Simba na Yanga bila kuwa na kitu cha kujivunia.
Tafakari! Chukua hatua! Nawatakiwa siku njema!.
Chanzo:shaffihdauda.com
0 comments:
Post a Comment