Aliyekuwa Rais wa TFF, Leodigar Chila Tenga alikuwa mchezaji muhimu wa Taifa Stars miaka ya 1980
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
HISTORIA inaonesha kuwa zamani mpira
wa miguu ulikuwa unachezwa kutoka ngazi ya chini mpaka juu na walipatikana
wachezaji wengi wa kulisaidia taifa.
Taifa Stars iliyoshiriki michuano ya
mataifa ya Afrika nchini Nigeria miaka ya 1980, ni ushahidi tosha juu ya suala
hilo.
Katika kipindi hicho kisichosahaulika
miongoni mwa wadau wengi wa soka nchini, wachezaji waliounda Taifa Stars walitoka timu mbalimbali za chini na za juu.
Klabu kubwa za Simba na Yanga hazikutoa wachezaji wake kwa asilimia kubwa.
Leo hii klabu moja inakuwa na
wachezaji 6, 8 mpaka 10 katika kikosi cha Taifa Stars. Zamani haikuwa hivi,
Simba na Yanga miaka ya 80 wakati Stars ikiifunga Kenya, Harambee Stars 5-0 zilitoa
wachezaji wanne tu (kila timu wawili).
Hii ilitokana na kuwepo wachezaji
wengi sana. Makocha wa Stars walikuwa na wigo mpana wa kuteua wachezaji kutoka
klabu mbalimbali hadi za daraja la pili. Mashindano yalikuwa mengi mno kuanzia
chini na mpira ulipigwa kila kona ya nchi.
Leo hii mambo ni tofauti kabisa, mpira
hauchezwi kwa misingi mizuri. Hakuna mashindano mengi maalumu. Taifa Stars inategemea
wachezaji kutoka Yanga, Simba na Azam fc.
Kutokana na mazingira hayo, wachezaji
wamebaki walewale kila siku. Leo hii kocha wa Stars, Mart Nooij akimuacha
Mrisho Ngassa, unadhani ni mchezaji gani mwenye kiwango cha juu atabadili
nafasi yake?
Nani anaweza kurithi vizuri nafasi ya
Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbwana Samatta au Thomas Ulimwengu? Makocha
wamejikuta hawana machaguo kwasababu ndio wachezaji waliopo katika kiwango cha
juu kwasasa.
Taifa Stars enzi hizo ilikuwa moto wa kuotea mbali
Kocha amekosa wigo mpana wa kuchagua
wachezaji wa Stars, lakini zamani kocha alikuwa anaamua mwenyewe amchukue
mchezaji wa aina gani na haikuwa lazima kuzifikiria Simba na Yanga .
Ukweli ni kwamba wachezaji wengi ambao
waliibuka na kuwa nyota wa Tanzania
walitoka ligi za mchangani.
Ligi hizi zilikuwa na ushindani na
hamasa kubwa, kwahiyo Dr Mwaka Sports Xtra Ndondo Cup inajaribu kurudisha hali
hiyo na kutoa fursa kwa vipaji vingi vilivyopo mtaani na kuvipatia jukwaa la
kuonekana.
Haya sio mawazo mpya, tayari yalishafanyika
huko nyuma, lakini michuano hii inakuja kwa ‘staili’ nyingine ya kileo na
itatangazwa.
Wachezaji bora wa mashindano
watapatikana na kutafutiwa njia ya kuweza kuwaendeleza.
Pia lengo ni kuzitengenezea klabu kubwa
sehemu ya kutafuta wachezaji wapya kuliko kusajili hovyo hovyo. Kwasasa hakuna
wigo mpana wa kusajili wachezaji, hivyo michuano hii inataka kuibua vipaji
vingi vilivyopo mitaani.
Kwa mfano Mtibwa Sugar kila mwaka
inauza wachezaji, lakini bado inaendelea kuwepo na kutafuta vipaji vipya kutoka
mchangani. Wachezaji wapo wengi, lakini hakuna mashindano.
Kutokana na mazingira haya, Sports Xtra
ya Clouds fm imeamua kuanzisha mashindano yanayokwenda kwa jina la DR MWAKA
SPORTS XTRA NDONDO CUP.
Michuano hii itakayoendeshwa kwa mfumo
wa kisasa kabisa itashirikisha wachezaji wa mchangani kutoka timu 32.
Kivumbi kinatarajia kuanza Septemba 27 mwaka huu ambapo mechi ya
ufunguzi itawakutanisha Friend’s Rangers
na Kiluvya United katika uwanja wa Makulumla, Magomeni, Dar es salaam, majira
ya saa 10:00 jioni.
Mbali na dimba la Makulumla, viwanja vingine
vitakavyotumika katika mashindano hayo ni Kinesi (Shekilango), Benjamini Mkapa
(Ilala) na Mizinga (Kigamboni).
Timu 32 zitakazoshiriki zimepangwa
katika makundi nane yenye timu nne.
Kundi A: Boom fc, Beira Hotspurs,
Tabata fc na Tuamoyo
Kund B: Sifa Politani, Vijana Ilala,
Kijichi, Micco Villa
Kundi C: Friend’s Rangers, Temeke
Market, Kiluvya United na Muheza fc
Kundi D: Ukonga United, Sinza Stars,
Congo Shooting na Snow White
Kundi E: Zakhem, Black Six, TP Same na
Makumba
Kundi F: Villa Squad, Scud fc, Nyota
Afrika na Burudani fc
Kundi H: Stakishari fc, Abajalo,
Shelaton na Kimara United
Kundi G: Temeke United, Sifa United,
Forteagle na Segerea fc.
0 comments:
Post a Comment