
Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba sc, Zacharia Hans Poppe
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
MASHABIKI na wadau wengi wa soka nchini Tanzania wanapenda sana kuona mpira wa miguu unapiga hatua na kufikia kiwango cha juu kama ilivyo kwa baadhi ya mataifa ya Afrika hususani Afrika Magharibu.
Ni ukweli kuwa soka halina njia ya mkato kufikia malengo.
Lazima kuwepo na mfumo sahihi wa kutunza na kuendeleza vipaji vya soka hasa
soka la vijana na mfumo mzuri wa uongozi au utawala.
Nchi nyingi zilizoendelea katika soka duniani kama
vile Hispania, Uholanzi, Ujerumani, Brazil na nyinginezo zimeweka watu sahihi
katika maeneo sahihi.
Waliandaa mpango mkatati wa kitaifa kwa soka la
vijana na kutekelezwa kwa ufanisi na hatimaye wamefika hapo walipo.
Soka la Tanzania kiukweli lina changamoto nyingi
kuanzia mfumo mzima wa kutunza vipaji, uongozi wa vyama na klabu kuanzia madaraja
ya chini mpaka juu.
Simba na Yanga ni klabu mbili zinazobeba
utambulisho wa Tanzania kimataifa. Azam wameanza kuja kwa mbali na kadiri miaka
inavyokwenda wanazidi kujitangaza kimataifa kutokana na uwekezaji mkubwa
walionao katika soka na mfumo mzuri wa utawala.
Huwezi kuzungumzia Soka la Bongo usitaje Simba na
Yanga. Hizi ni klabu zinazochukuliwa kama ‘’Tunu’ ya Taifa.

Atatisha tena?: Mfungaji bora wa ligi kuu soka Tanzania Bara Msimu uliopita, Mrundi, Amiss Tambwe
Lakini kuna changamoto nyingi sana katika klabu
hizi ambazo kwa asilimia kubwa zinachangia wachezaji wa timu ya taifa ya
Tanzania, ‘Taifa Stars’.
Kuna mitazamo mingi juu ya klabu hizi na kila mtu
anakosoa kadiri awezavyo, lakini waliowengi wakati fulani huendeshwa na
mitazamo binafsi, masilahi binafsi, chuki na kutumiwa na watu.
Najua yapo mapungufu mengi katika klabu hizi
kuanzia utawala na namna wachezaji wanavyopatikana, lakini kuna wakati fulani
viongozi wa timu hizi wanalazimika kufanya kazi kwa kutumia mazoea au
kulazimishwa na mfumo uliopo katika soka letu.
Mara nyingi nimekuwa nikiandika kuwashauri
viongozi wa Simba na Yanga kuanzisha mfumo na falsafa rasmi ya klabu hizo. Kuna
haja ya kujenga misingi bora ya soka la vijana ili kupata muendelezo wa
wachezaji.
Klabu kama Barcelona imefanikiwa sana kwa kuwekeza
katika soka la vijana, siwezi kuifananisha na Simba au Yanga kwasababu kuna
utofauti mkubwa wa uchumi baina ya timu hizi.
Kuna wakati mimi napinga sana kufafanisha soka la
Ulaya na Tanzania. Wenzetu wameendelea miaka mingi iliyopita na wamewekeza
fedha nyingi katika soka la Tanzania. Lakini kuiga baadhi ya mambo na kwenda
nayo ‘Mdogo mdogo’ sina tatizo hapo, ni muhimu sana.
Kutokana na uwezo wao wa kiuchumi wanaweza
kuwatunza vijana kwa muda wote, lakini kutokana na hali ya uchumi wa Simba na
Yanga, bado kuna tatizo la kuwatunza na kuwaendeleza vijana na kwa bahati mbaya
klabu hizo hazina akademi.
Ataendeleza jitihada za soka la vijana?: Makamu wa Rais wa Simba sc, Geofrey Nyange 'Kaburu'
Naamini katika klabu ya Simba kuna watu wenye
mitazamo mizuri katika soka la vijana kama vile makamu wa Rais wa Simba,
Geofrey Nyange ‘Kaburu’.
Kaburu ni mtu ninayemkubali sana inapofika hoja ya
soka la vijana. Katika uongozi wa Ismail Aden Rage alijitahidi kuboresha soka
la vijana akisaidiana na watu kama kocha Suleiman Abdallah Matola ‘Veron’ na
mjumbe wa kamati ya ufundi kwa wakati huo, Ibrahim Masoud ‘Maestro’.
Mpango ule ulizalisha vijana wengi ambao
wanatumika kwa sasa, mfano Haroun Athuman Chanongo, Ramadhan Singano ‘Messi’,
Wilium Lucian ‘Gallas’, Said Ndemla na wengineo.
Kuna wakati mipango ya akina Kaburu ‘inafeli’
kwasababu ya uwezo mdogo wa klabu kiuchumi. Naamini kuna baadhi ya mambo
yanafanyika kwa watu binfasi kutumia fedha zao za mfukoni, na kwasababu mtu
anaweza kuwa nacho leo na kesho akakosa, basi mambo yanaharibika.
Kwa bahati mbaya sana watu wengi wanakosoa bila
kutoa hoja mbadala. Leo hii mtu anafanya jitihada binafsi kuisaidia Simba au Yanga
kwa kutumia fedha zake, watu hawaheshimu, bali wanakazania kukosoa kila kitu.
Wengine watakuja?: Ramadhan Singano 'Messi' (kushoto) ni zao za soka la vijana Simba sc
Kama mtu anakosoa mfumo mbaya uliopo Simba na
Yanga na taifa zima huwa namuunga mkono kwa asilimia ‘800’, lakini linapokuja
suala la mtu binafsi hususani anayesaidia mambo muhimu kwenda siungi mkono.
Kwa muda mrefu sasa, Simba inawetegemea wafadhili
kuendesha mambo yake hususani kundi la Marafiki wa Simba ‘Friends of Simba,
F.O.S’.
Kuhusu kundi hili kila mtu anasema lake, wapo
wanaosema lina maana kubwa Simba na wengine wanadai linaitumia klabu kujipatia
masilahi binafsi.
Hii ni mitazamo tu. Unajua wanapoishi wengi huwa
kunakuwa na mitazamo tofauti. Kila mtu anatoa hoja zake na kutetea. Wanaosema
F.O.S hawafai wana hoja zao na wanaosema wanafaa wana hoja zao.
Kinachoonekana ni kutofautiana mitazamo, na sio
dhambi, lakini siku zote kama watu wanatofautiana kitu fulani, ujue kuna ukweli
upo katikati.
Ukweli huwa unabaki kuwa ukweli tu hata kama
mtatoana povu kubishana. Lakini binafsi naamini kuwa F.O.S ni kundi muhimu sana
kwa klabu ya Simba na lisiangaliwe kwa mtazamo hasi tu bali hata chanya
liangaliwe pia.
Yawezekana wanatumia mfumo mbovu kuisaidia Simba, na
kama tatizo ni mfumo ndio unawafanya wasiaminike kwa baadhi ya watu, hapo sina
tatizo, lakini kusema hawana maana sidhani.

Hebu fikiria watu kama Zacharia Hans Poppe, kwa
uwezo alionao kiuchumi, anaweza kukaa
nje ya Simba bila tatizo lolote, lakini kutokana na kuipenda klabu hii, anajikuta
kila kukicha anaihangaikia.
Ukweli upo wazi, Hans Poppe katoa fedha nyingi
sana na anaendelea kutoa ili kuijenga Simba. Yawezekana watu wanaamini ana
masilahi binfasi, lakini ukweli unabaki kuwa mtu huyu anatoa hela nyingi hata
kuliko anazoweza kuchukua Simba kama watu wanavyodhani.
Leo hii akaunti ya Simba sidhani kama ina fedha
nyingi za kusaidia kila kitu, lakini uwepo wa watu kama Hans Poppe unafanya
mambo muhimu yaende.
Kwasasa usajili unaendelea katika klabu ya Simba,
Hans Poppe ndiye mwenyekiti wa kamati ya usajili. Jitihada zake zinaonekana
wazi, amekuwa akihangaika huku na kule kutafuta wachezaji.
Kwa bahati nzuri kila ninapopata nafasi huwa
nampigia simu keptein huyu wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania kujua
machache kuhusu harakati zake za usajili, hata yeye anaweza kuwa shahidi mzuri
kwa hili.
Ni mtu anayesafiri mara kwa mara kutafuta
wachezaji. Sidhani kama safari zote analipwa na Simba. Ni mapenzi makubwa
aliyonayo katika klabu hiyo, ni mwanachama halisi, anatoa bila kusubiri faida
yoyote.
Juzi juzi tu, Hans Poppe alikuwa kushuhudia michuano ya
kombe la Kagame inayoendelea mjini Kigali, Rwanda. Nilijua kuwa lengo la
mwanajeshi huyu wa zamani lilikuwa ni kupepesa macho ili kuona kama anaweza
kupata angalau mchezaji mmoja.
Kitasa: Donald Mosoto anasemekana kuondoka Msimbazi
Kwanini anatafuta mchezaji mwingine? Sababu ni
rahisi tu, kuna mapungufu yapo ambayo si rahisi kuyajua bila kumuuliza yeye kama
mwenyekiti wa kamati ya usajili au benchi la ufundi.
Hans Poppe aliwahi kunieleza kuwa Gilbert Kaze
aliyesajiliwa kutoka Vital’O ya Burundi aliomba kuondoka. Kaze kwa muda mrefu
alisumbuliwa na majeruhi, hivyo Simba wakamruhusu kuondoka kwasababu
asingewasaidia kwa msimu ujao.
Juzi juzi tu nimesikia kuna mchezaji wa kigeni
ambaye ameomba kwenda kucheza soka la kulipwa na taarifa zinaeleza kuwa ni
Donald Mosoto, raia wa Kenya. Simba ninavyoifahamu mimi, ni klabu inayofanya
vizuri linapokuja suala la kuruhusu wachezaji kutafuta maisha sehemu nyingine.
Wachezaji wengi wameenda kutafuta maisha nje ya
nchi kupitia Simba. Mchezaji kama vile Mbwana Samatta, Mwinyi kazimoto wote
walitokea Simba na waliruhusiwa vizuri tu.
Ipo idadi kubwa sana, Henry Joseph Shindika,
Haruna Moshi, Shaaban Kisiga, Dani Mrwanda na wengine wengi walienda kucheza
soka la kulipwa wakitokea Simba.
Simba haina utamaduni wa kuwabania wachezaji, na
ndio maana linapotokea suala la Mosoti kuomba kuondoka, hakuna ubishi hata kama
ni mchezaji muhimu.
Kwa kuzingatia upungufu unaoenda kujitokeza, Hans
Poppe kama mwenyekiti wa kamati ya usajili alishauriana na wenzake (sina
uhakika na benchi la ufundi) kuwa aende Kagame kutafuta mbadala wa Mosoti.
Katika mashindano haya yanayoendelea Kigali, Mkurugenzi
wa zamani wa ufundi wa TFF, Sunday Kayuni yupo. Hans Poppe alimuona beki mmoja
wa klabu ya Telcom ya Djibout, Butoyi Hussein.
Hakuwa na muda wa kupoteza, akajaribu kumuuliza
mtaalamu Kayuni ambaye alimhakikishia kuwa ni beki mzuri kwasababu alionekana
kucheza vizuri.
Inawezekana timu inayochezea haina kiwango kizuri
na haikufika mbali, lakini kuna jambo moja katika mpira linaitwa kipaji binafsi
‘Individual Talent’. Timu inaweza isiwe nzuri, lakini mchezaji mmoja akawa
mzuri.
Ndio maana TP Mazembe walimuona Samatta akiwa na
timu ya Simba ambayo haikufika mbali. Wakamsajili na anawasaidia mpaka sasa.
Mazembe hawakuangalia kiwango cha Simba kama
klabu, lakini waliangalia uwezo wa Samatta waliyemuona katika mechi mbili,
Lubumbashi na Dar es salaam.

Mbwana Samatta (kushoto) na Patrck Ochan (kulia) waliuzwa TP Mazembe kutokea Simba sc
Kwahiyo kwa suala la Butoyi kuonwa katika mechi
mbili si geni. Anaweza kuwa mchezaji mzuri kwa Simba, ingawa sio lazima.
Baada ya yote, Hans Poppe aliamua kumsafirisha
kuja kufanya majaribo. Maana yake anaweza kusajiliwa au hapana, kutegemeana na
kocha Patrick Phiri atasemaje.
Kwa hili sioni kama Hans Poppe amekosea kwasababu
ndio utaratibu wa timu za Tanzania inapofika kutafuta wachezaji wa kigeni.
Wenzetu wameendelea sana. Ni mara chache
kuwajaribu wachezaji wa kuwasajili, lakini kama wanataka wachezaji vijana wa
kuwaendeleza katika akademi zao, mara zote wanawachukua maeneo mbalimbali
hususani ligi za chini na mashindano ya vijana kisha wanawajaribu na
kuwachukua.
Kwa wachezaji wa timu za kwanza, mara zote
wanasajili moja kwa moja. Wanaweka dau mezani na kukubaliana na timu
inayommiliki na mambo binafsi na mwanandinga huyo, kisha anapimwa afya, akifuzu
anasaini mkataba. Haya yanawezekana kwasababu ya maendeleo makubwa waliyonayo
pamoja na ligi zao kuoneshwa duniani kote.
Kwetu Afrika usajili wa hivi huwa ni mara chache
kufanyika. Huwezi kusema leo hii utaitazama ligi ya Ivory Coast, Mali, Nigeria
na kwingineko kiundani ili kuona wachezaji wa kuwasajili moja kwa moja.
Hakujawa na mfumo wa kuwaona vizuri na njia rahisi
ni kutafuta wachezaji na kuwafanyia majaribio kama wafanyavyo akina Hans Poppe
na kamati yake kwa kushirikiana na benchi la ufundi.

Atarudi rekodi ya 2009?: Kocha mkuu wa Simba Patrick Phiri ndiye mwenye maamuzi ya mwisho juu ya wachezaji
Sioni shida kwa Butoyi kuletwa na Hans Poppe .
Mwenye uwezo wa kujua kama anaweza kutumika ni mtaalamu Patrick Phiri.
Binafsi naheshimu sana jitihada za Hans Poppe
katika usajili wa Simba. Anafanya kazi nzur, lakini nashauri kufanyika jitihada
ili kutafuta mfumo sahihi wa kusajili wachezaji.
Yawezekana isiwe leo wala kesho, lakini mfumo wa
kuwaleta wachezaji wengi wa kigeni, kuwapangia hoteli, kuwalisha chakula,
kuwasafirisha na kuwapa posho wakati wa majaribio sio jambo la kuendelezwa
sana.
Siku za usoni nitatamani Simba ipige hatua na
kuweka watu maalumu wa kuzungukia maeneo tofauti barani Afrika kutafuta
wachezaji na sio kuwaleta kwa ajili ya majaribio.
Siwezi kumpinga Hans Poppe kwasababu mfumo ndio
unamfanya afanye hivyo na asipofanya hivyo, maana yake Simba haitapa wachezaji
wa kigeni.
Kuhusu idadi ya wachezaji wa kigeni kulundikana
Simba au Yanga sio sababu ya kudidimiza soka letu. Hata tusema wachezaji wa
kigeni wasiwepo, soka la Tanzania litabaki kuwa nyuma.
Tatizo la msingi sio idadi ya wachezaji wa kigeni,
tatizo lipo kwenye mfumo wetu. Mbona kuna timu za ligi kuu hazina wachezaji wa
kigeni, lakini haziendelei.
Kama taifa, tunatakiwa kurudi nyuma na kuwa na
mpango mkakati wa kitaifa wa kujenga mfumo imara wa soka la vijana na tukifanya
hivyo na kushindwa kupata mafanikio, basi turudi kujadili wachezaji wa kigeni.
Naamini kama tutarudi kwenye soka la vijana
tutaendelea.
Sina tatizo na Hans Poppe na namna anavyopata
wachezaji, lakini nina tatizo na mfumo mzima wa soka la Tanzania.
Sijui kama
kweli kamati hizi za usajili kwa asilimia mia moja zinasajili kwa matakwa ya
mabenchi ya ufundi. Kuna wakati malalamiko yanasikika kutoka kwa makocha,
lakini haya yanatokea kutokana na mfumo wetu mbovu.
Wachezaji wa kigeni waliopo Simba mpaka sasa ni Mganda
Joseph Owino, Wakenya, Donald Mosoti na Paul Kiongera. Pia wapo Warundi wawili,
Amiss Tambwe na Pierre Kwizera.
Tayari Simba imekamilisha idadi ya wachezaji wa
kigeni, lakini mwenyekiyi wa Kamati ya usajili Zacharia Hans Poppe amesema kuna
mchezaji mmoja ameomba kuondoka, hivyo kama Butoyi atafuzu majaribio atapewa mkataba.
0 comments:
Post a Comment