Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Julai 23, 2014, saa 1:57 usiku
WANANDINGA wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars
wana matumaini ya kuwafunga Msumbiji (Black Mambas) katika mechi ya marudiano itakayopigwa
kati ya Agosti 2 na 3 mwaka huu kwenye uwanja wa taifa wa Zimpeto mjini Maputo.
Taifa stars ilitoka sare ya mabao 2-2 mwishoni mwa
wiki iliyopita dhidi ya Mambas ndani ya dimba la Taifa jijini Dar es salaam,
hivyo wanahitaji ushindi wa mabao 1-0 au sare ya mabao 3-3 ili kufuzu hatua ya
makundi kusaka tiketi ya kucheza fainali za mataifa ya Africa, AFCON, nchini Morocco.
Mlinda mlango namba mbili wa Stars ambaye katika
mechi iliyopita alikaa benchi, Aishi Manula amesema kama kama Msumbiji
walipata mabao mawili Dar es salaam nao
wanaweza kupata ushindi mjini Maputo.
“Watanzania wakitulaumu ni sahihi, wakati fulani sio
sahihi kwasababu mpira ni mchezo wa makosa. Ili tufunge lazima Msumbuji wafanye
makosa na ili wao wafunge, lazima sisi tufanye makosa”. Alisema Manula.
“Tutajipanga vizuri, wao wameweza kupata mabao
mawili kwetu, sisi tunapoenda Msumbiji tutahitaji kupata bao la mapema. Tukishinda
ushindi wowote hata moja bila tutasonga mbele”. Aliongeza Manula.
Mlinda mlango namba mbili wa Taifa Stars, Aishi Manula
Aidha, mlinda mlango huyo wa Azam fc aliongeza
kuwa mpira wa miguu wakati fulani unakwenda na bahati, hivyo Mungu ndiye anajua
nini watavuna ugenini.
“Watu wanafikiria tofauti, lakini huwezi kujua
nini Mungu ametuandalia . Tuwaombe watanzania waendelea kutuamini kwasababu timu
yetu ilivyo, inaweza kupata matokeo mazuri”.
“Makosa madogo madogo yaliyotokea yanaweza
kurekebishika na tukafanya vizuri”. Alisisitiza Manula.
Kikosi cha Taifa Stars kinatarajia kuondoka kesho
(Julai 24 mwaka huu) kwenda Mbeya ambapo kitapiga kambi ya wiki moja kujiandaa
kwa mechi ya marudiano dhidi ya Msumbiji.
Mechi hiyo ya raundi ya pili ya michuano ya
Afrika kutafuta tiketi ya kushiriki Fainali za Afrika (AFCON) zitakazochezwa
mwakani nchini Morocco itafanyika wikiendi ya Agosti 2 na 3 mwaka huu nchini
Msumbiji.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro
Premium Lager itaondoka nchini Julai 31 mwaka huu kwenda Johannesburg, Afrika
Kusini ambapo itafanya mazoezi ya mwisho kabla ya kutua Maputo kwa ajili ya
mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Taifa wa Zimpeto.
0 comments:
Post a Comment