TAARIFA za chini ya kapeti ambazo mtandao huu
umezipa kutoka chanzo cha uhakika, uongozi wa klabu ya Simba chini ya rais,
Evans Aveva umedhamiria kumtimua kocha mkuu wa klabu hiyo, Mcroatia, Zdravko
Logarusic.
Sababu kubwa iliyoelezwa na chanzo hicho makini ni
kuwa Loga amekuwa akiwasumbua viongozi wa klabu hiyo kwa kukataa wachezaji
wanaoletwa na viongozi kwa ajili ya kusajiliwa.
Simba wapo katika harakati za kuimarisha kikosi
chao, lakini Loga amekuwa akiwapiga chini wachezaji wanaoletwa na viongozi kwa
madai kuwa hawana viwango vizuri.
Hata hivyo mtandao huu umepenya ndani na kujua
kuwa Loga amekuwa na msimamo mkali kwa viongozi hao akihitaji kuchagua mwenyewe
wachezaji.
Kwa siku nyingi, kundi maarufu katika klabu ya Simba,
Friends of Simba (F.O.S) linaloundwa na mamilionea, limekuwa likishutumiwa
kuwapangia makocha wachezaji wa kusajiliwa na kupangwa kucheza katika mechi.
Aliyekuwa kocha mkuu wa klabu hiyo kabla ya kuja kwa Mfaransa Patrick Liewig,
Mserbia, Milovan Circovic aliwahi kulalamika kuwa viongozi wa wakati ule
walioongozwa na mwenyekiti Ismail Aden Rage na makamu mwenyekiti, Geofrey
Nyange `Kaburu` walikuwa wanaingilia upangaji wa kikosi chake.
Milovan alieleza kuwa viongozi ambao ni wanachama
wa kundi la F.O.S walikuwa wanampangia wachezaji wa kucheza kinyume na taratibu
za ualimu.
Kukosa uhuru kwa makocha katika upangaji wa
kikosi, ni kinyume na mpira wa kisasa unaomtaka kocha kuwa mwamuzi wa mwisho
kujua nani anacheza na nani hatacheza.
Mbali na kuwapangia makocha wachezaji wa kucheza,
pia kundi hili limekuwa likiingilia mchakato wa usajili na kuleta wachezaji
wasiokuwepo kwenye mipango ya kocha.
Kitaalamu, kocha ndiye mwenye mamlaka ya kuamua
mchezaji gani asajiliwe na nani aachwe. Lakini kwa klabu mbili za Simba na
Yanga, kuna baadhi ya wachezaji wanaletwa na viongozi na sio matakwa ya benchi
la ufundi.
Kwa taarifa za uhakika, Simba wapo katika
mazungumzo na kocha wa Gor Mahia ya Kenya, Bobby Williamson.
Kabla ya kuja kwa Loga, Williamson alikuwa katika
rada za Simba baada ya kuacha kazi ya kuifundisha timu ya Taifa ya Uganda, The
Cranes.
Mtandao huu unafuatilia kwa kina suala hilo ili
kujua nini hatima yake.
0 comments:
Post a Comment