Kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime
Na Baraka Mpenja, Dar e salaam
Imechapishwa Julai 25, 2014, saa 5:50 asubuhi
MTIBWA sugar kila mwaka inabomolewa na timu
nyingine za ligi kuu soka Tanzania bara kwa kuwasajili wachezaji wengi muhimu
wanaong`ara klabuni hapo.
Kocha mkuu wa klabu hiyo, Mzalendo, Mecky Mexime
amesema amejikuta kila mwaka anakuwa na kazi ya kujenga upya timu, kwasababu
msimu unapoisha, wachezaji watatu au wanne wa kikosi cha kwanza wananunuliwa na
timu nyingine zikiwemo Simba na Yanga.
“Timu nyingi zinaangalia kwetu Mtibwa, kila mwaka
tunabomolewa, kila mwaka unajenga upya timu, kwasababu wanaondoka wachezaji
watatu wanne, tena wachezaji muhimu”. Alisema Mexime.
“Sisi hatusajili wachezaji wa gharama, tunatafuta
vijana wadogo na kuwajenga, lakini unakuta mwakani wamenunuliwa tena”.
Beki huyo na Nahodha wa zamani wa Mtibwa na timu
ya taifa ya Tanzania , Taifa Stars alikiri kuwa kutengeneza upya timu ni jambo
gumu, lakini amekuwa akijitahidi kila msimu kuja na vijana wapya.
Kuhusu maandalizi ya ligi kuu, Mexime alisema wana
siku ya tatu tangu waanze kujifua jijini Dar es salaam, na wanamshukuru Mungu
wanaendelea vizuri.
“Namshkuru mwenyezi mungu mazoezi yanakwenda
vizuri na ninamuomba mwenyezi mungu awape wachezaji nguvu ili waweze kuyapokeza
vizuri mafundisho” . Alisema Mexime.
Pia kocha huyo alisema wakati huu wa maandalizi
wanahitaji mechi za kirafiki ili kujipima uwezo wao na Agosti 8 mwaka huu
amethibitisha kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Azam fc ndani ya dimba la
Taifa jijini Dar es salaam.
Siku za karibuni, Simba ilimsajili mlinda mlango
nambo moja wa Mtibwa Sugar, Hussein Sharrif `Casillas`, lakini Mexime alisema
kipa huyo hajaondoka na Mtibwa, hivyo watasajili kipa mwingine.
Kwa muda mrefu Mtibwa imekuwa kitalu cha kuzalisha
wachezaji wanaochukuliwa na timu za Simba na Yanga, kwa mfano Hussein Javu,
Said Bahanuzi waliojiunga na Yanga wakitokea Mtibwa.
Wapo wachezaji wengi waliotokea Mtibwa na kujiunga
na timu za Simba na Yanga, kama vile Mussa Hassan Mgosi, Juma Kaseja, hivyo ni
kweli kuwa klabu hiyo imekuwa ikibomolewa mara nyingi.
0 comments:
Post a Comment