Na Baraka Mpenja, Dar es saalam
Imechapishwa Julai 22, 2014, saa 3:36 asubuhi
MSIMU uliopita wa ligi kuu soka Tanzania bara, Juma
Mwambusi wa Mbeya City fc alichaguliwa kuwa kocha bora wa msimu baada ya
kuiongoza klabu hiyo mpya kushika nafasi ya tatu katika msimamo.
Mbeya City fc walizisumbua klabu kubwa za Simba na
Yanga, hata mabingwa Azam fc. Walimaliza nafasi ya tatu mbele ya mnyama Simba
kwa kujikusanyia pointi 49 kibindoni.
Walishinda mechi 13, wakatoka sare mechi 10 na
kufungwa mechi 3. Walikula kipigo cha kwanza cha bao 1-0 kutoka kwa Yanga ndani
ya uwanja wa Taifa. Wakalala 2-0 dhidi ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union,
Mkwakwani Tanga. Na mechi ya tatu kufungwa ni ile ya 2-1 dhidi ya Azam fc.
Mechi hii ilipigwa uwanja wa Sokoine na kimsingi
ndio iliamua ubingwa kutua mikononi mwa wana Lambalamba.
Mwambusi ni kocha maarufu nchini, kila timu
anayoifundisha inapata mafanikio. Kumbuka alipokuwa na wajelajela Tanzania
Prisons hali ilikuwaje.
Msimu uliopita, Mwambusi alikuja na kikosi chenye
wachezaji wapya kabisa katika michuano ya ligi. Walikuwa vijana wadogo wasio na
uzoefu, lakini aliwaamini kwasababu alitoka nao ligi daraja la kwanza ambapo
alipanda kucheza ligi kuu bila kufungwa mchezo wowote.
Mwambusi ni mtu wa kuthubutu na ukizingatia nyuma
yale alikuwepo msaidizi imara, Maka Andrew Mwalwisyi, ingawa kocha huyu mwenye
leseni B ya CAF ameamua kuachana na klabu hiyo.
Anapotajwa kuwa kocha bora wa msimu, manake
aliwazidi wenzake mbinu . Mwambusi alikuwa na timu changa na alipambana na
makocha wenye timu kubwa kama Hans van Pluijm (aliyekuwa kocha wa Yanga),
Joseph Marius Omog wa Azam na Zdravko Logarusic wa Simba.
Wakati Omog, Pluijm, na Loga wakiwa na wachezaji
wa kimataifa katika vikosi vyao, Mwambusi alikuwa na vijana wa Kitanzani, tena
wengi wao wanatoka nyanda za juu kusini, hususani Mbeya.
Kwa mafanikio aliyopata kuzingatia timu aliyokuwa
nayo, tuzo ya kocha bora ilimfaa.
Lakini Mwambusi anatambua ugumu uliopo mbele yake
baada ya kuwa kocha bora msimu uliopita?
Kocha huyu anasema msimu ujao utakuwa na
changamoto kubwa kwake kwasabababu timu zote zinajiandaa na yeye ataingia kama
mshindani wa ubingwa, huku akiamini kuwa timu zitacheza naye kwa nguvu kama
ilivyo kwa Simba, Yanga na Azam fc.
Kocha wa Mbeya City fc, Juma Mwambusi (katikati) akizungumza na wachezaji wake Hassan Mwasapili (kushoto) na Peter Richard (kulia).
Mwambusi aliongeza kuwa maandalizi ya msimu mpya
yanakwenda vizuri na atapiga kambi nje ya nchi ambapo atacheza mechi kadhaa za
kirafiki.
Tayari uongozi wa klabu hiyo ulishapewa programu ya
kocha wao, na mwenyekiti wake, Mussa Mapunda alisema watakwenda Malawi na
Zambia ambapo watacheza angalau mechi mbili mbili za kujipima ubavu.
Kocha Mwambusi alisema: “Ligi msimu ujao itakuwa ngumu
na mbele yetu kuna changamoto kubwa, lakini siku zote tunajiandaa kwa mechi
zote 26. Kila mchezo kwetu huwa unakuwa muhimu, kwahiyo tunajiandaa vizuri”.
“Falsafa yetu sio kusajili majina makubwa,
tunawaamini vijana wetu. Timu yangu imebaki vilevile, ingawa nimeongeza
wachezaji wawili watatu”. Aliongeza Mwambusi.
Kocha huyo alisema hatishiki na makocha wa kizungu
kwasababu mbinu za mpira ni zile zile, hivyo anajiandaa vizuri kukabiliana na
changamoto hizo.
Msimu ujao, wachezaji wa Mbeya City wanaweza
kufanya vizuri ukizingatia watakuwa na uzoefu wa msimu mmoja. Kuongezeka kwa
Them Felix `Mnyama` aliyesajiliwa kutoka Kagera Sugar kutaifanya safu ya
ushambuliaji kuwa na nguvu zaidi.
Them atafanya kazi na akina Mwegane Yeya, Paul
Nonga, Deus Kaseke na Peter Mapunda.
0 comments:
Post a Comment