Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Julai 24, 2014, saa 1:33asubuhi
WEKUNDU wa Msimbazi Simba wamedhamiria kurejesha
heshima yao iliyopotea kwa miaka mitatu mfululizo katika michuano ya ligi kuu
soka Tanzania bara.
Simba ambayo imemuongezea mkataba wa mwaka mmoja
kocha wake mkuu, Mcroatia, Zdravko Logarusic ipo katika maandalizi ya msimu
mpya na malengo yao kwasasa ni kuelekea katika mchezo maalumu wa kirafki
utakaopigwa siku ya Agosti 9 mwaka huu dhidi ya Ismailia ya Misri kwenye
tamasha la klabu hiyo la ‘Simba Day’ ndani ya uwanja wa Taifa jijini Dar es
salaam.
Tamasha la ‘Simba Day’ ni maalumu kwa mashabiki,
viongozi na wanachama wa klabu hiyo kukutana kwa lengo la kubadilishana mawazo.
Pia linatumika kama sehemu ya kutambulisha wachezaji wapya waliosajiliwa kwa
ajili ya msimu mpya.
Kiungo wa zamani wa Simba na kocha msaidizi wa
klabu hiyo, Suleiman Abdallah Matola `Veron` amesema kuwa wanaendelea na
mazoezi vizuri ambapo wanafanya maeneo matatu tofauti.
“Tumekuwa tukifanya programu ya maandalizi vizuri.
Tumekuwa tukienda Ufukweni, Gmy na jioni tunafanya mazoezi uwanja wa chuo kikuu
cha Dar es salaam. Kwasasa maandalizi
yanalenga mechi ya Agosti 9 siku ya Simnba Day”. Alisema Matola.
Ismailia watakabiliana na Simba sc siku ya Simba day Agosti 9 mwaka huu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam
Kuhusu wachezaji waliokuja kufanya majaribio
klabuni hapo, Matola alisema wote wamepigwa chini na kocha Loga kutokana na
kuwa na kiwango cha kawaida kulinganisha na mahitaji wake.
“Wachezaji waliokuja kufanya majaribio kutoka nchi
za Rwanda, Afrika kusini na Congo, kiukweli mwalimu hajavutiwa na yeyote kutokana
na uwezo mdogo walioonesha, hivyo ameamua kuelekeza nguvu kwa wachezaji aliopendekeza
wasajiliwe. Tunaamini kufikia wiki ijayo watapatikana,”. Alisema Matola.
“Mwalimu anataka washambuliaji na viungo, lakini
wengine wameshasaini na wengine wanatafutwa”.
“Tumekuwa tukifanya mazoezi na wachezaji wachache,
lakini wiki ijayo tutakuwa tumekamilika zaidi”.
Aidha Matola aliwaomba wanachama wa Simba kuwa na umoja na mshikamo wakati huu ambao timu
yao inajengwa.
Alisema umoja utaifanya klabu itimize malengo yake
msimu ujao na kurejesha heshima iliyopotea kwa muda mrefu.
0 comments:
Post a Comment