Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Julai 16, 2014, saa 1:00 asubuhi
WASHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania wanaocheza
klabu ya TP Mazembe ya Congo, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu
wamewasili asubuhi ya leo tayari kuwavaa Msumbiji (Balck Mambas) jumapili ya
wiki hii ndani ya dimba la Taifa.
Mechi hiyo ni ya kuwania kupangwa hatua ya makundi
kusaka tiketi ya kushiriki fainali za kombe la mataifa ya Afrika, mwakani
nchini Morocco na mshindi wa jumla katika mechi mbili ndiye atafuzu hatua ya
makundi.
Nyota hao wametua nchini kwa ndege
ya Egypt Air wakitokea
Tunisia ambapo timu yao ya TP Mazembe imepiga kambi kwa ajili ya mechi za Ligi
ya Mabingwa Afrika.
Taarifa njema kwa
mashabiki wa soka nchini ni kuwa washambuliaji hao wenye uzoefu na mechi za
kimataifa wamewasili wakiwa fiti kwa kazi.
Samatta aliwakosa
Zimbabwe mjini Harare, lakini safari hii yuko fiti na ameahidi kufanya kazi ya
kulisaidia taifa katika mchezo wa jumapili.
Pia shukurani kwa TP
Mazembe waliowaruhusu wachezaji hawa mapema kujiungga na wenzao, hivyo ni
matarajio ya kuwaona nyota hao wakisaidiana na wenzao kuifunga Msumbiji
nyumbani.
Taifa stars inahitaji
ushindi wa zaidi ya magoli matatu katika uwanja wa nyumbani ili kujiweka
mazingira mazuri ya kusonga mbele kabla ya mchezo wa marudiano utakaopigwa wiki
mbili baadaye mjini Maputo nchini Msumbiji.
Taifa Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imepiga kambi Tukuyu mkoani Mbeya
ikijiandaa kwa mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Mahmoud Ashour kutoka
Misri.
Stars itarejea
jijini Dar es Salaam siku ya Ijumaa (Julai 18 mwaka huu) kwa ajili ya mechi
hiyo wakati Mambas nao wanatarajiwa kutua siku hiyo hiyo. Mechi ya marudiano
itachezwa kati ya Agosti 1 na 3 mwaka huu nchini Msumbiji.
0 comments:
Post a Comment