Kocha wa Yanga sc, Marcio Maximo akimuelekeza jambo Nizar Khalfan
Na Baraka Mbolembole
Imechapishwa Julai, 15, 2014, saa 11:40 jioni
Usajili
wa kiungo wa kushoto, Andre Coutinho katika klabu ya Yanga umepokelewa kwa
mikono miwili. Katika usajili huo kila upande una malengo yake. Mkufunzi mkuu
wa kikosi hicho,Mbrazil, Marcio Maximo ameingia mkataba wa miaka miwili na
mabingwa hao mara 24 wa Tanzania Bara. Mkataba kati ya Maximo na mwajiri wake
upo kwa sisi kuuona. Wakati makocha waliopita katika klabu walitumia fedha na
muda wao mwingi kusaka wachezaji kutoka nchi za Kiafrika, Maximo ambaye amewahi
kufanya kazi Tanzania kwa kipindi cha miaka minne akiwa kocha wa Taifa Stars
ameamua kusajili mbali zaidi.
Yanga
imefanikiwa kumsaini, Mbrazil, Coutinho baada ya Mwalimu huyo kupendekeza
asajile. Huwezi kuona maana yake wakati huu timu ikijiandaa na msimu mpya wa
ligi kuu Bara ambao unataraji kuanza Mwezi, Septemba. Kuwasili kwa Maximo kama
kocha wa Yanga ni wazi kuwa timu hiyo itabadilika kimfumo na kimpira pia.
Marcio ni kocha ambaye mafanikio yake kiufundi ni kuipeleka Tanzania katika
fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani, ni mtu
alijawa na nguvu na mtazamo wa mafanikio. Katika mkutano wake wa kwanza na
vyombo vya habari kama kocha wa Yanga kocha huyo alisema anafuraha kurudi tena
Tanzania kufundisha soka. Wote tumempokea kwa mikono miwili na mashabiki wa
Yanga wanashahuku kubwa ya kuitazama timu yao ikicheza.
Andrey Coutinho (kushoto) akifanya mazoezi
Coutinho ameweza kuwavutia wengi katika
mazoezi ya timu hiyo. Ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kupiga mipira ya
krosi, kona na inawezekana akaibuka mchezaji wa hatari katika mipira ya adhabu
msimu ujao. Maximo anajua anachotakiwa kufanya katika klabu ya Yanga. Coutinho
ameweka wazi kuwa hakuwa mchezaji wa ligi ya ushindani nyumbani kwao Brazil ila
anachukulia kusajiliwa kwake na Yanga kama kitu kikubwa ambacho kitamsaidia
kuendeleza ndoto zake za kuwa mchezaji mahiri wa Brazil. Wabrazil wanacheza
soka popote pale duniani hivyo ujio wa Coutinho una maana kubwa kwa klabu,
zaidi Mwalimu ambaye anafahamu ni mbinu gani atazitumia katika kikosi hicho.
Leo
Yanga wanataraji kumpokea mshambulizi, raia wa Brazil, Geilson
Santos Santana "Jaja". Maximo anataka nini? Timu ambayo itashambulia
kwa uhakika na kufunga mabao kadri itakavyowezekana na jambo hilo huwezi
kulipata kutoka kwa wachezaji ambaom hawatulii klabuni. Usajili wa Wabrazil hao
utamsaidia sana kocha hyu ndani ya uwanja kwa kuwa nina hakika watakuwa
wachezaji ambao watayapokea na kucheza kutokana na maagizo na mafunzo ya
Mwalimu wao. Yanga inatakiwa kupiga hatua na wakati huu uongozi ukipanga
mikakati ya kiuchumi timu itaimarika ndani ya uwanja. Huu ni usajili wa Mwalimu
kitu ambacho mara zote kimekuwa kikipigiwa kelele .
Ukiachana na umakini, kazi aliyochukua
Maximo ni ngumu nafikiri atahitaji busara zaidi za kimpira kama ngazi ya
kumsaidia kutimiza malengo yake katika klabu hiyo. Kitendo cha kuja nchini na
wasaidizi wawili ambao watamsaidia katika kufikisha mawasiliano kwa wachezaji
kinaongeza gharama katika timu ila timu kubwa ni lazima ziwe na wakufunzi wenye
mtazamo na malengo yanayoendana. Salvatory Edward ni mchezaji wa zamani wa timu
hiyo, amekuwa kocha wa timu ya Vijana kwa miaka mitatu naye anaongeza namba
katika benchi la ufundi kitu ambacho kitaongeza urahisi kwa Maximo katika
ufundishaji.
Wengi tunataraji kurudi kwa Maximo
nchini na kuingia mkataba wa miaka miwili kuifunza Yanga kutaisogeza mbele
zaidi timu hiyo katika michuano ya vilabu barani Afrika. Maximo atatukumbusha
kuhusu vipaji vilivyosahulika ambavyo kwa mtazamo mwingine hawakuwa wachezaji
wazuri wa muda wote. Coutinho atatumika kuijenga timu katika ushambuliaji wa
mipira ya krosi hivyo ni lazima timu iwe na mchezaji mfungaji wa uhakika kwa
mipira ya juu. Ujio wa mshambulizi, Jaja unaweza kuifanya Yanga kuwa timu bora
katika ufungaji wa mabao ya vichwa. Yanga ni timu kubwa Tanzania, Afrika
Mashariki na Kati na timu mashuhuri katika michezo ya vilabu Afrika. Asante,
Marcio Maximo kwa usajili wako wa Wabrazil kikosini, Yanga SC, tunawasubiri kwa
hamu katika ligi kuu ya Tanzania Bara. Karibu Countinho, tunamsubiri, Jaja.
0714 08 43 08
Chanzo: shaffihdauda.com
0 comments:
Post a Comment