Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
Imechapishwa Julai 23, 2014, saa 2:12 asubuhi
UONGOZI wa Simba sc chini ya Rais Avens Elieza
Aveva jana umemsainisha mkataba wa mwaka mmoja kocha mkuu wa klabu hiyo,
Mcroatia, Zdravko Logarusic.
Loga alijiunga na Simba desemba mwaka jana kwa
mkataba wa mfupi wa miezi sita baada ya Abdallah Kibadeni kutimuliwa na aliiongoza
Simba mzunguko wa pili wa ligi kuu ambapo alishika nafasi ya nne katika
msimamo.
Kulikuwa na tetesi nyingi kuwa uongozi wa Simba uko
mbioni kuachana na Loga kwasababu ya kutofautiana katika masuala ya wachezaji na
ilielezwa kuwa kocha huyo mwenye msimamo mkali anakataa wachezaji wanaoletwa na
viongozi.
Kabla ya kumsainisha mkataba kocha huyo,
niliandika makala nikieleza namna Simba watakavyofanya makosa kwa kumfukuza
Loga ambaye alianza kuwa na muelekeo mzuri na kikosi chake.
Nilitangaza wazi kutounga mkono hata kidogo
maamuzi ya kumtimua Loga na nikasema nategemea kusikia amepewa mkataba na si
vinginevyo.
Nilifuaatilia kwa kina suala hilo, maamuzi ya uongozi
wa Simba yakaenda sawa na fikira zangu. Ni wazi taarifa za kufukuzwa kwa Loga
zilikuwa na ukweli kiundani, lakini
nadhani busara imetumika kwasababu hakukuwa na sababu ya msingi ya kumuacha.
Loga ni mwalimu mwenye msimamo mkali na anaamini
zaidi katika falsafa yake. Wataalamu wanasema ukiwa kocha lazima uwe na aina fulani
ya falsafa yako na lazima iheshimiwe.
Kocha huyo wa zamani wa Gor Mahia ya Kenya mara
baada ya kuwasili mwaka jana alikuja na mambo mapya kabisa katika klabu ya Simba
na kuwafanya wachezaji waone kama hafai vile.
Ninayoyakumbuka kwa haraka ni pamoja na
kupendekeza kuanzisha utaratibu wa kuwakata mishahara wachezaji watakaoshuka
kiwango na kutocheza kikosi cha kwanza.
Pia aliwataka wachezaji kufika mazoezini nusu saa
kabla ya mechi na wakifika, lazima wawe wanachezea mpira na kupashapasha kabla
ya programu ya mazoezi ya mwalimu kuanza.
Tofauti na miaka ya nyuma, baadhi ya wachezaji
walikuwa wanatumia sehemu ya mazoezi kama sehemu ya kupiga domo wakimsubiri
kocha awasili uwanjani. Wengine waliwahi kuripotiwa kuvuta sigara na bangi kabla ya mazoezi
kuanza.
Hapa ilikuwa baada ya kushinda mechi ya Nani Mtani Jembe desemba mwaka jana ambapo Simba waliitandika Yanga mabao 3-1
Kwa Loga hili lilikuwa ndoto, masharti yake
yalikuwa magumu kwa wachezaji waliozoea maisha mepesi.
Kubwa zaidi ni namna ambavyo hana uvumilivu pale
mchezaji anapovurunda uwanjani. Loga hachelewi kufanya mabadiliko. Aliwahi
kuwatoa wachezaji ndani ya dakika 3. Wachezaji kama Betram Mombeki, Henry
Joseph, Ramadhani Singano, na wengine wengi walishaonja joto la kocha huyu.
Pia ni kocha wa kuthubutu. Kumbuka mechi za mwisho
msimu uliopita alifanya maamuzi ya kumchezesha Henry Joseph nafasi ya beki wa
kulia. Wengi wanamfahamu Joseph kama kiungo, na amecheza nafasi hiyo kwa muda
mrefu, lakini Loga akaja na jipya.
Huku ni kujiamini. Ukiwa mwalimu lazima ufanye
unachofikiria. Wengi walishangaa, lakini ni moyo wa uthubutu wa kocha huyu ndio
ulimfanya afikie maamuzi hayo.
Loga ni mtu mwenye msimamo, anaipenda kazi yake,
anajiamini kwa taalamu yake. Hata mwaka jana zilipozagaa taarifa za yeye
kufukuzwa baada ya msimu kumalizika, yeye alieleza kuwa yupo tayari kwa maamuzi
hayo.
Mara kadhaa baadhi ya wachezaji wa Simba walikuwa
wanalalamika kuwa Loga hafai, ni mkali na anashindwa kuwatetea kwa viongozi
pale mambo yanapokuwa magumu.
Kwa maisha ya watanzania wengi, mtu anayekusimamia
kwa ukaribu na kukupangia masharti, anachukuliwa kama muonevu. Hata wanafunzi
wanachukizwa na mwalimu anayefuatilia sheria. Watasema ni mbaya.
Wachezaji wengi ni wavivu inapofika suala la
mazoezi, wengine hawataki kufuatiliwa. Kumbe mpira hauko hivyo.
Kwa aina ya kocha kama Loga, anawafaa sana
wachezaji wa Kiswahili. Na ndio maana kama uliiangalia Simba ya msimu uliopita,
wachezaji walionekana kabisa kutojituma na kushuka morali.
Niliamini kuwa wengi hawakumtaka Loga na wengi walisingizia
kutolipwa mishahara na posho. Kimsingi, Loga alichukuliwa vibaya na baadhi ya
wachezaji, lakini haifuti ukweli kuwa kocha huyu ni bora kwa aina ya soka la
Tanzania.
Uongozi wa Simba umekuwa sikivu. Umeachana na
mambo yote na kuamua `kufunga ndoa` nyingine ya mwaka mmoja na Loga.
Sasa ni wakati wa Loga kuyaendeleza mazuri
aliyoanza nayo. Suala la nidhamu kwa wachezaji, lazima liendelee kukaziwa.
Cha msingi, uongozi wa Simba umsajilie timu bora ili
msalaba wote aubebe yeye. Baada ya kusaini jana, alieleza kufurahishwa na suala
hilo na akaahidi ubingwa.
Naye makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange `Kaburu`alisema
kuwa wamemtwisha msalaba wote Loga na ahakikishe klabu hiyo inabeba kombe la
ligi kuu msimu ujao.
Kwa kumpa mkataba Loga kutamfanya atulize kichwa kutekeleza
majukumu yake na bila shaka akipata wachezaji anaowataka, atafanya vizuri.
Kocha huyo amekuwa akisema kila siku kuwa
anahitaji wachezaji wenye uzoefu kwasababu kikosi chake kina wachezaji wengi
vijana. Maana yake anataka watu wa kumfanyia kazi na sio kujengwa kila siku.
Mawazo ya Mcroatia huyu ni mazuri, lazima kikosi
cha ushindi kiwe na aina yote ya wachezaji (wenye uzoefu na vijana). Huu ni
wakati wa kumtafutia wachezaji anaowahitaji.
Bahati nzuri, TFF imeongeza muda wa usajili, hivyo
ni nafasi ya kumsikiliza Loga ili wapatikane watu anaowataka.
Nawapongeza Simba kwa kumuamini Loga, kocha ambaye
msimamo wake naukubali hasa kwa suala la nidhamu ya mchezo wa wachezaji.
0 comments:
Post a Comment