Mbwana Samatta (kushoto) na Mrisho Ngassa (kulia) wataanza pamoja
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Julai 20, 2014, saa 7:00 mchana
TAIFA STARS chini ya kocha Mholanzi, Mart Nooij
inaingia uwanjani jioni ya leo kuvaana na Msumbaji (Black Mambas) katika mchezo
wa kuwania kupangwa hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali za
mataifa ya Afrika, AFCON, mwakani nchini Morocco.
Stars yenye bunduki zake zote itakabiliana na
Mambas wenye historia ya kuiharibia katika michezo muhimu kwani waliwahi kufungwa
bao 1-0 uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam mwaka 2007 kuwania kucheza fainali
za AFCON , mwaka 2008 nchini Ghana.
Pia mwaka 2012, Msumbiji waliitoa Stars chini ya
Kim Poulsen kwa mikwaju ya penati kuwania kucheza AFCON mwaka 2013 nchini
Afrika kusini..
Kuelekea katika mchezo huo, kocha mkuu Mart Nooij
alisema maandalizi yamekamilika na wanasubiri muda ufike ili wakaoneshe
walichojiandaa katika kambi ya Botswana na mjini Tukuyu mkoani Mbeya.
Wachezaji wote wamesema wapo tayari kwa mechi ya
jioni ya leo ambapo Mbwana Samatta alisema yuko fiti kwa asilimia 100 na
ataisaidia Stars kuibuka na ushindi.
Naye Thomas Emmanuel Ulimwengu alisema mechi
itakuwa ngumu, lakini wapo katika morali ya kufanya kazi kwa umoja zaidi
uwanjani, huku akiwaomba watanzania kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yao.
Beki Shomary Kapombe yeye alisema kambi ya Tukuyu
imekuwa na matunda kwasababu wachezaji
wote wapo katika morali ya kutafuta ushindi. Hata hivyo aliwaomba mashabiki
kufika kwa wingi kuwaongezea hamasa ya ushindi.
Kocha Mart Nooij anahitaji ushindi si chini ya
mabao 3-0 ili kujiweka mazingira mazuri ya kusonga mbele katika mchezo wa
marudiano wiki mbili zajazo mjini Maputo nchini Msumbiji.
Katika mchezo wa leo, Nooij amewaanzisha
washambuliaji wanne, Mbwana Ally Samatta, Thomas Emmanuel Ulimwengu, John
Raphael Bocco `Adebayor` na Mrisho
Khalfani Ngassa `Anko`.
Mlinda mlango ataendelea kuwa Deogratius Munish
`Dida`, huku mbavu ya kulia ikikamatwa na Shomary Kapombe.
Upande wa kushoto atasimama Oscar Samwel Joshua,
wakati vitasa vya kati ni Kevin Yondan na nahodha Nadir Haroub ` Cannavaro”.
Safu ya kiungo atasimama Erasto Edward Nyoni na Mwinyi
Kazimoto Mwitula.
Nyoni amechukua nafasi ya kiungo majeruhi, Frank
Domayo `Chumvi`. Kikosi cha Nooij hakijawa na mabadiliko ukilinganisha na kile
kilichoifunga Zimbabwe bao 1-0 ndani ya dimba la Taifa.
Thomas Ulimwengu (kushoto) anawaonesha kazi Mambas jioni ya leo
Katika mchezo wa leo, kocha wa Stars anatarajia
kucheza mpira kwa mfumo wa kulinda lango, kumiliki mpira na kushambulia kwa
kasi.
Ni muhimu kuwazuia Msumbiji kupata bao lolote la
ugenini, hivyo mabeki wanatakiwa kukaba nafasi na kuwafanya Msumbiji wasicheze
mpira wanaotaka.
Mabeki wana kazi ya kuwafanya washambuliaji wa Msumbiji
washindwe kutekeleza mipango yao. Stars inahitaji kumiliki mpira kwa muda mrefu
na kutengeneza mashambulizi.
Kazimoto ana kazi ya kuwachezesha washambuliaji wa
Stars. Mashambulizi ya kasi na makini yataifanya Stars ipate matokeo jioni ya
leo.
Nao mashabiki wana wajibu wa kuishangilia timu kwa
muda wote ili vijana wawe katika hamasa kubwa.
Kila la kheri Taifa stars kuelekea mchezo muhimu
jioni ya leo.
0 comments:
Post a Comment