Kocha mkuu wa Simba sc, Mcroatia, Zdravko Logarusic (wa kwanza kushoto)
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
Imechapishwa Julai 22, 2014, saa 2:43 asubuhi
HAKUNA uchawi
katika soka!. Kabumbu ni mipango na kupita njia sahihi ili kufikia kiwango
cha juu.
Tanzania ni miongoni mwa nchi `tia maji tia maji`
kwenye mipango ya soka. Viongozi na mashabiki wanataka kupita njia ya mkato
`short cut` ili kupata mafanikio.
Moja ya kosa kubwa wafanyalo watu wengi ni
kulifananisha soka letu na mataifa yaliyoendelea (barani Ulaya na Amerika).
Utasikia mbona hata Chelsea, Man United, Barcelona wanafukuza makocha?,
wanaacha wachezaji?.
Kumbe klabu hizi zina mipango na zimekamatwa na
wafanyabiashara ambao wamewekeza pesa zao. Hakuna mfanya biashara atayevulimilia
hasara. Mtu anainunua klabu kwa mabilioni ya fedha, mfano Roman Abramovich wa
Chelsea. Hawezi kuona kocha anavurunda na kumuacha, lazima achukue hatua
kwasababu anataka faida.
Loga akiwa kazini (wa kwanza kulia)
Pia klabu za Ulaya, mara nyingi kazi ya kocha ni
kutengeneza timu kiuchezaji, (ufundi na mbinu za mpira). kwa asilimia kubwa, wachezaji wanaowakuta
wanakuwa tayari wameandaliwa vizuri au ananunua wachezaji waliopikwa tayari. Kwa
maana ya kwamba, wana misingi ya mpira,
kazi yake inabaki kuunganisha timu kwa kutumia wachezaji walio tayari kufanya
kazi.
Kama kazi yako ni kuufundisha mpira na kuunganisha
wachezaji katika falsafa yako, yaani wachezaji wote ni wazuri, inashindikanaje
kufukuzwa unaposhindwa kuwapa mbinu sahihi za mpira?. Ndio maana makocha wengi
Ulaya wanawajibishwa kwa kushindwa kuipa mbinu za uhakika timu yake.
Leo hii huwezi kufananisha klabu za Tanzania (Simba,
Yanga) na klabu za Ulaya. Simba na Yanga ni klabu
kongwe na kimsingi zinapendezesha soka la Tanzania. Hizi ni klabu za wanachama,
kwa msingi huo, wanachama wana nguvu kubwa na wanaweza kuleta athari hata kwa
benchi la ufundi.
Unajua siku zote, watu wanaochaguliwa kwa
kunyoshewa vidole na wananchi au wanachama, kwa asilimia kubwa wanawajibika kwa
watu hao. Leo hii Mbunge hawezi kuwadharau wananchi wa jimboni kwake kwasababu
anajua kuna uchaguzi unakuja.
Leo hii kiongozi wa klabu ya Simba au Yanga
anachaguliwa kwa kupigiwa kura na wanachama. Halafu ana malengo ya kugombea
tena baada ya muda wake kumalizika, anashindwaje kukubaliana na matakwa ya wanachama
hata kama si ya kimpira?
Mara nyingi utawasikia mashabiki na wanachama wa
klabu hizi wakitoka povu kwa kuwakandia makocha na wachezaji, mara fulani hafai,
kocha fulani fukuza, mchezaji fulani ameshuka kiwango, au kwanini kocha
hampangi fulani.
Kitaalamu, kocha ndiye mwamuzi wa mwisho kuamua
mchezaji gani anapangwa na nani hapangwi. Yeye anachagua kikosi. Hata katika
usajili, yeye ndiye mwenye mamlaka ya kuagiza nani asajiliwe na nani aachwe na
si viongozi.
Leo hii Jose Mourinho, Aserne Wenger, Brendan
Rodgers akiamua kumnunua mchezaji, anapeleka pendekezo lake kwa viongozi,
wanaangalia kapuni kama kuna kitita, kama mzigo upo wanaingia sokoni. Kama
watashindwa bei, watamwambia kocha hatutamnunua
Kama tunapenda kujifananisha na ulaya, basi hata
hili tujaribu basi kujifananisha. Kwanini watu wanaoitwa `Friends of Simba`
(F.O.S) wamsajilie mwalimu timu au kwanini Yusuf Manji na wenzake wamsajilie
kocha wachezaji? Huu ni uzamani kabisa.
Lazima kila mtu afanye majukumu yake. Inafika
wakati, hakuna njia ya mkato zaidi ya kuzibadili Simba na Yanga kuwa katika mfumo
wa kampuni na si klabu ya wanachama.
Yanga wamemleta nchini Marcio Maximo. Kocha huyu
alikuwa anaifundisha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa stars kuanzia mwaka 2006
mpaka 2010. Kwa wenye kumbukumbu nzuri, Mbrazil huyu ana msimamo mkali hasa
linapofika suala la nidhamu kwa wachezaji.
Maximo yupo na Wabrazil wenzake watatu kwa maana
ya msaidizi wake Leonado Neiva, na wachezaji wawili raia wa Brazil, Geilson
Santos Santana na Andrey Coutinho ambao wote walisaini mkataba wa miaka miwili.
Katibu mkuu wa Yanga, Beno Njovu anasema wachezaji
wote ni mapendekezo ya kocha Maximo na wao wanajitahidi kutekeleza. Kama ni
kweli, basi ni jambo zuri katika utendaji wa kazi, hasa muda huu ambao soka
linakwenda kisasa zaidi.
Maximo anaonekana kuaminiwa na kuheshimiwa sana na
viongozi wa Yanga na mashabiki. Hii inatokana na historia yake. Lakini haiondoi
ukweli kuwa kocha huyu anahitaji kupewa muda ili kufikia malengo.
Yanga inahitaji kutengeneza mfumo wa soka la
vijana ili kuwa na muendekelezo wa timu. Ili hili linafanikiwe, wanatakiwa
kuwaamini walimu wao wa Kibrazil na kuwapa majukumu yote. Lakini uvumilivu
uwepo kwasababu soka halina njia ya mkato.
Kwa upande wa Simba, mengi yanazungumza. Wanaye
kocha Mcroatia, Zdrvako Logarusic. Jamaa huyu ni mtu mwenye msimamo mkali,
hakika Loga hana mchezo kwa wachezaji.
Hawezi kumvumilia mchezaji anapofanya vibaya. Ni
kocha sahihi kwa aina ya wachezaji wa Kitanzani. Wanandinga wengi nchini si
waumini wa nidhamu ya mpira, hivyo aina ya makocha kama Loga ni muhimu. Lakini
kuna mambo tofauti yanazungumzwa.
Viongozi wa Simba wanasema wapo katika mazungumzo
na Loga ili wampe mkataba mwingine wa miaka miwili baada ya ule wa awali wa
miezi sita kumalizika mwishoni mwa msimu uliopita.
Suala la Loga kupewa mkataba lilianza wakati wa
uongozi wa Ismail Aden Rage, walisema kila kitu kimekwenda sawa na atakaporudi kutoka
mapumzikoni itakuwa ni kumwaga wino tu.
Hata Rais Evans Aveva alipoingia madarakani,
alisema uongozi wake hautamfukuza Loga, lakini siku za karibuni kumekuwepo na taarifa
za chini kwa chini kuwa uongozi wa Simba unataka kuachana na Loga na upo katika
mazungumzo na kocha wa Gor Mahia ya Kenya, Bobby Williamson.
Viongozi wao wanadai wapo katika mazungumzo ya
kumuongezea mkataba, lakini taarifa kutoka vyanzo makini zinadai Loga anaweza
kufungashia virago.
Sababu kubwa inayoelezwa ni kwamba Loga anakataa
wachezaji wanaoletwa na viongozi kwa ajili ya kusajiliwa. Sasa wanaona
anawasumbua tu, bora wakatafuta kocha mwingine.
Kundi la `Friends of Simba` (F.O.S) kwa muda mrefu
limekuwa likishutumiwa kuwa na tabia ya kuwasajiliwa makocha wachezaji, na
wanafika mbali mpaka kuwapangia timu ya kucheza.
Kocha wa zamani wa Simba, Mserbia, Milovan
Circovic aliwahi kulalamika kuwa viongozi walikuwa wanampangia timu. Hata
usajili, viongozi walifanya wao.
Hili ni tatizo na kirusi kikali cha soka la Simba.
Kama watu hawa wataendekeza tabia hii katika uongozi wa Aveva, basi watashindwa
vibaya mno kufikia malengo yao.
Loga ndiye mwenye uamuzi wa mwisho, mchezaji gani
asajiliwe na nani aachwe. Viongozi mnamleteaje wachezaji? Kwani hakupendekeza?
Kama kweli aliwapa ripoti na mapendekezo ya
wachezaji anaowataka, inakuwaje akatae kuwachukua watu aliowapendekeza? Hapa kama
kuna kamchezo fulani.
Nadhani kuna watu wanaendelea na utaratibu wa
kujisajilia tu. Kocha kumkataa mchezaji
sio tatizo. Labda kuna mengine nyuma ya pazia. Mwisho wa siku yeye atalaumiwa
kwa timu kufanya vibaya, ndio maana anakuwa makini kuwaangalia wachezaji.
Kama Simba itamfukuza Loga, athari ya kufukuza
makocha itaendelea kuwatafuna kwa msimu mwingine. Kumbuka ndani ya miaka mitatu
au minne, tayari makocha wanne wameshatimuliwa.
Kuanzaia kwa Cirvociv, ndani ya muda mfupi akaja
Patric Liewig kutoka Ufaransa,alikaa nusu msimu na kufukuzwa. Baadaye akackuliwa
Abdallah Kibadeni , naye akaiongoza timu nusu msimu uliopita na kufukuzwa na sasa
Loga.
Kama Loga anafukuzwa, manake ameiongoza timu kwa
nusu msimu. Manake atakamilisha idadi ya makocha watatu (Liewig, Kibadeni,
Loga) kuiongoza Simba kwa nusu msimu ndani ya muda mfupi.
Unadhani kwa staili hii Simba itakwenda mbele? Hata
aje Mourinho, Van Gaal, Guardiola, hakuna mafanikio kama tabia hii itaendelea.
Simba inahitaji kukaa na makocha kwa muda mrefu ili kujijenga upya.
Maamuzi pekee nitakayoyaunga mkono ni kusikia Loga
amesaini mkataba na sio tumeshindwa kufikia makubaliano.
Kama viongozi watakuja na kauli hiyo, binafsi
sitaamini kwasababu taarifa zilishavuja kuwa Loga hatakiwi kwasababu anakataa
wachezaji wanaoletwa na viongozi.
Kila la Kheri Simba kuelekea michuano ya ligi kuu
soka Tanzania bara.
0 comments:
Post a Comment