Mbwana Ally Samatta (kushoto) ni miongoni mwa silaha za Taifa Stars nchini Msumbiji
Imechapishwa Julai 31, 2014, saa 3:00 asubuhi
TAIFA Stars imeondoka jana kwa ndege ya Air
Tanzania kuelekea Afrika kusini ambapo itaweka kambi ya siku mbili kabla ya
kutua Mjini Maputo kwa ajili ya mechi ya marudiano dhidi ya wenyeji Msumbiji ,kuwania
kupangwa hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali za mataifa ya
Afrika mwakani nchini Morocco.
Ikiwa nchini Afrika kusini, Stars itajikamilisha
kwa wanandinga wake wawili wanaocheza soka la kulipwa katika klabu ya TP
Mazembe, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu kujiunga na wachezaji
wenzao.
Mwinyi Kazimoto anayecheza soka la kulipwa nchini
Qatar yeye alishajiunga na timu tangu ikiwa Dar es salaam.
Mechi hiyo itachezwa Agosti 3 mwaka huu uwanja wa
Taifa wa Zimpeto uliopo nje kidogo ya mji mkuu wa Maputo na Stars inahitaji
ushindi au sare ya kuanzia mabao 3-3 ili kusonga mbele.
Taifa stars ililazimishwa sare ya mabao 2-2 na
Msumbiji julai 20 mwaka huu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Baada ya mechi hiyo, kikosi kiliweka kambi mjini
Tukuyu kwa malengo ya kufanya marekebisho ya makosa yaliyojitokeza.
Bila shaka baada ya sare ya Dar es salaam, benchi
la ufundi limefanya uchambuzi wa makosa yaliyojitokeza na kutafuta mbinu mpya
za kuwatoa Msumbiji.
Naye Thomas Ulimwengu (mwenye mpira kushoto) anatarajia kuisadia Taifa Stars
Stars ikiwa Dar es salaam ilikuwa na mpango wa
kushinda na kujilinda ili isifungwe, lakini ikaambulia sare na sasa mpango
umebadilika.
Inakwenda Msumbiji kutafuta ushindi tu, kwa maana
hiyo lazima kocha mkuu Mholanzi Mart Nooij kwa kusaidiana na Salum Mayanga wameshatafuta
mbinu mpya za kuwatoa Msumbiji.
Taifa stars inahitaji ushindi Msumbiji, lakini
inashindaje? hilo ni juu ya benchi la ufundi.
Kocha hatakiwa kulaumiwa kwa matokeo yoyote, kwasababu kuna wakati fulani makocha wanawapa
mbinu wachezaji, lakini wachezaji hao hao wanashindwa kuelewa na kuzitumia,
hivyo lengo mama halipatikani.
Mechi ngumu ya Msumbiji inatakiwa kila upande
ufanye kazi yake vizuri. Kama kila upande unatekeleza majukumu yake kwa
asilimia 100, basi ushindi utapatikana.
Ili kufikia kilele cha mafanikio, kila mdau
anatakiwa kuchangia kwa asilimia 100. Kwa mfano tujifunze kwa Ujerumani ambao
wamefikia mafanikio ya kutwaa ubingwa wa kombe la dunia.
Wengi wanadhani Ujerumani wamefikia mafanikio yale
kwasababu ya umahiri wa wachezaji kama Toni Kroos, Thomas Muller, Phillip Lahm
na wengineo pamoja na benchi zima la ufundi linaloongozwa na kamanda mkuu
Joachim Low.
Eneo la Bahia ambapo Ujerumani waliweka kambi
Kumbe mambo ni tofauti. Ujerumani walipoona
mashindano yanakwenda kufanyika Brazil, waliamua kutuma mtaalamu wa mazingira
aliyeenda kuisoma Brazil na Amerika kusini kwa ujumla. Walihitaji kujua hali ya
hewa ikoje na ni eneo gani litakuwa zuri kwa timu kukaa ili kurahisisha safari
za kwenda viwanja mbalimbali watakavyocheza.
Mtaalamu aligundua kuwa eneo la Bahia ni zuri
sana, lina hali ya hewa nzuri, na ni rahisi kwa usafiri wa ndege ili kufika
viwanja mbalimbali.
Baada ya mtaalumu yule kurudisha ripoti, chama cha
soka nchini Ujerumani DFB kwa kushikiriana na wadhamini, wakaenda kujenga kambi
yao maeneo ya Baia ambapo waliweka vifaa vyote vya mazoezi na uwanja.
Kocha Joachim Low na Meneja mkuu wa timu ya
Ujerumani, Oliver Bierhoff walifurahia kambi ya Bahia na kuweza kutimiza
majukumu yao vizuri, hivyo kujenga morali kubwa kwa wachezaji wao.
Baada ya uwekezaji mkubwa kiasi kile, kwa kila
mdau kutimiza majukumu yake, Ujerumani ikafikia kilele cha mafanikio.
Hata sisi Tanzania tunaweza kujifunza. Sio kulaumu
makocha tu pale timu inapofanya vibaya. Lazima tujiulize, kila mdau anayehusika
anatimiza majukumu yake kwa asilimia 100?
Je, TFF wanaandaa mazingira ya timu kufanya
vizuri. Wanawajibika kwa asilimia mia moja? Kama hapana, basi nao wanatakiwa
kubeba mzigo wa lawama.
Pia lazima tujiulize, wadhamini wanatoa pesa kwa
wakati ili kurahisisha mazingira ya timu kufanya vizuri? Posho ya wachezaji
inatoka kwa wakati? kambi inawekwa kwa wakati? Kama jibu ni hapana, basi nao
wadhamini wanatakiwa kulaumiwa kwa matokeo mabaya ya timu.
Hatusemi wadhamini hawatimizi wajibu wao kwa
wakati na kwa asilimia 100, lakini ni angalizo tu kuwa tujifunze kwa wenzetu
ili kufikia malengo yetu.
Kuwalaumu wachezaji na makocha haitasiaidia,
lazima tuhakikishe kila mdau anayehusika anatimiza majukumu yake.
Taifa stars kama itacheza kwa uangalifu na kufuta
makosa yalitokea mechi ya kwanza, inaweza kupata matokeo mbele ya ‘Black Mambas’.
Kila la kheri Taifa Stars. Mungu ibariki Tanzania,
Mungu ibariki Taifa Stars.
Chanzo: shaffihdauda.com
0 comments:
Post a Comment