Kwani hawa walienda kwa mbeleko Simba sc au ni uwezo tu?
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
Imechapishwa Julai 23, 2014, saa 14:10 asubuhi
KANUNI ya kuwa mchezaji bora wa mpira wa miguu ni
ndogo tu. Fanya mazoezi na zingatia nidhamu ya mchezo wenyewe. Ukifanya vitu
hivyo, utaweza kufikia malengo yako.
Mpira una misingi yake, kuna sheria, kanuni na
namna ya kuucheza. Ukifundishwa na makocha waliosomea, unaweza kuucheza.
Lakini mpira ni kipaji, sio kila mtu anaweza kuwa
mchezaji mpira. Ndio maana unaona kuna watu wanapenda wawe wachezaji, lakini imeshindikana
kwasababu hawana vipaji vya soka.
Sio kila mtu acheze mpira. Yapo mambo mengi sana
ya kufanya kwa kuzingatia kipaji alichonacho. Lakini kuna watu wanataka wacheze
mpira wakati hawawezi kuucheza.
Mpira wa miguu ni mchezo wa hadharani, huwa hauna
kificho. Mtu anayejua utamuona hadharani. Mpira hauhitaji mtu akubebe mgongoni
ili upate nafasi ya kucheza. Mpira ni kuonesha uwezo na utapata nafasi
kirahisi.
Kumekuwepo na wimbi kubwa la vijana wanaotaka
kucheza mpira katika klabu za ligi kuu na ligi daraja la kwanza. Mara nyingi
wanawafuata watu wenye ushawishi mkubwa ili wawatafutie nafasi katika timu
hizi.
Yaani mtu anamfuata mtu anayefahamika, kwa mfano
kocha wa zamani, mwandishi wa habari, kiongozi mkubwa wa soka au tofauti na
soka akimuomba amfanyie mpango wa kutafuta timu kwa kutumia jina na ushawishi
wake.
Vijana wa Coastal Union walitwaa ubingwa wa kombe la Uhai
Tatizo la Wabongo tumejengwa katika misingi ya
kubebana bila hata kuwa na uwezo. Ukienda sehemu nyingi za kazi, utamkuta mtu
anafanya kazi na hana ueledi kabisa. Ukifuatilia, unagundua aliletwa na mtu fulani
au ni mtoto wa mtu fulani. `Tunafeli` vitu vingi sababu ya tabia hii.
Katika mchezo wa soka, kubebana ni kufanya dhambi
kubwa. Huwezi kumleta kijana `galasa` kwasababu tu una uhusiano naye. Najua
haya yanafanyika sana na watu wanawatafuta ndugu zao.
Siku za karibuni, Ruvu Shooting na JKT Ruvu
zilifanya majaribio ya kutafuta wachezaji vijana watakaounda timu zao za umri
chini ya miaka 20. Vijana wengi walijitokeza kutoka maeneo mbalimbali ya nchi
hii.
Mfano JKT Ruvu walisema zaidi ya vijana 600
walijitokeza katika majaribio hayo chini ya kocha mkuu, Fred Felix Minziro
Cataraiya Majeshi baba Isya. Kwa idadi kubwa kiasi hiki, unagundua kuna vijana
wengi wanaotaka kucheza soka.
Lakini wakati zoezi hili linaendelea, nilipokea
ujumbe na kupigiwa simu na vijana wanaonifahamu wakilalamika kuwa kuna undugu,
upendeleo na watu wameletwa na viongozi wa klabu.
Moja ya hekaheka za michuano ya Uhai
Kimsingi ukiwasikiliza vijana hawa, unagundua kama
kuna `ladha` ya ukweli hivi kwa kuzingatia utamaduni wa Kibongo wa kupeana
mbeleko.
Najua wapo viongozi ambao wanajali sana maslahi
binafsi. Wanawachukua watoto wa marafiki zao, ndugu zao na kuwasajili katika
timu. Wanaacha wachezaji wazuri, eti kisa tu hawana undugu nao.
Kwa aina hii ya viongozi, soka la Tanzania litazidi
kudidimia. Lazima wabadilike na kuja na mtazamo wa kisasa.
Vijana wasajiliwe kwa uwezo wao. Kama mtu anajua
mpira achukuliwe, kama hajui aachwe. Kwasababu tumekuwa na vijana wengi
wasiojua mpira kwenye timu zetu na wanaojua wanahangaika mitaani.
Halafu kwa vijana, ushauri wangu ni kwamba, soka
ni mchezo wa hadharani, unaweza kuchukuliwa hata kama huna ndugu wa kukubeba.
Kila mtu anataka mchezaji mzuri. Kama kweli una
kipaji kikubwa cha soka, lazima utachukuliwa tu.
Sema changamoto inayoonekana ni njia ya kupata
nafasi. Yaani unaendaje Simba, Yanga, Azam kufanya majaribio? Hapo ndipo kuna
tatizo.
Lakini njia rahisi ni kulazimisha. Wewe nenda
mazoezini, waeleze nia yako. Wakikataa, endelea kupasha pasha hapo hapo,
ukibahatika kupata nafasi, ndio muda wa kuwapoteza.
Mimi naamini unaweza kutoka bila kubebwa kama
kweli una vitu adimu. Watu wanahitaji sana watu wenye vipaji vikubwa, ukipata
nafasi onesha kama unajua.
Tatizo la vijana wengi ni kwamba wameshaharibiwa
na mfumo wa mbeleko. Basi muda wote wanatafuta watu wa kuwaunganisha kihuni-huni
tu. Lakini jambo la msingi ni kujijenga katika mazoezi ili ubaki kufuta nafasi
ya kuonesha kipaji chako.
Yaani mtafute mtu akuunganishe na viongozi wa timu
ili ukajaribiwe. Hapa lengo liwe ni kukupatia mawasiliano tu, ukienda huko na
kuchemsha ujue huna uwezo mkubwa.
Usirudi tena kupiga simu, `aaah kaka ongea na kocha wa Simnba kaka kwasababu unamfahamu’.
Huu ni mfumo wa kivivu. Kama hujachaguliwa, ni
changamoto kwako. Lazima ujiulize, labda nimekosea wapi, halafu ujipange upya.
Vijana jipangeni na jifunzeni mpira, nafasi zipo
hata bila kubebwa. Kipaji chako kitakutangaza tu.
Wangapi walitokea kusikojulikana, lakini kwasababu
walionesha vitu adimu, wakachuliwa na kuwa wachezaji wakubwa.
Viongozi na ninyi badilikeni, haka ‘katabia ka
kubebana’ kwa mbeleko ni sumu ya soka la Tanzania.
0 comments:
Post a Comment