Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
Imechapishwa Julai 16, 2014, saa 3:13 asubuhi
KOCHA wa Simba sc, Mcroatia, Dravko Logarusic ameanza kazi kukinoa kikosi chake kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara katika uwanja wa Chuo kikuu cha Dar es salaam (UDSM).
Loga ameamua kuanza kambi mapema kwa lengo la
kurejesha heshima ya Simba iliyopotoea kwa miaka mitatu mfululizo.
Katika mazoezi hayo, wachezaji wa zamani ambao
hawapo katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kinachojiandaa na mechi ya Julai
20 dhidi ya Msumbiji wanahudhuria pamoja na wachezaji wapya.
Mshambiliaji wa zamani wa Supersport United ya
Afrika kusini, Dani van Wyk amekuwa akihudhuria mazoezi hayo kama sehemu ya
kujaribiwa na Loga kabla ya kufanya maamuzi ya kumsaininisha mkataba.
Mchezaji huyo amekuwa akijitahidi kuonesha uwezo
wake, lakini Loga anasema anahitaji muda kumtazama kabla ya kufikia
makubaliano.
Mlinda mlango bora wa ligi kuu soka Tanzania bara
msimu uliopita, Hussein Sharrif `Iker Casillas` amesharipoti kuanza mazoezi na
Simba baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili akitokea Kagera Sugar.
Wachezaji wengine wapya walioanza mazoezi ni
pamoja na Michael Mgimwa kutoka Thailand, Mohammed Hussein maarufu kama
Tshabalala kutoka kwa `wanankulukumbi`, Kagera Sugar.
Wakati Simba wakiendelea na mazoezi hayo, nao
watani wao wa jadi, Yanga sc wanaendelea kunoa makali katika uwanja wa shule ya
sekondari Loyola chini ya kocha mkuu, Mbrazil Marcio Maximo akisaidiwa na
Leonardo Neiva.
Katika harakati zake za kufanya vizuri msimu ujao,
Yanga imewanasa nyota wawili kutoka Brazil, kiungo mshambuliaji, Andrey
Coutinho aliyewasili siku moja baada ya Maximo kutua nchini kutokea nchini
Brazi.
Mshambuliaji mwingine kutoka Brazil, Geilson
Santos Santana `Jaja` aliwasili jana akitokea mjini Sao Paul nchini Brazil tayari
kwa kuanza kazi Dar Young Africans.
Jaja alikuwa anacheza timu ya Itabaina FC ya
nchini Brazil na ujio wake unafikisha idadi ya Wabrazil wanne katika kikosi cha
Yanga , (makocha wawili na wachezaji wawili).
Asubuhi ya leo, Jaja anatarajia kuonekana kwenye
mazoezi ya Yanga katika shule ya sekondari Loyola.
Usajili wa Yanga umevuta hisia za mashabiki wengi
na kupandwa na `midadi` ya kukiona kikosi hicho msimu ujao wa ligi kuu
unaotarajia kuanza kushika kasi septemba 20 mwaka huu.
Yanga ya Maximo inatarajiwa kubadilika kimfumo na
nidhamu ya wachezaji kwa ujumla. Maximo ni kocha mwenye msimamo mkali, anapenda
nidhamu ya wachezaji uwanjani na nje ya uwanja. Hapendi kuingiliwa katika
maamuzi yake.
Hii ilionekana alipokuwa na timu ya Taifa ya
Tanzania kuanzia mwaka 2006 mpaka 2010. Mara nyingi Maximo aliweka wazi kuwa
kama mchezaji hana nidhamu, hawezi kucheza katika kikosi chake. Kwa muda mrefu
walitofautiana na aliyekuwa kipa namba moja wa Tanzania, `Tanzania One`, Juma
Kaseja kwa madai ya utovu wa nidhamu.
Hata wakati Mrisho Ngassa anaitwa kwa mara ya
kwanza katika kikosi cha Taifa stars na Maximo, kocha huyo alionesha msimamo
wake licha ya watu wengi kushinikiza winga huyo ajumuishwe kikosini.
Maximo aliweka wazi kuwa anahitaji kumuona Ngassa
kwenye mechi zaidi ya moja ili ajiridhishe. Mashabiki walipiga kelele kwasababu
Ngassa alikuwa kwenye kiwango cha juu, lakini alimuita mpaka alipojiridhisha.
Haruna Moshi `Boban`, Athuman Idd `Chuji` waliwahi
kukumbana na joto la jiwe kutoka kwa Maximo kutokana na utovu wa nidhamu.
Ipo mifano mingi ya kutolea kuhusu Maximo, lengo likiwa
ni kuonesha jinsi anavyoamini katika nidhamu ya wachezaji.
Huyu ni kocha anayeiamini falsafa yake. Wachezaji
wa Yanga watalazimika kuwa wapole kwa Mbrazil huyu. Longo longo za utovu wa
nidhamu si rahisi kusikika kwa Maximo.
Wakati Maximo akisifika kwa kuzingatia nidhani,
kwa mwenzake Logarusic wa Simba hali ni kali zaidi.
Loga ni moto wa kuotea mbali. Tangu ajiunge na
Simba mzunguko wa pili wa msimu uliopita akirithi mikoba ya Abdallah Kibadeni,
Mcroatia huyo aliwawashia indiketa nyekundu wale wote waliopuuza maelekezo
yake.
Loga haoni shida kumchomoa mchezaji uwanjani ndani
ya dakika tatu. Huwa hana subira pale mchezaji anapovurunda. Betram Mwombeki,
Henry Joseph Shindika, na wengineo wanalijua vizuri hilo.
Loga alifika mbali zaidi kwa kuweka masharti
magumu kwa wachezaji akiwemo kukatwa mishahara na posho wanaposhuka viwango,
kufika mazoezini nusu saa kabla ya muda wa mazoezi na mchezaji akifika
uwanjani, lazima uwe unachezea mpira kuweka mwili sawa na si kukaa na kupiga
domo tu.
Wachezaji waliona Loga hafai na mara kadhaa
waliibua maneno ya chinichini wakisema kocha huyo ni mkali mno.
Hata hivyo, uongozi wa Simba uliwapuuza na
kumuonezea mkataba wa miaka miwili zaidi. Loga ni muumini wa nidhamu kwa kiasi
kikubwa na ana msimamo mkali.
Marcio Maximo na Dravko Logarusic wanafanana kwa
kuzingatia nidhamu na kusimamia misimamo yao. Ni makocha wanaopenda kutekeleza
falsafa zao bila kuingiliwa.
Kwa aina hii ya makocha, Simba na Yanga zinaweza
kufanana kwa nidhamu, lakini viwango vya uchezaji vinaweza kuwa tofauti
kutokana na aina ya wachezaji walionao.
Simba ya Loga, Yanga ya Maximo, kuna kitu kipya
kitaonekana kuanzia septemba 20, mwaka huu. Acha tusubiri kuona mbwembwe za
watani wa jadi.
0 comments:
Post a Comment