Imechapishwa Julai 18, 2014, saa 3:57 asubuhi
VICENTE del Bosque amevunja ukimya kuhusu hatima
yake kwa kuweka wazi kuwa bado ana nia ya kuendelea kuwa kocha wa timu ya Taifa
ya Hispania mpaka fainali za mataifa ya Ulaya mwaka 2016.
Hispania iliboronga na kushindwa kutetea ubingwa
wa dunia waliotwaa mwaka 2010 nchini Afrika kusini ambapo katika fainali za
mwaka huu nchini Brazil walitolewa hatua ya makundi wakifungwa mabao 5-1 na Uholanzi
na 2-0 dhidi ya Chile.
Licha ya timu yake kufanya vibaya mwezi uliopita,
Del Bosque amesisitiza kuwa hana nia ya kujiuzulu na anafurahi kuendelea
kuisaidia Hispania.
“Tunaweza kufanya mengi mazuri na kurudi kwenye
mstari,” kocha huyo mwenye miaka 63 aliwaambia waandishi wa habari nchini
Hispania.
“Tutajitahidi kutetea ubingwa wetu wa mataifa ya
ulaya. Mabadiliko ya mfumo sio lazima, badala yake tunatakiwa kuendelea na
mfumo wetu kwa kuongeza mabadiliko kidogo”.
Kocha huyo wa zamani wa Real Madrid aliyemrithi
Luis Araggones baada ya ubingwa wa fainali za Euro 2008, aliiongoza Hispania
kwa mafanikio katika fainali za mataifa ya ulaya za mwaka 2012 na za kombe la
dunia mwaka 2010.
“Nimekuwa katika mawasiliano na shirikisho wakati
huu mgumu na wamefikiria kuwa mafanikio ya miaka sita iliyopita ni muhimu zaidi
kuliko matokea mabaya katika mechi mbili,” alisema Del Bosque ambaye mkataba
wake unaisha mwaka 2016.
“Shirikisho lina mtazamo chanya na wanathamini
kazi yangu. Tunajiona imara na tutaendelea kufanya kazi yetu kama awali”.
“Tunajipanga vizuri na tutafanya baadhi ya mabadiliko katika timu
yetu kama tulivyofanya siku za nyuma”.
0 comments:
Post a Comment