Na Baraka Mpenja, Mbeya
Imechapishwa Julai 28, 2014, saa 11:34 jioni
DHAHIRI Mbeya City fc imeharibiwa mpango wake wa kucheza mechi
za kirafiki katika nchi za Zambia na Malawi kufuatia shirikisho la soka
Tanzania, TFF, kupiga teke ratiba ya ligi kuu mpaka septemba 20 mwaka huu.
Kocha mkuu wa klabu hiyo Juma Mwambusi anakiri wazi kuwa kusogeza
mbele ligi kuu kumeathiri mipango mingi ya maandalizi ikiwemo ratiba ya kucheza
mechi za kirafiki nchi jirani.
Awali Mwambusi alikuwa na mpango ya kucheza mechi mbili nchini
Zambia, halafu baadaye mbili Malawi, lakini sasa imekuwa ngumu kwasababu hata
wapinzani wao katika nchi hizo watakuwa na ratiba nyingine.
“Kusogezwa mbele ligi kuu kumetuharibia mipango yetu mingi ya
maandalizi, kuhusu mechi za kimataifa za kirafiki, sasa itategemeana na nafasi yao kama tunataka kuwaomba tena kucheza,”
alisema Mwambusi.
Mwambusi aliongeza kuwa bajeti ya timu kuwa ndogo kumemfanya
avunje kambi ya maandalizi na kuwapa likizo wachezaji wake.
Mbeya City fc ni moja ya timu zilizofanya vizuri msimu uliopita
kwa kushika nafasi ya tatu baada ya kujikusanyia pointi 49.
City ilishinda mechi 13, ilitoka sare mechi 10 na kufungwa mechi
3. Ilifunga mabao 33 na kufungwa mabao
20, hivyo wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa kuwa 13.
Mbeya City ilifanikiwa kumaliza mzunguko wa kwanza bila kufungwa
mechi yoyote, lakini mzunguko wa pili ilifungwa mechi tatu dhidi ya Yanga,
Coastal Union na Azam fc.
Timu zilizoshika nafasi ya kwanza mpaka ya nne kwa maana ya
Azam, Yanga, na Simba, ni mabingwa Azam pekee waliweza kutoka na pointi tatu
katika dimba la Sokoine jijini Mbeya.
Simba na Yanga ziliambulia pointi moja tu, lakini Mnyama
alishindwa kushinda hata Dar es salaam na kutoka sare ya 2-2, wakati Yanga
walishinda bao 1-0 dhidi ya Mbeya City.
Azam waliifunga Mbeya City mabao 2-1 uwanja wa Sokoine, wakati
Coastal Union wao waliwafunga mabao 2-0 katika dimba la Mkwakwani jijini Tanga.
Msimu ujao, Mbeya City fc wanatazamiwa kuwa washindani wa
ubingwa kutokana na wachezaji wake wa kikosi cha kwanza kubakia na kuongeza nguvu
kidogo ikiwemo kumsajili mshambuliaji wa Kagera Sugar, Them Felix `Mnyama`.
0 comments:
Post a Comment