Watashinda?: Taifa Stars wakiwa chini ya Mart Nooij watachuana na Msumbiji julai 20 mwaka huu ndani ya uwanja wa Taifa.
Na Baraka
Mpenja, Dar es salaam
0712461976
Imechapishwa Julai 13, 2014, saa 9:47 alasiri
TIMU ya Taifa
ya Tanzania, Taifa Stars, ipo kambini Tukuyu, mkoani Mbeya kujiandaa na mchezo wa kuwania kupangwa hatua
ya makundi ya kusaka tiketi ya fainali za mataifa ya Afrika, AFCON
zikazofanyika mwakani nchini Morocco.
Stars chini ya
kocha Mart Nooij baaada ya kambi ya wiki mbili nchini Botswana aliamua kuweka kambi Tukuyu ili afanye mazoezi
sehemu ya baridi kama ilivyokuwa Gaborone kwa sababu za kitaalamu.
Nooij ataiongozo
Stars katika mechi ya tatu ya mashindano dhidi ya Msumbuji ndani ya dimba la
Taifa jijini Dar es salaam, julai 20 mwaka huu. Mechi ya marudiano itachezwa
wiki mbili baadaye mjini Maputo nchini Msumbiji.
Mwaka 2007,
Taifa stars iliyokuwa chini ya kocha Marcio Maximo ilifungwa bao 1-0 uwanja wa Taifa , jijini Dar es salaam katika
mchezo wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika mwaka 2008 nchini Ghana.
Kwa wenye
kumbukumbu, bao la mapema la nahodha wa wakati huo wa Msumbiji, Tico Tico
liliyeyusha ndoto za mamilioni ya Watanzania waliokuwa na imani ya kwenda
Ghana. Ulikuwa msumari wa moto kwa Watanzania na wengi walihuzunishwa na
matokeo yale kwasababu ng`ombe mzima alikuwa ameliwa na ulibaki mkia tu.
Atawatungua Msumbiji?: John Bocco `Adebayor` (aliyenyosha vidoke juu) alifunga bao pekee katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Zimbabwe kwenye dimba la Taifa jijini Dar es saalam
`
Miaka miwili
iliyopita, Stars ilikutana na Msumbiji katika mechi ya mtoano kuwania kukata
tiketi ya AFCON mwaka 2013 nchini Afrika kusini.
Kim Poulsen
aliiongoza Stars kupata sare ya 1-1 uwanja wa Taifa, na baadaye wiki mbili
kwenye mechi ya marudiano, timu hizo zilipata matokeo kama hayo. Taifa Stars
ikatupwa nje kwa changamoto ya mkikwaju ya penati ambapo mshambuliaji Mbwana
Samatta alikosa penati yake.
Ukiangalia
matokeo haya ya miaka ya karibuni, ni rahisi kugundua kuwa Msumbiji wamekuwa
wasumbufu kila wanapokutana na Taifa stars. Hata mechi ijayo haitakuwa rahisi
kwa Mart Nooij, hivyo maandalizi ya nguvu yanahitajika.
Kuanza
nyumbani ni jambao jema, lakini lazima timu ijipange kupata matokeo. Kuwa
mwenyeji ni moja ya sababu ya kushinda ingawa sio lazima. Lakini unapokuwa
nyumbani unakuwa na faida nyingi kama vile za kimazingira, mashabiki wengi,
hivyo unakuwa na nguvu ya kufanya vizuri.
Moja ya mbinu
ya kushinda wanayotumia waarabu ni kulazimisha sare ugenini au kufungwa si
zaidi ya bao moja, na wanaenda kumaliza mchezo kwao.
Unapocheza
nyumbani lazima ucheze kwa kujiamini kwamaana ya kulinda lango lako, kumiliki
mpira na kushambulia kwa nguvu ili kupata mtaji mkubwa wa mabao.
Nooij
anatakiwa kushambulia na kupata angalau mabao 3-0 katika mchezo wa nyumbani,
ili akienda Maputo afanye kazi kubwa ya kulinda ushindi, kucheza mpira na
kutengeneza nafasi za kufunga. Ili kupata matokeo, wachezaji wanatakiwa kujifua
kucheza kitimu na si kutegemea mchezaji mmoja mmoja.
Mbwana Samatta atakuja kuongeza nguvu Taifa stars.
Kukaba kwa
pamoja, kushambulia na kuzuia kwa pamoja kutawafanya Black Mambas wakose njia
ya kupata mabao dhidi ya Stars.
Uzalendo
utahitajika kwa wachezaji wa Stars. Kama itatokea timu ikashindwa kucheza
vizuri, lakini mchezaji mmoja mmoja akawa na uwezo wa kuamua matokea, basi
itakuwa jambo jema kuisaidia timu.
Walimu
wanafanya kazi yao vizuri, na zikiwa zimesalia siku 7 tu kushuhudia mechi hiyo,
nao mashabiki wana wajibu mkubwa wa kutengeneza matokeo.
Mashabiki ni
mchezaji wa 12 uwanjani. Kikubwa Watanzania lazima watambue kuwa vijana wa
Taifa stars wanawategemea sana katika mechi hiyo, hivyo wafurike kwa wingi
kuwashangilia.
Kwa kiwano
walichoonesha Stars katika mechi mbili dhidi ya Zimbabwe, kinatoa picha nzuri
kama Nooij atafuta makosa na kuongeza nguvu.
Mechi ya
Harare, Mbwana Samatta hakucheza, lakini mwenzake Ulimwenu alicheza, Mechi
ijayo, Samatta amesema anakuja kuongeza nguvu.
Hii itawapa
presha Msumbiji kwasababu wanamfahamu Samatta na Ulimwengu kupitia TP Mazembe.
Kama watajaribu kuwawekea ulinzi, basi itakuwa nafasi kwa akina Ngassa na Bocco
kuwaadhibu.
Msumbiji watakuwa na kazi kubwa ya kuwazuia Taifa stars.
Beki ya Stars
chini ya nahodha Nadir Haroub `Cannavaro` imeonekana kuimarika sana. Kuna
vitasa kama Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Kelvin Yondan, Oscar
Joshua, Said Moradi na wengineo. Hawa wanatosha kuisaidia Stars dhidi ya Mambas
Weusi.
Frank Domayo
hatakuwepo katika mechi hiyo, huku Jonas Mkude na Himid Mao wakiwa hatarini
kukosa mechi hiyo kutokana na majeruhi. Lakini kuitwa kwa mkongwe, Shaban Nditi
kutaifanya Stars kuwa salama eneo la kiungo.
Kwa safu ya
ushambuliaji, kama Ulimwengu na Samatta watakuwepo na kuwa katika viwango vyao
vya TP Mazembe, naamini wataweza kufanya kazi nzuri sambamba na Mrisho Ngassa,
John Bocco, Mwegane Yeya na wengineo.
Timu lazima
iandaliwe kucheza kwa pamoja na lazima wachezaji wawekwe sawa kisaikolojia ili
kama itatokea kufungwa goli la mapema, watulie na kutafua kusawazisha na
hatimaye kupata magoli ya ushindi.
Kila la Kheri
Taifa stars katika maandalizi yenu dhidi ya Msumbiji, mamilioni ya watanzania wapo
nyuma yenu.
0 comments:
Post a Comment