Na
Baraka Mpenja, Dar es salaam
Tel: 0712461976
Imechapishwa Juni 2, 2014, saa 6: 09 mchana
YANGA SC ipo katika mchakato wa kusaka kocha mkuu ili kuziba pengo lililoachwa wazi na Mholanzi, Hans Van der Pluijm aliyetimkia Saudi Arabia baada ya kumalizika kwa msimu wa 2013/2014 wa ligi kuu soka Tanzania bara.
Hata
hivyo, Pluijm alikuwa na mkataba mfupi wa miezi sita na baada ya kumaliza,
hakuona haja ya kuongeza kwa sababu alikuwa amepata kazi mpya Uarabuni.
Namna
ambavyo Pluijm aliondoka Yanga, lilikuwa
jambo jema kwasababu walikaa meza moja, wakaongea, akawaeleza nia yake ya
kutaka kuondoka na viongozi wa Yanaga wakabariki.
Aliondoka
`kiroho safi` na hakukuwa na tatizo lolote baina yake na viongozi wa Yanga.
Pluijm alifika mbali na kuwaahidi Yanga kuwa atawasaidia kupata wachezaji nyota
kutoka nchini Ghana alikofanya kazi miaka ya nyuma.
Kuondoka
kwa Pluijm kumewalazimu Yanga kuhaha kusaka mrithi wake na jana katika mkutano
wa mabadiliko ya katiba uliofanyika kwenye bwalo la maofisa wa Polisi Osterbay
jijini Dar es salaam, mwenyekiti wa Yanga, Yufus Manji amesema Kamati ya
Mashindano imemkabidhi mapendekezo yao na kwa sasa yupo kwenye mazungumzo na
Marcio Maximo aliyewahi kuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania kuja
kukinoa kikosi cha Jangwani.
Suala
la Maximo kuhusishwa na mpango wa kurejea nchini kwa majukumu ya kuinoa Yanga
halijaanza jana wala juzi. Tetesi hizi zilikuwepo mwaka 2012 ambapo alikuwa
anatajwa kuja kurithi mikoba Mserbia, Kosta Papic, lakini kibarua kikaangukia
mikononi mwa Mbelgiji, Tom Saintfiet.
Hakika
ujio wa Maximo kwa wakati ule ulivuta hisia za mashabiki wa Yanga na watanzania
wengi waliokuwa na mapenzi makubwa kwa kocha huyo wakati alipokuwa anafanya
kazi Taifa stars, lakini ndoto za wengi kumuona Marcio zilizima ghafla baada ya
uongozi wa Yanga kumleta Saintfiet.
Sasa
Yanga wapo katika jaribio la pili kumleta Maximo. Kama bosi mwenyewe ndiye
ameshikilia suala hilo, kuna uwezekano mkubwa wa Brazil huyo kutua jangwani.
Juni
29, 2006, Maximo aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya Tanzania, Taifa Stars. Uteuzi
wa kocha huyo ulitokana na ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Jakaya Mrisho Kikwete ambaye alisema serikali yake italeta kocha wa timu ya
taifa ya Tanzania.
Mhe. Kikwete
aliahidi kuliokoa soka la Tanzania na kusema serikali yake itakuwa inalipa
mshahara wa kocha na mambo mengine ya msingi. Alifanikisha dhamira yake baada
ya kumleta Maximo kutoka nchi inayonukia soka, Brazil.
Wakati
Maximo anakuja Tanzania, Taifa Stars ilikuwa hofi bin taabani. Soka letu
lilikuwa bovu na mashabiki wa soka walikuwa wameshakata tamaa na timu yao.
Haikuwa
rahisi kuwakuta mashabiki kwenye mechi za Taifa stars kwenye uwanja wa `Shamba
la Bibi`. Kila kukicha kauli ilikuwa `Tanzania ni kichwa cha mwendawazimu`.
Ni
Maximo aliyekuja kuwaunganisha tena mashabiki wa soka nchini. Alifanya kazi ya
kuiboresha Taifa stars kwa kiwango kikubwa. Timu ilipendwa chini ya Maximo. Mashabiki
walifurika uwanjani na kuishangilia Taifa stars.
Maximo
alifanya kazi kubwa na mwaka 2009 aliisaidia Taifa Stars kufuzu fainali za
mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani, CHAN.
Fainali hizi zilifanyika nchini Ivory Coast
kuanzia February 22 mpaka machi 8 mwaka 2009. Tanzania ilifuzu baada ya kuitoa
Sudan kwa wastani wa mabao 5-2.
Wakati
huo, mashabiki wengi walibadilisha mtazamo wao kuhusu timu ya taifa. Waliipenda
na nyimbo mbalimbali zilitungwa kuwasapoti wachezaji na kumshangilia Maximo.
Baada
ya fainali za CHAN, Maximo aliongeza
mkataba wake na TFF mpaka mwezi julai 2010, lakini baadaye aliondoka na mikoba
yake kuchukuliwa na Jan Borge Poulsen.
Kuondoka
kwa Maximo kulichukuliwa kwa mitazamo tofauti. Wengine walisema kocha huyo
ameishiwa uwezo wa kuisogeza mbele zaidi Tanzania. Yaani mbinu zake zimefika
kikomo. Lakini wengine walipinga na kudai kocha huyo angepewa muda zaidi.
Desemba
mwaka jana aliteuliwa kuwa kocha wa klabu ya Brazili ya Democrata. Alifukuzwa
kazi katika klabu hiyo desemba 13 mwaka 2012.
Mwezi
juni 2012 alikuwa kwenye tetesi za kumrithi Kosta Papic katika klabu ya Yanga,
lakini kazi hiyo ilitua mikononi mwa Mbelgiji, Tom Sainfiet. Lakini mwezi
novemba 2012 alichagua kukaa Brazil ambapo anaiongoza klabu ya Francana.
Tangu
Maximo aondoke, Taifa Stars haijawa na mvuto kama kipindi chake. Watu
wanaipenda timu, lakini huwezi kufananisha na kipindi kile.
Inawezekana
Maximo alikuwa na mvuto kwasababu aliitoa timu shimoni na kuipandisha sehemu fulani,
wakati wenzake waliikuta ikiwa sehemu fulani.
Marcio
Maximo anaweza kutua nchini safari hii kwa majukumu ya ngazi ya klabu. Binafsi
naona litakuwa jambo jema kwasababu ni kocha mzuri.
Uzuri
wa Maximo kwa klabu ya Yanga na soka la Tanzania unatokana na mambo mengi, lakini machache kati ya hayo
ni haya hapa;
Mosi:
Ni Kocha mwenye mvuto kwa mashabiki; duniani kote, kocha akiwa na mvuto lazima
atapendwa na mashabiki. Leo hii angalia Jose Mourinho anavyopendwa na mashabiki
na waandishi wa habari. Kuna faida ya kocha kuwa na mvuto akiwa kazini. Hii
inapandisha morali ya wachezaji na mashabiki katika kuisaidia timu.
Enzi
zake akiwa Tanzania, Maximo alikuwa anazungumzwa kila kona. Alikuwa anaimbwa na
mashabiki dakika zote uwanjani. Watu walimpenda kwa kazi yake. Hii ilisababisha
muunganiko mkubwa kupitia jina lake. Hata waandishi wa habari walipenda sana
kumhoji kocha huyu. Alijua kuongea na waandishi wa habari na alijua kucheza na
maneno. Aliwatia hamasa mashabiki kwa maneno yake matamu na watu walifurika
uwanjani kushuhudia matokeo ya maneno yake.
Mvuto
ni jambo muhimu mno kwenye timu. Kama Maximo atakuja na kasi ile ya Taifa stars
katika klabu ya Yanga, hakika mitaa ya jangwani itakuwa na shamrashamra kubwa
wakati wa uongozi wake.
Pili;
ni kocha mwenye msimamo mkali. Maximo ana falsafa yake ya kazi. Hataki hata
siku moja kuingiliwa katika maamuzi yake. Unakumbuka alivyoweka ngumu
kumuingiza Mrisho Ngassa katika kikosi cha Stars?. Watu waliongea mengi, lakini
akasema siwezi kumuingiza mchezaji timu ya taifa kwa kumuangalia mechi moja tu.
Lakini baadaye alipojiridhisha alimuita. Pia alizinguana na Juma Kaseja nchini
Senegal alipofungwa mabao 4-0, kutoka hapo alisema hatamuita tena Kaseja na
alifanya hivyo.
Msimamo
wa Maximo umejikita katika nidhamu. Kama mchezaji hana nidhamu kwa mujibu wa
vigezo vyake, hawezi kucheza chini yake. Kama atakuja Yanga, basi atawanyoosha
baadhi ya wachezaji wasiokuwa na nidhamu. Maximo hana masihara katika kazi
yake. Maamuzi yake ni magumu. Na viongozi wa Yanga wajipanga kumuacha afanye
kazi yake.
Tatu;
Maximo ni kocha anayejua mbinu ya kulinda lango lake. Enzi zake akiwa Taifa
stars, safu ya ulinzi ilikuwa imara mno. Achana na kipigo cha mabao 4-0
alichopata nchini Senegal, Maximo hakuwahi kufungwa zaidi ya mabao 2 katika
mechi zote za mashindano.
Alisuka
safu bora ya ulinzi iliyosheheni wachezaji wenye nidhamu kubwa ya mchezo kama
Shadrack Nsajigwa, Nadir Haroub `Canavaro`, Meck Mexime, Salum Swedi `Kussi`,
Victor Costa `Nyumba` na wengineo.
Soka
la kisasa linahitaji timu ijilinde, icheze mpira na kushambulia. Kanuni hii
ndiyo inayotumiwa duniani kote. Ili timu ishinde, lazime ijilinde sehemu yake
ya ulinzi, lazima imiliki na kucheza mpira na kushambulia ili kupata mabao.
Kama
unashindwa kujilinda, utafunga lakini utafungwa zaidi. Ili kupata matokeo lazima
uwe na safu nzuri ya ulinzi. Kwa aina ya mabeki waliopo Yanga kwa sasa, kama
Maximo atapewa kazi na kukaa nao, Yanga inawezekana Yanga ikwa na safu bora mno ya ulinzi kwasababu ndio staili
ya mwalimu huyo.
Nne;
Maximo anaijua vizuri Tanzania, anajua utamaduni wa mashabiki wa Tanzania
kwasababu alikaa muda mrefu nchini. Anajua namna ya kuwakonga nyoyo mashabiki
na kuwakera mashabiki wa Tanzania.
Kutokana
na uzoefu wake na soka la Tanzania, inakuwa rahisi kuendana na mfumo mzima. Kwa
hili Maximo atafanikiwa na Yanga watakuwa chini ya kocha mzuri.
Pia
Maximo ni mtu wa watu. Anajua kuishi na watu. Ndio maana aliigiza moja ya
filamu nchini Tanzania. Haya yalikuwa mambo nje ya taaluma yake, anajua kukaa
na watu na anapendwa na watu kila anapofanya kazi.
Yapo
mambo mengi ambayo nitaendelea kukueleza kuhusu Maximo, lakini nimalizie makala
hii kwa kutoa tahadhari kwa Yanga.
Maximo
anaweza kuja Tanzania, hatukatai!, lakini lazima Yanga wajiandae kwa mambo
mawili.
Maximo
anaweza kufanikiwa au asifanikiwe. Mpira umebadilika na katika maisha ya ukocha
kuna kushindwa pia.
Kocha
anaweza kuwa na historia nzuri, lakini akashindwa kufanya vizuri kwasasa.
Kwahiyo, Maximo anapokuja, mashabiki na viongozi wa Yanga wasitegemea makubwa.
Anatakiwa kuaminiwa na kumuacha aweke mipango yake kwa mujibu ya falsafa yake
ya ufundishaji. Yanga wasije kuwa na papara.
Kila
la Heri Yanga katika mchakato huo wa kusaka kocha mpya. Kama mtafanikiwa
kumleta Maximo,hakika mtatukumbusha mambo matamu ya Mbrazil huyu.
0 comments:
Post a Comment