Mtadanganyika?: Wanachama wa Simba jiepusheni na siasa nyepesi za wagombea. Tumieni muda kutafakari sera za wagombea.
Na Baraka Mpenja, Dar
es Salaam
0712461976
Imechapishwa Juni 22, 2014, saa 3:30 asubuhi
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) baada ya kupokea na kuzingatia maombi ya Simba na kwa kuzingatia Ibara ya 26 ya Kanuni za Uchaguzi za TFF toleo la 2013 limeiruhusu klabu hiyo kuendelea na mchakato wa uchaguzi wao uliopangwa kufanyika Juni 29 mwaka huu.
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) baada ya kupokea na kuzingatia maombi ya Simba na kwa kuzingatia Ibara ya 26 ya Kanuni za Uchaguzi za TFF toleo la 2013 limeiruhusu klabu hiyo kuendelea na mchakato wa uchaguzi wao uliopangwa kufanyika Juni 29 mwaka huu.
Hata hivyo, TFF inawahimiza wanachama wa klabu ya
Simba kuwa watulivu na wafanye uchaguzi wao kwa amani.
Taarifa hizi kwa asilimia 100 ni njema kwa wanachama,
mashabiki, viongozi, wafadhili na wadhamini wa klabu ya Simba sc.
Watu wote wanaopenda ustawi wa mpira wa nchi hii
walitegemea busara za Rais wa TFF, Jamal Emil Malinzi ambaye alitangaza
kusimamisha uchaguzi huo jumapili iliyopita. Kauli yake ilizua utata miongoni
mwa wanasimba na yakazungumzwa mengi, lakini usikivu wa Malinzi umefanikisha
ndoto za Wanasimba kupata viongozi wao juni 29.
Juhudi za Rais wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage
zimewasha taa ya kijani kwa Simba baada ya kumuomba Malinzi maandalizi ya
uchaguzi yaendelee na hatimaye kufanyika juni 29 kama ulivyopanga. Ingekuwa
mbaya kama uchaguzi usingefanyika siku hiyo kwasababu klabu inahitaji viongozi
ili usajili uanze na maandalizi ya msimu mpya wa ligi kuu.
Zoezi linalosubiriwa kwasasa ni kuzinduliwa kwa
kampeni ili kila mgombea anadi sera zake na kuwajulisha wanasimba kwanini
anaomba nafasi ya uongozi.
Nafasi mbili za juu, Urais na makamu wa Rais zinavuta
hisia za wanachama wengi, lakini kuondoshwa kwa Michael Richard Wambura,
kumewaacha Evance Aveva na Andrew Tupa kupambana.
Simba iliyoifunga Yanga mabao 5-0 ilikuwa yenye ubora, lakini kwa miaka miwili iliyopita, mambo yakekuwa magumu
Safari ya kuenguliwa kwa Wambura ilikuwa na mizengwe
mingi na ilisababisha mvutano mkubwa ndani ya klabu ya Simba, lakini mwisho wa
siku sheria na kanuni zimetoa jibu.
Ni imani yangu kuwa utulivu utakuwepo na wale
waliokuwa wanamuunga mkono Wambura watakuwa wavumilivu kwasababu kila
unaposhindana lazima ukumbuke kuna kushinda na kushindwa.
Tatizo la watu wengi wanawaza kushinda tu, lakini
kushindwa wanaona kama ni dhambi. Penda kushindwa, halafu jipange upya. Ukiwa
mtu wa kuwaza kushinda tu, ukishindwa `unapaniki` na hatimaye kushindwa kabisa
kabisa!.
Wanachama wa Simba mnatakiwa kuvunja kundi la Wambura
na kushirikiana kwa pamoja ili juni 29 mpate mtu atakayewaunganisha na kuifanya
Simba kuwa imara. Naamini uchungu mlioupata kwa miaka miwili sasa unatosha na
kuna haja ya kuijenga Simba ya ushindani.
Kwa kuanzia, lazima mpate viongozi sahihi, wenye
mtazamo sahihi na watakowafanya mpige hatua kwenda mbele.
Kampeni zinaanza juni 24 mwaka huu kwa mujibu wa
ratiba iliyotolewa na kamati ya uchaguzi chini ya wakili, Dkt. Damas Daniel
Ndumbaro.
Niwakumbushe kitu kimoja tu,kampeni ni nafasi ya
mgombea kunadi sera, mipango na kueleza
kwanini anagombea. Pia anaweza kueleza jinsi atakavyotekeleza sera zake na
kufanikiwa.
Katika chaguzi za kidemokrasia, Kampeni ndio muda
unaowafanya watu wapate viongozi bora na bomu. Hapa ndipo siasa ilipolalia.
Ushawishi huwa ni mkubwa na kudanganywa pia kupo.
Wanachama wa Simba sc juni 29 mwaka huu mna mamlaka makubwa kikatiba kuamua nani aingia na nani atoke.
Mara nyingi, wagombea wengi wanapenda kuongea mambo
yanayovutia na kushawishi. Usipokuwa makini unaweza kumchagua mtu mwenye maneno
mazuri, lakini ikifika wakati wa utekelezaji, mambo yanageuka.
Najua kwa muda wote huu, wagombea wote wamekuwa
wakiandika na kuandikiwa cha kuzungumza mbele ya wanachama wa Simba. Najua
yatazungumzwa mengi kutoka kwa wagombea, lakini umakini wa wanachama ndio
utachambua mtu sahihi wa kumpa kura.
Wapo watakaosema lazima wajenge uwanja wa kisasa,
wauze jezi za klabu kwa faida ya timu, wataifanya klabu kuwa bora uwanjani kwa
kusajili wachezaji wazuri, kuifanya Simba ijitegemee na mengine mengi.
Sina shaka na mtu atakayesema haya kati ya mengi
yatakayosikika. Najua kweli Simba inahitaji mambo kama hayo na mengine mengi.
Lakini mwisho wa siku, kuna kitu kinaitwa `sera au
ahadi zisizotekelezeka`. Hapa lazima wanachama wa Simba kuwa makini ili msije
kujenga imani kubwa na mgombea fulani kwasababu ya sera zake, kumbe
hazitekelezeki.
Lazima upime uwezo wa klabu yenu kifedha, halafu pima uwezo
wa mgombea anayezungumza, halafu dadavua kama kweli anaweza kufanikiwa
anayozungumza.
Sisemi uwezo wa kifedha hapa, nazungumzia utashi,
uimara na ujanja ujanja wa kutafuta njia
za kupata fedha kwa faida ya Simba. Mgombea mwenye uwezo wa kuhangaika kwa
ajili ya klabu kwa kuzungumza na makampuni, wadhamini na wafadhili ili
aitunishe akaunti ya timu kwa matumizi tofauti tofauti.
Moja ya siri ya kufanikiwa kwa kiongozi ni kuchagua
mambo machache kwa muda ulionao na kuyatekeleza ipasavyo. Lakini kwa siasa za
Tanzania, mgombea anaahidi mambo 10 anatekeleza matatu au hatekelezi yote.
Ikifikia wakati wa uchaguzi anajipanga na uongo mwingine.
Kiongozi bora ni Yule anayekuwa na malengo machache
ndani ya muda mfupi. Kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi, anajikita kwenye
ahadi zake chache na akiweza, atajijengea heshima.
Wanachama wa Simba, pimeni sera za wagombea wenu na
kuzichambua kama zinatekelezeka. Msije mkajidanganya na kuwaamini kwa maneno ya
mdomoni, lakini kiuhalisia hayawezekani.
Alhaj Ismail Aden Rage anaondoka madarakani na amefanya kazi nzuri kuhakikisha uchaguzi unafanyika tarehe iliyopangwa.
Wapo watu kazi yao ni kuandaa sera za wagombea. Wana
uwezo mkubwa wa kuandaa mipango yenye mvuto, lakini utekelezaji wake unakuwa
mgumu kwasababu wanaandika tu bila kuangalia mazingira ya pale wanapoenda
kuongoza.
Maneno si kigezo cha kumuamini mtu, lazima ujua
anawezaje kufanikiwa kwa mazingira mliyonayo kwenye klabu.
Kwa wagombea, ogopeni kudanganya watu wazima. Kama
kweli mna nia ya dhati kuindeleza klabu ya Simba, njooni na sera
zinazotekelezeka na ambazo zipo chini ya uwezo wenu. Sio mnakuja na mambo
mazito ambayo Simba haiwezi kuyabeba.
Kama mtadanganya na kushindwa kufikia malengo yenu,
mjiandae kuingia katika orodha ya wanasiasa waliovamia mpira bila kuwa na nia
ya kweli. Ni imani yangu kuwa mmeomba nafasi kwasababu mnataka kufanya kazi
nzuri.
Simba inahitaji mabadiliko baada ya kupitia kipindi
kigumu cha miaka miwili. Kila atakayepewa nafasi, basi awajibike vizuri.
Wanachama wa Simba, juni 29 mna mamlaka makubwa
kikatiba. Ninyi ndio mtashika rungu na kuamua nani anaingia nani anatoka. Msichague
kwa kushawishika na wenzenu.
Kura ni siri ya mtu na lazima iwe siri. Kama mtu
anatoka ndani ya chumba cha kupigia kura anatakiwa aendelee na mambo yake, sio
anamwambia mwenzake, mimi nimemchagua fulani, nawewe kumchague. Kila mtu aingie
kivyake na kufanya yake
Kila la heri wana Simba kuelekea uchaguzi wenu wa Juni
29. Amani na iwe nanyi kwa wakati huu muhimu.
0 comments:
Post a Comment