
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Juni 10, 2014, saa 10:30 asubuhi
KAMATI ya rufani ya shirikisho la kandanda
Tanzania, TFF chini ya mwenyekiti wake, mwanasheria Julius Lugaziya leo mchana
inaendelea kumalizia kujadili rufani ya mgombea aliyeenguliwa kuwania nafasi ya
urais katika uchaguzi wa Simba unaotarajia kufanyika juni 29 mwaka huu, Michael
Richard Wambura.
Kikao cha kamati hiyo kilianza jana majira ya saa
5:00 asubuhi katika hoteli ya Courtyard, Upanga, jijini Dar es salam na kuahirishwa saa 4:30
usiku, lakini ngoma ililala bila kufikia maamuzi na leo hii kamati inatarajia
kukutana tena saa 6:00 mchana ili kumalizia na kufikia maamuzi ya mwisho.
Hamu ya wadau wengi wa soka na wanachama wa Simba
wanahitaji kufahamu kama Wambura anarudishwa au anaondolewa rasmi katika
kinyang`anyiro hicho.
Jana kamati ya Lugaziya alifikia sehemu nzuri kwa
kuhoji pande zote mbili kwa maana ya wakata rufaa na wakatiwa rufaa na leo
wanaanza kupitia maelezo yao na kuyapima uzito na kufanya maamuzi.
Mtandao huu umekuwa ukipokea simu na jumbe fupi za
simu kutoka kwa wadau wake wakiuliza nini maamuzi ya kamati ya rufani ya TFF iliyokutana
jana.
Jana timu yetu ilipiga kambi maeneo ya Courtyard
kufuatilia `ngado kwa ngado` kinachoendelea kwenye kamati hiyo ili kuja na jibu
sahihi, lakini kulikuwa na usiri mkubwa mno, japokuwa kila mtu alikuwa anasema
lake.
Hata siku moja, mtandao huu hauandiki taarifa
ambayo haijathibitishwa na vyonzo makini.
Ukipita kwenye mitandao ya kijamii, watu wengi
wanaandika kuwa Wambura karudishwa wengine wanasema kaondolewa.
Taarifa hizi si rasmi kwasababu maamuzi
hayajafikiwa mpaka sasa.
Kuna uwezekano hatima ya Wambura ikajulikana leo
jioni, kwahiyo wadau wetu kuweni na subira.
Taarifa za kwenye mitandao si za kiziamini kwa
asilimia zote kwasababu kuna uhuru wa kuandika na kuchapisha habari. Wengine
wapo kwa ajili ya kuwavutia wasomaji, lakini sisi hatufanyi kazi kwa misingi
hiyo.
Hatujapata taarifa rasmi na wahusika walisema
wanakaa tena leo, kwa maana hiyo taarifa rasmi itatoka leo.
Asante kwa kuwa nasi na tutazidi kuwafahamisheni
kinachoendelea kwa wakati huu.
0 comments:
Post a Comment