Na Baraka Mpenja, Dar
es saaam
0712461976
KAMATI ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) inakaa kesho Jumatatu (Juni 9 mwaka huu) kusikiliza rufani
moja inayopinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba SC.
Michael Wambura amewasilisha rufani yake TFF akipinga
uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba iliyomwengua katika kinyang’anyiro cha
kuwania urais katika uchaguzi wa klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika juni 29
mwaka huu.
Kamati hiyo inayoongozwa na Wakili Julius Lugaziya
itakutana saa 5 asubuhi kwenye hoteli ya Courtyard iliyopo Upanga, jijini Dar
es Salaam.
Wanachama wengi wa Simba na wadau wa soka kwa ujumla
wanasubiri kuona nini kitatokea kesho katika kikao hicho. Swali kubwa ni je,
Wambura atarudishwa kwenye uchaguzi au rafana yake itapigwa chini?
Majibu ni hapo kesho. Sinema kubwa ilitokea muda mfupi
baada ya Wambura kuondolewa katika mchakato wa uchaguzi wa Simba. Wambura aliingia
katika vita ya maneno na mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi, Wakili Dkt. Damas Ndumbaro.
Wanaume hawa walishambuliana vikali na kuvuka mipaka
na kuingia katika maisha binafsi. Wakacha mambo ya uchaguzi na kuanza
kudhalilishana kwenye vyombo vya habari mpaka pale Wambura alipoamua kutumia
busara yake.
Kwenye mkutano wa mwisho na waandishi wa habari, watu
wengi walitegemea Wambura angejibu mapigo ya maneno mazito ya Ndumbaro, lakini
aliendeshwa na busara na hapo sinema ikatulia.
Sasa kesho, uchaguzi wa Simba unaanza kuingia sura mpya
hasa kuhusiana na kuondolewa kwa Wambura. Tayari baadhi ya wanachama wa Simba
walishaanza kumlaumu Malinzi kuwa anambeba Wambura na wengine wameripotiwa
kumshitaki FIFA.
Lakini mwisho wa siku kila kitu kujulikana kesho. Ni
ndumbaro au Wambura?.
Wambura anahangaika na kigingi cha kuipeleka Simba
mahakamani kinyume na sheria za mpira. Alijitetea wakati wa pingamizi lakini
ikashindikana. Pia suala la kusimamishwa uanachama mwaka 2010 lilimsumbua sana,
ila kuna utata katika hili.
Maamuzi ya kamati ya Ndumbaro kujadiliwa kesho TFF
Wambura alisema kamati ya Ndumbaro haikumtendea haki
na ndio maana alikata rufaa kwa kuweka sababu 14 za kupinga kuenguliwa kwa jina
lake.
Huyu bwana ana hoja zake na kesho kamati ya TFF
itazichambua na kufikia maamuzi. Majibu ya kamati yanasubiriwa kwa hamu kubwa
kwasababu Wambura ni miongoni mwa wagombea waliokuwa na mvuto mkubwa.
Wambura ana watu wengi nyuma yake. Watu waliandamana
kwa ajili yake, watu wamemtete kwa kila namna. Wanachama wanataka agombee ili
kupambana na Evans Aveva na Andrew Tupa.
Inaonekana kutakuwa na vita kubwa kati ya Aveva na
Wambura kama watasimama katika uchaguzi. Wawili hawa wana watu wengi nyuma yao.
Wanaompenda Aveva wakiwemo watu wenye ushawishi mkubwa
Simba kama Zacharia Hans Poppe wanaeleza sababu nyingi za kutaka Aveva awe Rais
wa Simba.
Wanasema katika enzi zake za kusimamia kamati ya
usajili, Simba ilikuwa kali na haijawahi kutokea.
Lakini mtu kama Poppe anaposema anataka Aveva ashinde
ili wafanye kazi nzuri kwasababu wana mtazamo unaofanna, inakuwa ngumu kujua ni
mtazamo upi na kwa faida ya nani.
Yeye alishasema msimamo wake mapema kuwa kama Aveva na
Kaburu hawatachaguliwa, hatakuwa tayari kufanya kazi na viongozi wengine.
Hawa waliandamana kupinga kuenguliwa kwa Wambura
Poppe alisema amechoka kupoteza muda wake na fedha
zake kwa Simba, hivyo anataka watu watakaofanya kazi kwa faida.
Ni dhahiri kuna watu `wanapiga hela` Simba sc. Ni kundi
la watu fulani linalochumia matumbo yao. Kundi hili halina mpango na klabu hii
kongwe.
Hawa ndio Wambura analia nao. Kila kukicha anasema
yeye akipita katika nafasi ya urais ataiondoa Simba kwenye mikono ya wachache
na kuwa klabu inayojitegemea.
Pia anasema atatumia rasimali za Simba kuifanya kuwa klabu
yenye uwezo mkubwa kiuchumi. Anataja kutumia vitu kama nembo ya Simba kujiingizia
hela, kuuza jezi za klabu, kusimamia mapato kwa faida ya klabu.
Ukikaa na kumsikiliza Wambura, hakika ana mawazo
yanayohitajika kwa Simba. Ni aina ya
kiongozi anayetakiwa. Lakini kama anaweza kufanya hayo, hapo ni kitu kingine.
Mawazo hayapingwi, ni mazuri sana, labda apingwe mtu anayetaka kuyatekeleza.
Lakini hata kama atapita Aveva au Tupa, mawazo haya ya
Wambura ni muhimu mno kwa Simba sc.
Wambura ni mtu wa mpira, yawezekana alishaona jinsi watu wanavyopiga
hela Simba sc. Hawezi kusema tu. Lakini watu wengi wanaonekana kumuamini na
kutaka kumpa nafasi, ingawa kuna vikwazo vingi.
Kama Wambura atavuka kizingiti hicho, basi anaweza
kuwa kiongozi aliyepitia misukosuko mingi zaidi. Lakini kuna mambo yanakosa
majibu, kwa mfano mtu anaposema kwanini
wambura anapingwa kila anapogombea?
Watu wanatumia kupingwa kwake kama mtu ambaye hafai.
Lakini wangapi wanajiuliza ni nani anampinga Wambura na ana malengo gani?
Inawezekana kupeleka masuala ya mpira mahakamani
imekuwa tatizo kwake, lakini tumejiuliza kwanini alifikia maamuzi hayo?, Lazima
kuna watu walifanya vibaya na ndio maana alifikia maamuzi hayo kwa lengo la
kutafuta haki.
Sina lengo la kuzungumzia suala hili, makala hii
inalengo kuwakumbusha wanachama wa Simba, hususani wanaomuunga mkono Wambura
kuwa katika rufaa kuna kushinda na kushindwa.
Yote ni matokeo, hivyo lazima wajiandae kupokea majibu
ya aina yoyote ile ili uchaguzi uendelee.
Kuna watu hawatataka Wambura ashindwe katika rufaa,
lakini kumbuka jambo lolote linakuwa na pande mbili.
Yote
yanawezekana, anaweza kushinda na kurudi katika uchaguzi au akatupwa nje zaidi.
Najua kuna kanuni zinazotumika kuamua. Zipo wazi na
hakuna haja ya kudadidi kwasababu zinaelekeza wazi. Kama watatumia kanuni
vizuri na kutumia vigezo sahihi, basi maamuzi yatatoka vizuri.
Kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF, kumbukeni ninyi
ndio mnaweza kuinusuru Simba. Maamuzi yenu yataweza kuleta mivutano kama
hayatakuwa sahihi.
Jiridhisheni kwa kufuatilia vigezo vyote. Msiwe ni
papara. Nyaraka zote zipitieni kwa uangalifu mkubwa kwasababu amani ya Simba
imebakia mikononi mwenu.
Wadau wanataka kuona Simba inafanikisha uchaguzi wake,
fanyeni maamuzi kwa kuzingatia kanuni.
Wana Simba tulieni katika kipindi hiki, subirini kesho
ili mpate jibu. Wale wanaompenda Wambura, jiandaeni kwa majibu ya aina yote.
Msiwaze kushinda tu, hata kushindwa kupo.
Najua kila majibu yatakuwa na sababu zake. Hivyo
itakuwa busara kusikiliza kwanini jibu fulani limetoka na kufikia maamuzi.
Kila la kheri kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF,
tunawataka kuwa waangalifu na kuepuka kushawishia kinyume na kanuni.
0 comments:
Post a Comment