
Nahodha wa Yanga sc na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa stars, Nadir Haroub `Cannavaro` mwenye jezi namba 13 wakati Stars ilipolazimisha sare ya 2-2 na Zimbabwe mjini Harare.
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Juni 13, 2014, saa 11:59 jioni
KIKOSI cha timu yoyote kinapoingia uwanjani,
lazima awepo kiongozi ambaye hujulikana kwa jina la nahodha.
Nahodha katika timu ni mchezaji anayechaguliwa ndani
ya kikosi kuwa kiongozi wa timu uwanjani: mara nyingi anakuwa mchezaji mkongwe
au mwenye uzoefu kwenye kikosi au mchezaji mwenye ushawishi kwa wenzake.
Nahadho wa timu anafahamika kwa kuvaa kitambaa kwenye mkono wake.
Hata timu ya taifa lazima iwe na nahodha wake kama
ilivyo kwa Nadir Haroub `Cannavaro` ambaye anaiongoza Yanga na Taifa Stars.
Kibongo bongo, nahodha anaonekana mtu wa kawaida,
huku baadhi ya makocha, viongozi na wachezaji wengine wakimchukulia mtu wa
kawaida, lakini kwa wenzetu, unahodha ni cheo kikubwa sana.
Nahodha ni mtu mwenye ushawishi hata kwa kocha wa
timu. Wachezaji wanamheshimu kwa nafasi yake na kumsikiliza kila anapozungumza.
Majukumu rasmi ya nahodha yanayotambuliwa na
sheria za mchezo ni kushiriki kwenye zoezi la urushaji wa shilingi wakati wa
kuchagua magoli pindi mechi inapotaka kuanza na huwa wa kwanza kupiga penati.
Kinyuma na wengi wanavyofikiri, kisheria nahodha
hana mamlaka ya kupinga maamuzi ya mwamuzi. Japokuwa mwamuzi anaweza kuzungumza
na nahodha wa timu yoyote kuhusu tatizo la mchezo pale inapobidi.

Nahodha wa Azam fc, John Raphael Bocco `Adebayor` wa kwanza kulia akiwa ameshikilia kombe la ligi kuu walilotwaa msimu uliopita
Kuna wakati ukienda mitaani kuangalia ndondo,
nahodha anaweza kumkomalia mwamuzi bila kujua hana uwezo huo.
Hii inatokana na watu kutojua wajibu wa nahodha
uwanjani, lakini kupitia makala hii maalum kwa kutoa elimu, kazi za mtu huyu
zitafahamika.
Wakati wa zoezi la ugawaji wa zawadi kwenye mechi
inayoipa ubingwa timu fulani, nahodha ndiye anawaongoza wachezaji wenzake
kuvalishwa medali. Kombe ambalo timu imeshinda, nahodha ndiye wa kwanza
kukabidhiwa na ndiye atakuwa wa kwanza kulinyanyua juu.
Nahodha ndiye mwenye kazi kubwa ya kupandisha
morali ya wachezaji inaposhuka, yeye ndiye mwenye majukumu ya kuwaunganisha
wenzake ili wafanye kazi nzuri wawapo uwanjani.
Nahodha anaweza kuungana na kocha kwenye uteuzi wa
kikosi cha kwanza kwa baadhi ya mechi. Kwenye michezo ya vijana au michezo ya
kawaida ya kujiburudisha, mara nyingi nahodha anakabidhiwa majukumu makubwa
ambayo yanatakiwa kufanywa na kocha.


Nahodha siku zote huwa anakuwa kiungo au beki na mara
chache anaweza anaweza kuwa mlinda mlango au mshambuliaji, na hii inatokana na
sehemu wanazokaa wachezaji hawa na majukumu yao mazito uwanjani.
Nahodha wa klabu anateuliwa kwa msimu. Kama hayupo
au hajachaguliwa kwa ajili ya mchezo fulani, nahodha msaidizi ndiye atateuliwa
kufanya majukumu yake.
Nahodha wa mechi ndiye mtu wa kwanza kubeba kombe
ambalo timu imeshinda hata kama sio nahodha wa klabu. Mfano mzuri ni UEFA ya
mwaka 1999 wakati nahodha wa mechi Peter Schmeichel alinyanyua kombe la
Manchester United kwasababu nahodha Roy Keane alikuwa amesimamishwa.
Mwaka 2012 kwenye michuano ya UEFA, nahodha wa
mechi (ambaye alikuwa nahodha msaidizi) Frank James Lampard kwa pamoja walinyanyua
kombe na John Terry aliyekuwa anatumikia adhabu, lakini alipewa ruhusa maalum
na UEFA.
Nahodha msaidizi ni mchezaji anayetarajia
kuiongoza timu wakati nahodha hajapangwa kwenye kikosi cha kwanza au amekwenda
benchi na kumpisha mchezaji mwingine au amepata kadi nyekundu.
Mara nyingi nahodha msaidizi huwa anateuliwa kuwa
nahodha mkuu pale nahodha anapoondoka katika klabu, mfano Iker Casillas
alimbadili Raul Gonzalez katika klabu ya Real Madrid.
Kwa kifupi huyu ndiye nahodha ambaye anatakiwa
kuheshimika na kuwa na uwezo mkubwa uwanjani na utashi wa kuongoza wenzake.
0 comments:
Post a Comment