Na Boniface Wambura, Dar es salaam
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa
masikitiko kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wake (wakati huo ikiitwa FAT), Kanali
mstaafu Ali Hassan Mwanakatwe kilichotokea leo asubuhi (Juni 7 mwaka huu)
katika Hospitali Kuu ya Jeshi (GMH) Lugalo jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa binti wa marehemu, Sophia, baba yake
alianguka bafuni nyumbani kwake Mbezi Beach ambapo alikimbizwa katika Hospitali
ya Lugalo ambapo ndipo umauti ulipomfika wakati madaktari wakimpatia matibabu.
Kanali Mwanakatwe alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa
Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) katika uchaguzi uliofanyika mwaka 1993
mjini Kibaha mkoani Pwani.
Baada ya kuondoka FAT, aligombea nafasi ya Katibu Mkuu
wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kufanikiwa kushinda
katika uchaguzi uliofanyika mwaka 1997.
Msiba
huo ni mkubwa katika fani ya mpira wa miguu nchini na Afrika kwa ujumla kwani,
Kanali Mwanakatwen enzi za uhai wake alitoa mchango mkubwa akiwa kiongozi, na
mkufunzi wa utawala wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF). Pia aliwahi
kuwa Kamishna wa CAF.
TFF
tunatoa pole kwa familia ya marehemu Kanali Mwanakatwe, DRFA, na Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika
kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Taratibu
za mazishi zinaendelea kufanywa na familia yake nyumbani kwake Mbezi Beach
karibu na hoteli ya Giraffe wakati ndugu wakisubiriwa kutoka mikoani. TFF
tunasubiri taratibu hizo ili tujipange jinsi ya kushiriki katika msiba huo.
Sisi
sote ni waja wake Mola. Hakika kwake tutarejea.
0 comments:
Post a Comment