Rais
wa TFF, Jamal Emil Malinz (kushoto) mkurugenzi wa Plan International, Jorgen
Haldorsen (wa pili kushoto) wakitia sahihi katika mkataba huo mchana wa leo.
(picha na Baraka Mpenja).
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Juni 19, 2014, saa 8:05 mchana
NDOA za utotoni zinawazuia mamilioni ya watoto wa
kike nchini wasiweze kumaliza shule, kufikia ndoto zao katika maisha na
kuwafanya waendelee kuteseka katika umasikini.
Kuna `mijibaba` inayoharibu watoto wa kike bila
huruma na kama haitoshi inaamua kufunga ndoa za `kihuni` na watoto ambao ni
taifa la kesho.
Serikali na mashiriki binafsi ya kutetea haki za
watoto yanapambana dhidi ya tatizo hili, huku wazazi na watu wazima wakiwa
sehemu ya tatizo.
Mpira wa miguu ni mchezo unaoongoza kuwa na
mashabiki wengi nchini na dunia kote, hivyo mchezo huu unaweza kutumika kama
njia ya kupambana na ndoa za utotoni.
Kwa kutambua mchango unaoweza kuletwa na mpira wa
miguu, shirikisho la soka Tanzania, TFF limeingia ubia na shirika la kutetea
haki za watoto la `Plan International` kwa ajili ya kutetea na kuhamasisha juu
ya ulinzi wa haki za mtoto hapa nchini.
Mkataba wa ushirikiano umesainiwa leo katika ofisi
za TFF makao makuu jijini Dar es salaam baina ya Rais wa TFF, Jamal Malinzi na
mkurugenzi wa `Plan International Tanzania`, Jorgen Haldorsen . Ushirikiano huo
una lengo la kufanya kazi pamoja katika kushughulikia masuala ya ukatili wa
kijinsia, ndoa na mimba za utotoni.
Kwa mujibu wa Bw. Haldorsen, soka ndio mchezo
unaongoza nchini na duniani kote kuwa na mashabiki wengi na kwamba joto la
kombe la dunia linaloendelea kule Brazil na namna watanzania wanavyofuatilia
kupitia luninga na wengine wakiwa Brazil ni ushahidi tosha.
“Tunatambua uwezo wa mchezo huu kuwajumuisha watu.
Sasa tunataka tuwajumuishe watu sio tu kwa ajili ya furaha, pia kama njia ya
kuleta mabadiliko juu ya usawa wa kijinsia kwa kutetea na kuhamasisha juu ya
haki za mtoto wa kike”. Alisema Haldorsen.
Mkurugenzi huyo wa `Plan International Tanzania`
alidokeza kuwa ushirikiano na TFF ni sehemu ya kampeni ya kimataifa
inayoendeshwa na shirika hilo ulimwenguni inayoitwa `Because I Am A Girl`-BIAAG
au kwa Kiswahili-KWA SABABU MIMI NI MSICHANA ambapo inalenga kuwatoa mamilioni
ya wasichana kutoka katika umaskini kupitia uhamasishaji juu ya haki zao, elimu
na stadi za maisha.
Rais
wa TFF, Jamal Emil Malinz (kushoto) mkurugenzi wa Plan International, Jorgen
Haldorsen (wa pili kushoto) wakionesha mkataba huo kwa waandishi wa habari
(hawapo pichana). (Picha na Baraka Mpenja)
“Kwa kupita ubia huu tutakuwa na uwezo wa
kuwafikia mamilioni ya Watanzania na tutawapa wasichana ujumbe kuwa KWA SABABI
MIMI NI MSICHANA, lazima nipate fursa sawa na wavulana. KWA SABABU MIMI NI
MSICHANA, lazima niwe na uwezo wa kufunga magoli kufikia ndoto zangu katika
maisha”. Alieleza Bwa.Haldorsen.
Kwa upande wake, Rais wa TFF ambaye ni mjumbe wa kamati
ya Huduma kwa jamii ya Shirikisho la mpira wa miguu Ulimwenguni, FIFA, alisema
ubia huo ni sehemu ya utekelezaji wa sera za huduma kwa jamii ya TFF na wana
furaha kushirikiana na Plan International kwa lengo hili muhimu.
“Ushirikiano huu ni muhimu sana kwetu kwani
unakileta chombo kikubwa kabisa cha michezo hapa nchini pamoja na shirika la
kutetea haki za watoto (plan International) hususani kwa ajili ya haki za mtoto
wa kike. Tunategemea kutumia mtandao wetu nchi nzima kuelimisha juu ya usawa wa
kijinsia na uhamasishaji wa haki za mtoto wa kike,” . Alisema Rais Malinzi.
KUHUSU PLAN INTERNATIONAL: Plan
International ni shirika la kimaendeleo la misaada ya kibinadamu, linalomlenga
mtoto lisilofungamana na mrengo wowote wa kidini, kisiasa au kiserikali.
Plan International ilianzishwa zaidi ya miaka 70
iliyopita na inaendesha shughuli zake katika nchi 70 duniani. Plan
International imekuwa inafanyakazi hapa Tanzania tangu mwaka 1991 ikiwasaidia
watoto na jamii kupata huduma za afya, elimu, maji, usafi na mazingira,
kujikimu na ulinzi. Inaendesha miradi Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Geita,
Pwani, Mwanza na Rukwa.
KAMPENI YA KWA SABABU MIMI NI MSICHANA
–BIAAG: Kampeni ya Kwa Sababu Mimi ni Msichana-BIAAG
(2012-2016) ni kampeni ya Plan ulimwenguni kote inayolenga kuelimisha na
kutetea haki za mtoto wa kike na kuwatoa mamilioni ya wasichana kutoka kwenye
lindi la umaskini kupitia elimu na utoaji wa stadi za maisha na kazi.
Kampeni hii inalenga kupambana na ubaguzi wa
kijinsia na kuboresha maisha ya wasichana milioni 4 duniani na zaidi ya laki 3
hapa Tanzania kwa kuwawezesha kujiunga shuleni, kupata stadi za kiufundi na
maisha, kujikimu, na kushiriki katika shughuli mbalimbali katika jamii na
kulindwa, kwa kukabiliana na vikwazo dhidi ya maendeleo ya mtoto wa kike.
0 comments:
Post a Comment