Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Juni 1, 2014, saa 5: 36 asubuhi
TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars inaingia kibaruani jioni ya leo kuvaana na Zimbabwe katika mchezo wa marudiano , mjini Harare, kuwania kupangwa hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali za kombe la mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco.
Stars wanaingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya
ushindi wa bao 1-0 walilopata uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam. Bao hilo
pekee lilifungwa na John Raphael Bocco `Adebayor`.
Majirani wa Taifa Stars, Kenya na Uganda wamefuzu
hatua inayofuata kutokana na matokeo mazuri waliyopata jana na juzi.
Ijumaa ya wiki hii, Kenya (Harambee stars) walitoka sare ya 1-1 na Comoros ugenini na kusonga
mbele kwa wastani wa mabao 2-1 kwani mechi ya kwanza mjini Nairobi walishinda bao
1-0.
Uganda The Cranes jana waliibuka na ushindi wa bao
1-0 dhidi ya Madagascar na kufanikiwa kusonga mbele kwa wastani wa mabao 2-2,
lakini Uganda walinufaika na bao la ugenini walilopata katika kipigo cha mabao
2-1 nchini Madagascar.
Leo ni zamu ya Tanzania kuonesha maujanja na
kuwaiga majirani zao wa jumuiya ya Afrika mashariki.
Baada ya Taifa stars kuwasili nchini Zimbabwe,
vitendo visivyo vya kiungwana viliripotiwa ikiwa ni pamoja na wachezaji
kufungiwa milango ya Hoteli walipotoka mazoezini kwa madai ya kutolipiwa hoteli
hiyo.
Iliezwa kuwa chama cha soka nchini Zimbabwe
kinadaiwa deni kubwa na Hoteli hiyo ambayo timu yake inaweka kambi mara kadhaa,
hivyo walitaka kulipwa fedha kwanza ili wawaruhusu wachezaji na viongozi
wa Taifa stars kulala hotelini hapo.
Wachambuzi wa mambo wanasema inawezekana zikawa ni
njama za kuwaondoa mchezoni wachezaji wa Taifa stars.
Kikubwa, wachezaji wetu wasichanganyikiwe na njama
hizo kwasababu walishawahi kukumbana na matatizo mengi, ikiwemo kukataliwa
kuingia uwanjani kufanya mazoezi nchini Morocco.
Wachezaji wa Tanzania wanatakiwa kuingia uwanjani
kwa kujiamini, na kukumbuka kuwa mamilioni ya watanzania wapo nyuma yao.
Wasifikiri hawawezi kuwafunga Zimbabwe, wacheze
kwa kutulia na kutumia nafasi muhimu watakazobahatika kupata uwanjani.
Kutoa sare au kushinda inawezekana, hivyo ni
jukumu la wachezaji kuwajibika ipasavyo na kuzingatia maelekezo ya kocha wao,
Mholanzi, Mart Nooij.
Mechi ya ugenini huwa ngumu siku zote.
Unakabiliana na presha kubwa ya wenyeji wako, lakini ukitulia unaweza kupata
matokeo kama kawaida.
Ni dhahiri Zimbabwe watashambulia sana kwasababu
ni watumwa wa kusawazisha bao walilofungwa jijini Dar es salaam, lakini kama
safu ya ulinzi ya Taifa stars itakuwa na utulivu kama mechi mbili -tatu za
nyuma na kufuta makosa madogo madogo, wanaweza kuwazuia Zimbabwe kupata mabao.
Stars wanatakiwa kuondoa hofu, wamiliki mpira,
walinde lango lao na kushambulia kwa kasi ili kupata matokeo mazuri.
Viungo wanatakiwa kubadilika sana, wacheza mipira
kwa kwenda mbele ili kuwapa nafasi washambuliaji kupata nafasi za kufunga.
Watanzania wachache waliosafiri na timu kwenda
Zimbabwe, wakumbuke kuwa wanawawakilisha watanzania wengi ambao hawajapata
nafasi ya kwenda Zimbabwe, hivyo wawe wazalendo na kuwapa moyo wachezaji bila kujali
ni matokeo gani yatakuwa yakiendelea uwanjani.
Kila la kheri Taifa stars katika mechi yenu na
Zimbabwe leo.
0 comments:
Post a Comment