
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Juni 10, 2014, saa 4:56 asubuhi
MAAFANDE wa
Ruvu Shooting wamedhamiria kufanya maajabu katika msimu wa 2014/2015 wa ligi
kuu soka Tanzania bara unaotarajia kuanza kutimua vumbi mwezi agosti mwaka huu.
Masau Bwire, afisa habari wa klabu hiyo ameuambia
mtandao huu kuwa wanaendelea vizuri na mazoezi waliyoanza jana chini ya kocha
mkenya, Tom Alex Olaba katika uwanja wao wa Mabatini, Mlandizi, mkoani Pwani.
Masau amesema nia yao ni kujiimarisha mapema ili
kuleta changamoto mpya na ili kufanikisha ndoto hiyo, ndio maana Shooting
imekuwa timu ya kwanza kuingia kambini.
“Lengo letu ni kuchukua ubingwa au nafasi ya pili.
Tukishindwa sana, sana tunahitaji nafasi ya tatu. Hatuongei kwa kujifurahisha,
tunajipanga vilivyo”. Amesema Masau.
Afisa habari huyo alisema bado kurunzi zao
zinaangaza huku na kule illi kupata
nyota wengine watakaokuwa msaada mkubwa kwa msimu ujao.
Masau alisema Olaba aliagiza wapatikane wachezaji
wenye uzoefu na ligi kuu na kwa kutekeleza hilo wamesajili wachezaji kadhaa
akiwemo beki wa kati wa Mtibwa Sugar, Salvatory Ntebe.
“Hatujamaliza usajili, bado kurunzi yetu inaangaza
huku na kule. Tumedhamiria kufanya makubwa sana msimu ujao”. Alisema Masau.
Katika hatua nyingine, Masau alisema Ruvu Shooting
ni klabu inayowajali wachezaji wake nje na ndani ya uwanja.
“Kuna taarifa mbaya kwetu sisi. Kuna wachezaji
tumevunja mikataba yao na wanatusema vibaya. Lakini nikwambie, moja ya timu
inayojali wachezaji hapa Tanzania, Ruvu shooting ni kiboko”. Alisema Masau.
Hivi karibuni mchezaji wa klabu hiyo, Cosmas Adel
Lewis alivunja mkataba na klabu hiyo na kudai kuwa hakuridhishwa na maisha ya
Mabatini.
Cosmas alisema mpira ni ajira yake na anautumia
kujiingizia kipato, lakini kwa mazingira ya Shooting asingetimiza malengo yake
ikizingatiwa yeye bado ni kijana mdogo.
Nyota huyo aliuponda uongozi wa klabu hiyo kwa
kushindwa kuwajali wachezaji wake kimaslahi na ikafikia wakati wanatoroka
kambini kwenda kucheza ndondo ili kujiongezea kipato.
Akijibu hilo, Masau alisema mchezaji kutoroka
kambini na kwenda kucheza ndondo ili kujiongezea kipato halikubaliki hata kidogo
na kama aliona pesa haimtosha, kwanini alisaini mkataba?.
Masau alisema wachezaji walioachana na klabu hiyo
waache kuipaka matope kwenye vyombo vya habari.
Cosmas alisema kuna timu za ligi kuu
amekwishazungumza nazo, na wakati wowote atasaini mkataba na moja ya klabu ya
ligi kuu.
0 comments:
Post a Comment