
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
Imechapishwa Juni 14, 2014, saa 4:53 asubuhi
UCHAGUZI ni habari kubwa kwasasa katika klabu ya Simba, lakini kuna maisha mengine yanaendelea ikiwemo utekelezaji wa mpango wa kujenga uwanja wa kisasa katika eneo la Bunju, jijini Dar es salaam.
MPENJA
BLOG
jana iliripoti kuwa uongozi wa Simba sc umepelekea magereda na malori ambayo
kwa kutwa nzima yalikuwa yanafanya kazi ya kuondoa udongo mweusi uliopo eneo
hilo na kuweka udongo mpya utakaofaa kuotesha nyasi za uwanja.
Jitihada za kuwatafuta viongozi wa Simba
zilifanywa ili kupata ufafanuzi juu ya suala hilo na mtandao huu umejitahidi
kumtafuta rais wa Simba anayemaliza muda wake, Ismail Aden Rage ili kutoa
ufafanuzi wa zoezi hilo na pesa zimepatikana wapi wakati huu Simba ikitarajia
kufanya uchaguzi juni 29 mwaka huu.
Kuna watu walihusianisha mpango huo na kampeni
kuelekea uchaguzi. Kuna wagombea fulani (majina tunayo) walikuwa wanahusishwa
na kutoa fedha hizo ili kujisafishia njia, lakini halikuwa jibu sahihi na ikabidi
Rage asakwe ili atoe maelezo.
Katika mahojiano yake na mtandao huu, Rage amesema
sasa wameshaanza mambo baada ya kupata fedha mahali fulani (hakutaka kutaja) na
suala la wanachama kwenda na majembe, mapanga wameacha.
“Uko katika hatua nzuri kuna kitu ambacho
wataalamu wa udongo wanaita, wametoa ule udongo mweusi, wameanza kuweka udongo
ambao utafaa kupandia nyasi za uwanja”. Alisema Rage.
‘Na kama unakumbuka mara ya kwanza tulipoanza
kukarabati au kuujenga, tuliwaomba wanachama, wakaenda na mapanga na majembe.”
“Sasa tumeacha, kwasababu tulipata pesa mahali fulani,
sasa kuna magereda na malori yanafanya kazi ya kutoa huo mchanga ambao haufai na kuweka mchanga unaofaa
kwa kuotesha nyasi”. Aliongeza Rage.
Rais huyo aliyekuwa na mvutano mkali na wanachama wa
Simba pamoja na viongozi wenzake wakati wa uongozi wake alisema ndani ya siku chache
zijazo watawakaribisha waandishi wa habari ili wakapige picha, waone uwanja ulivyokuwa mzuri, ulivyopendaze na
hatua nzuri ambazo wanazo.
Hata hivyo, Rage alisema wamechoshwa na kutumia
gharama kubwa za kuweka kambi Hotelini, hivyo anataka kujenga Hosteli za
wachezaji kabla hajakabidhi madaraka kwa uongozi mpya.
“Lakini ninafanya vilevile mpango, kwasababu
tunatumia gharama nyingi sana kuwaweka wachezaji wetu Hotelini wakati tunapofanya
kambi”.
“kwasababu eneo hilo ni zuri, tunataka ikiwezekana
kabla sijaondoka, angalau nipate michoro au niweze kuweka msingi au ghorofa
moja ikibidi, tujenge hosteli katika
muda huu mfupi uliobaki”. Alisema Rage.
Kuhusu usajili, Rage alisema anataka kuweka rekodi
ambayo haijawahi kutokea Simba ambapo atawaachia viongozi wajao kitita kirefu
cha pesa, si chini ya milioni 300 kwa ajili ya usajili.
“Sasa hiyo nawaachia viongozi wajao ambao
ninakusudia kuweka rekodi ambayo haijatokea Simba tangu miaka yote, kwa maana ya kwamba nitakapoondoka mimi nitawaachia
pesa za wao kufanya usajili si chini ya milioni 300 watazikuta pale klabu”.
“Sivyo kama mimi nilipoingia sikukuta hata
shilingi moja nilikuta madeni basi, hiyo ndiyo nataka niweke tofauti yangu mimi
ambaye ninaithamini klabu yangu hii”. Alieleza Rage.
Nako upande wa pili, mwenyekiti wa klabu hiyo,
Yusuf Manji ameongezewa muda wa mwaka mmoja na wanachama wa Yanga ili
kukamilisha baadhi ya ahadi zake ikiwemo ujenzi wa uwanja wa kisasa maeneo ya
Jangwani.
Hatua za Simba zinaweza kumshitua na akaongeza
kasi.
Simba na Yanga ni klabu kongwe ambazo hazina hata
uwanja wa mazoezi.
Azam fc ni klabu pekee yenye uwanja wake wenye
ubora wa kimataifa uliopo Mbande, chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Mbeya City fc ambao wameshiriki kwa mara ya kwanza
ligi kuu msimu uliopita, wana mpango wa kujenga uwanja wao maeneo ya Iwambi
jijini Mbeya.
0 comments:
Post a Comment