Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Juni 22, 2014, saa 1:20 usiku
KAMATI ya uchaguzi ya klabu ya Simba inatarajia
kuanika orodha ya mwisho ya wagombea wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa
klabu hiyo unaotarajia kufanyika juni 29 mwaka huu jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, wakili Dkt. Damas
Daniel Ndumbaro amesema kamati yake ilikuwa na kikao leo hii kwa ajili ya
kufanya maandalizi ya kuelekea ukingoni mwa shughuli nzima ya uchaguzi.
“Kesho kunako saa 5:00 asubuhi katika ukumbi wa
mikutano wa TFF tutakuwa na mkutano na waandishi wa habari kuwaeleza mambo
mengine pamoja na orodha ya mwisho ya wagombea, orodha ya wale ambao wamevuka
vikwazo na watashiriki uchaguzi wa Simba sc”. Alisema Ndumbaro.
Aidha Dkt. Ndumbaro aliongeza kuwa baada ya
kutangaza orodha hiyo ya mwisho, kamati yake itatoa ruksa ya wagombea kuanza
kampeni rasmi kwa wanachama wa klabu ya Simba.
“Kwasababu kanuni inasema angalau siku tano,
tukishawatangaza kesho, wataweza kuingia msituni na kuanza kazi ya kunadi sera
zao”. Alisema Ndumbaro.
Hata hivyo, Dkt. Ndumbaro alisisitiza kuwa kampeni
ziwe za utulivu, ustaraabu na zisiwe za lugha ya matusi, bali wagombea wauze
sera zao ili wanachama waweze kuamua nani anafaa kwa manufaa ya klabu ya Simba.
0 comments:
Post a Comment