Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Juni 6, 2014, saa 1:33 jioni
MSHAMBULIAJI hatari wa Mbeya City fc, Mwegane Yeya
amefurahishwa na kitendo cha kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya
Tanzania, Taifa Stars chini ya kocha Mholanzi, Mart Nooij.
Akizungumza na mtandao huu, Mwegane amesema kuwa
anamshukuru sana Mungu kwa kupata nafasi hiyo kwasababu Tanzania ina wachezaji
wengi wenye viwango vya hali ya juu, lakini amechaguliwa yeye.
“Hii ni nafasi nyingine muhimu kwangu. Niliwahi kuitwa
katika kikosi cha Young Future Taifa Stars na Kim Poulsen, lakini sikufanya
vizuri kwasababu nilikuwa majeruhi. Naamini kwasasa nitaitumia vizuri nafasi
hii”. Alisema Mwegane ambaye ni hatari kwa kufunga magoli ya kichwa.
Mwegane aliongeza kuwa kuitwa na Nooij ni ishara ya
kukubali kazi yake, hivyo anajiona mwenye wajibu mkubwa wa kuisadia Stars
kuelekea mchezo muhimu dhidi ya Msumbiji.
Nyota huyu wa Wagonga Nyundo wa Mbeya ni miongoni wa
wachezaji wa Kikosi cha Taifa Stars kinachotarajia kuingia tena kambini
Jumatano (Juni 11 mwaka huu) ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya raundi
ya pili ya michuano ya Afrika dhidi ya Msumbiji itakayochezwa Julai 20 mwaka
huu jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Afisa habari wa shirikisho la soka
Tanzania, TFF, Boniface Wambura Mgoyo, Taifa Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager itakuwa na kambi ya siku tatu jijini Dar es Salaam
ikijumuisha wachezaji 28. Kwa mujibu wa programu ya Kocha Mart Nooij, Stars
itaingia tena kambini Juni 24 mwaka huu.
Wachezaji wanaotakiwa kuripoti kambini ni Deogratias Munishi,
Aishi Manula, Benedictor Tinoko, Kelvin Yondani, Said Moradi, Nadir Haroub,
Joram Nason, Shomari Kapombe, Oscar Joshua, Edward Charles, Aggrey Morris na
Pato Ngonyani.
Wengine ni Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Amri Kiemba,
Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Said Juma, Haruna Chanongo, Himid Mao, Said Ndemla,
John Bocco, Simon Msuva, Kelvin Friday, Ramadhan Singano, Khamis Mcha, Mrisho
Ngasa na Mwegane Yeya.
0 comments:
Post a Comment