Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MBEYA CITY FC kwa mara ya kwanza imepata udhamini
wa mamilioni ya fedha baada ya Kampuni ya Binslum Tyre Company Limited kumwaga
kitita kirefa cha milioni 360 kwa miaka miwili.
Kampuni hii ina nia ya kuifanya klabu hii kuwa
bora zaidi katika michuano ya ligi kuu soka Tanzania bara . Siku zote ukifanya
kazi kwa moyo wote, ukawekeza nguvu kubwa kutafuta mafanikio, mwisho wa siku
juhudi zako zinakulipa.
Msimu uliopita, Mbeya City walionesha nguvu kubwa
na mipango mizuri ya ndani na nje ya uwanja. Walicheza kwa kujituma, kwa malengo
na nidhamu kubwa. Timu hii ilikuwa bora kuliko timu zote tatu zilizopanda ligi
kuu kwa msimu uliopita.
Ashanti United na Rhino Rangers ziliishia kuonja
tu utamu wa ligi kuu na kurudi tena ligi daraja la kwanza. Lakini kwa Mbeya
City fc ilikuwa ni tofauti, walishindana mpaka dakika ya mwisho na kumaliza
katika nafasi ya tatu.
Waliwachomoa wakongwe, Simba sc katika ushindani
wa nafasi tatu za juu. Nidhamu ya wachezaji na kuwa na uchu wa mafanikio, maandalizi
ya muda mrefu, falsafa ya kocha Juma Mwambusi, hamasa ya mashabiki, uongozi
wenye mipango, ni miongoni mwa sababu chache kati ya nyingi zilizowafanya Mbeya
City wafike pale walipo.
Lakini kilio chao kilikuwa ni kukosa udhamini. Viongozi
walisikika mara nyingi wakisema wanaomba makampuni mbalimbali kujitokeza
kudhamini klabu. Haikuwa rahisi kupata udhamini kwasababu ndio kwanza watu
walikuwa wanapima upepo wake.
Hakuna mtu anayeweza kuwekeza pesa sehemu ya
hasara. Timu bora inang`ang`aniwa na wadhamini. Wala hakuna haja ya kwenda
kuwalilia wadhamini, wewe fanya mipango ya uwanjani, jenga timu ya ushindani, ‘mipesa`
itakuja yenyewe. Mafanikio ya Mbeya City yamemtekenya Binslum na kumwaga
milioni 360.
Ni pesa nyingi na endapo viongozi wa klabu watakuwa
makini kuzitumia, basi zitawasogeza mbele zaidi.
`Mipesa` ndio hiyo sasa, lakini viongozi wa Mbeya
City kumbukeni mambo machache yafuatayo;
Mosi; wachezaji wenu ndio chanzo cha udhamini huo.
Kumbukeni sio mkurugenzi wa jiji, wala katibu, wala mwenyekiti aliyemvuta Binslum.
Ni juhudi za Juma Mwambusi na benchi lake, pamoja na wachezaji wenu.
Ukali wa Paul Nonga, Mwegane Yeya, Peter Mapunda,
Steven Mazanda, Antony Matogolo, Deus Kaseke na wengineo ndio chanzo cha kupata
udhamini huo. Kwa maana hiyo, hawa vijana ndio walioleta neema hiyo.
Cha msingi, wapeni haki zao. Kama walikuwa
wanalipwa kiasi kidogo, basi jaribuni kufikiria namna ya kuongeza dau.
Wamefanya kazi kubwa na wameona milioni 360, hivyo onesheni kuwajali na kuwapa
dau zuri. Haitakuwa jambo jema kubakia katika kiwango walichokuwa wanalipwa
awali, lazima mfanye `makeke` ili vijana waneemeke na jasho lao. Sisemi ndio
mtumie pesa zote kwao,lakini angalau muoneshe kuwajali. Inakuwa mbaya sana
unapozalisha pesa, wengine wanafaidi. Inakatisha tamaa. Jitahidini kuboresha
maslahi ya wachezaji.
Pili: siasa ndio adui mkubwa wa mpira wa Tanzania.
Wenzenu Simba na Yanga walianza kula matunda ya udhamini kwa miaka mingi.
Lakini sina hakika kama fedha hizo zimezinufaisha klabu. Nadhani tatizo ni aina
ya uongozi unaoziongoza klabu hizo. Kuna `waswahili` wengi na wachumia matumbo.
Watu wanaoingia katika klabu hizi wanajineemesha wao.
Kama kuna mtu ana uhakika, aseme ni kiongozi gani
amefanya kitu kikubwa na cha kihistoria kwa klabu hizi mbili. Jibu ni hapana!.
Bado uongozi ni tatizo kubwa. Hakuna watu wa kusimamia mapato ya klabu,
hawajapatikana watu wakutumia ipasavyo fedha za udhamini.
Watu wanajali maslahi binafsi, Ni timu ambazo
zinaendelea kutegemea fedha za watu wachache `mungu watu`.
Ili kufikia malengo yenu, epukeni na siasa.
Fanyeni kazi kwa malengo na kuzuia mianya ya kuibiwa kwa fedha zenu.
Tatu; boresheni kikosi chenu ili kijitegemea. Moja
ya malengo ya kocha Mwambusi ni kuwa na timu iliyojikamilisha kwa kuzalisha
wachezaji wake. Soka la vijana ndio kila kitu. Boresheni upande huo ili muwe na
timu isiyochoka. Akichoka huyu mnapandisha bunduki nyingine. Muwekeze huko bila
kujali mafanikio yatapatikana lini. Uvumilivu unahitajika, lakini itawalipa
baadaye. Tumieni muda mwingi kubuni namna ya kuboresha kikosi chenu kwa kujifunza
kwa wenzenu walioendelea nje ya nje.
Pia sajilini wachezaji kwa mipango ili muwe na
timu ya ushindani. Udhamini utakuja zaidi. Mwingine atakuja kuweka lebo kwenye
soksi tu, mwingine viatu, watang`ang`ania wenyewe. Lakini mkibweteka basi
mtamfukuza hata Binslum.
Kuna watu wanajaribu kuwafananisha na Tukuyu
Stars. Wanasema ni nguvu ya soda. Kwa hapo mlipofikia, nadhani mnahitaji
kujikaza zaidi ili kuwaziba midomo watu hawa. Milioni 360 ziwekeeni mipango.
Nne; Mpango wenu wa kujenga uwanja ukazieni. Ni
muhimu kuwa na uwanja wenu. Ni gharama kubwa kujenga uwanja, lakini mkiwa mdogo
mdogo mtaweza. Mbeya City fc ni timu changa, mkianza sahizi litakuwa jambo
zuri. Unapopata `vijisenti` unatakiwa uanze mipango, huwezi kujua kesho
itakuwaje. Anzeni kidogo kidogo, mwisho wa siku mtakuwa tofauti na wazee wenu
wa siasa, Simba na Yanga.
Tano; msijiingize katika migogoro. Simba na Yanga
zinasumbuliwa na migogoro ya viongozi kwa viongozi, viongozi na wachezaji,
viongozi na makocha, viongozi na wanachama, n.k. Kwepeni mfumo huu wa
kiuongozi. Kuweni wamoja na muachane na siasa za mpira.
Mtaweza kama mtakuwa wamoja. Kutofautiana mitazamo
isiwe kigezo cha kuzua migogoro. Kaeni chini na kuchambua mawazo ya watu ili
kutoka na msimamo wa pamoja.
Binslum hongera sana kwa kuthamini soka. Wewe ni
miongoni mwa watu wachache wanaopenda soka la Tanzania. Nina hakika udhamini
wako hautakulipa kama unavyotaka, lakini kwasababu unapenda mpira, ndio maana
umemwaga fedha nyingi kiasi hicho.
Mbeya City fc mtendeeni haki Binslum. Kila la
kheri katika harakati zenu za kubadilisha soka la Tanzania.
0 comments:
Post a Comment