
NA BARAKA MBOLEMBOLE KWA MSAADA WA MTANDAO
Imechapishwa Juni 10, 2014, saa 9:37 alasiri
SIKU YA Alhamis wiki hii, michuano ya 20 ya
fainali za kombe la dunia itakata utepe wake nchini Brazil. Bila shaka pamoja
na burudani inayotarajiwa kuonekana katika ardhi ya soka yapo matukio ambayo
yanaweza kuvuta hisia kubwa zaidi wakati
michuano ikiendelea na hata baada ya kumalizika kwake. Je, ni matukio
gani ambayo unakumbuka msomaji wa mtandao huu?
Yafuatao ni matukio ambayo yamewahi kushangaza
katika michuano ya kombe la dunia miaka ya nyuma.
VITA YA SANTIAGO:
Tukio hili linahusisha mpambano wa kukata na
shoka kati ya Italia na waliokuwa
wenyeji wa michuano ya Mwaka 1962, Chile dhidi ya mabingwa wa miaka ya 1934 na
1938, Italia . Ilikuwa ni mechi yenye rafu nyingi za hatari na ubabe wa kila namna.
Mwamuzi kutoka England, Ken Aston alikuwa na wakati mgumu uwanjani katika
mchezo ambao wenyeji waliibuka na ushindi wa magoli 2-0.
Giorgio Ferrinni, mlinzi huyo wa zamani wa Azurri
alioneshwa kadi ya njano katika sekunde ya 12 tu ya mchezo, na kufikia dakika
ya nane mchezaji huyo aliondoshwa nje ya uwanja na mwamuzi, Aston. Katika hali
iliyoleta taharuki kubwa, beki huyo wa
Italia aligoma kutoka uwanjani, na baada ya dakika kumi za kutumia nguvu hadi
msaada wa askari polisi, ndipo mchezaji huyo akatoka
uwanjani.
Wakati mechi ikiendelea kushika kasi mchezaji wa
Chile, Lionel Sanchez akampiga ngumi kwa
makusudi, Humberto Maschio wa Italia lakini bado mchezaji huyo hakupewa hata kadi ya njano achilia mbali nyekundu
ambayo alistahili kupata kutokana na kitendo chake hicho kisicho cha kiungwana.
David Mari wa Azurri alimrukia teke la shingo, Sanchez na kitendo chake hicho kilimfanya
kuondoshwa uwanjani na Aston na kupelekea kadi ya pili nyekundu kwa Italia. Hii
ilikuwa ni katika fainali za mwaka 1962 zilizofanyika nchini Chile ambazo Brazil walitwaa ubingwa wao wa kwanza
katika bara la Marekani ya Kusini.

BRAZIL ILIPOCHEMKA NA PELE WAO
England walitwaa ubingwa wao wa kwanza na wa pekee
mwaka 1962 katika michuano ambayo ilifanyika nchini humo. Mshambuliaji wa
zamani wa Brazil, Pele alikwenda katika fainali zake za tatu za kombe la dunia
baada ya kucheza zile za mwaka 1958 nchini Sweden akiwa na miaka 17 na kufunga
magoli sita, kisha akaenda katika fainali za Chile miaka minne baadaye na
kuisadia Brazil kutwaa ubingwa wake wa pili mfululizo. Akiwa na umri wa miaka
25, Pele hakuwa fiti kimwili katika michuano ya England
Ilikuwa ni faida kwa mabeki wa timu pinzani.
Katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi dhidi ya Bulgaria, Pele alichezewa
rafu nyingi sana na walinzi wa Bulgaria, ingawa alifunga goli moja katika
ushindi wa Brazil wa magoli 2-0 siku hiyo. Pele hakuweza kufurahia michuano.
Alikosa mchezo wa pili wa hatua ya makundi na aliporudi uwanjani katika mchezo
wa mwisho dhidi ya Ureno hakuonekana kuwa fiti kwa asilimia mia. Ilikuwa ni
mwisho wa Pele na Brazil katika michuano hiyo baada ya kuondolewa katika hatua
ya makundi.

ITALIA WALITAKA KUNUNU MECHI
Italia ilikuwa ikihitaji sare tu ili kuvuka hatua
ya makundi. Poland wakiwa tayari wamefuzu kwa hatua ya mtoano walikwepa mtego
wa kupanga matokeo ambao ulitaka kuchezwa na Italia. Azurri walikuwa wakihitaji
sare dhidi ya Poland katika michuano ya mwaka 1974 iliyofanyika nchini
Ujerumani. Walijaribu kuwafuata Poland ili wawauzie mechi lakini katika hali ya
kimchezo, Poland walikataa kufanya hivyo.
Na mara baada ya mchezo kumalizika, Italia
walikuwa wamelala kwa kuchapwa magoli 2-1 na kuondoshwa mashindanoni katika
hatua ya awali. Ujerumami waliokuwa wenyeji wa michuano hiyo walitwaa ubingwa.
Italia ni wataalamu wa kupanga matokeo
katika mchezo wa soka ila mbinu hiyo iligonga mwamba mbele ya Poland.
ARGENTINA ILICHUKUA UBINGWA WA KWANZA KWA NJIA
CHAFU?
Ujerumani ilitwaa ubingwa ilipokuwa wenyeji wa
michuano ya mwaka 1974. Safari katika fainali zilizorudi barani Amerika ya
Kusini, katika nchi ya Argentina ilishuhudia wenyeji wakitwaaa ubingwa katika
ardhi ya nyumbani na kufuata nyayo za mataifa ya Uruguay, England na Ujerumani.
Katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi, wenyeji Argentina walihitaji
ushindi usiopungua magoli 4-0 mbele ya Peru ili kufuzu kwa hatua ya mtoano
Argentina walipata magoli mawili ya mapema kupitia kwa wakali wake, Mario Kempes na Alberto Talantallini. Hadi
kufika mapumziko walikuwa mbele kwa magoli 2-0.
Mchezo ukaonekana kuwa na lengo la kuwabeba
wenyeji na kuwaacha Brazil wakirudi nyumbani. Baada ya kuanza kwa kipindi cha
pili, Argentina iliongeza magoli mengine manne na kufikia dakika 90 matokeo
yakawa ni 6-O. Aliyekuwa kipa wa Peru,
Ramos Quiroga ambaye ni mzaliwa
wa Argentina alidaiwa kuachia magoli kimakusudi ili kuhakikisha
Argentina wanavuka kundi na kuwatupa nje Brazil.
RAFU MBAYA ZAIDI
Italia ilitwaa ubingwa katika michuano ya mwaka
1982 nchini Hispania, Azurri walikuwa wakitamba kwa ‘ wataalamu wa rafu’.
Lakini muda wote wa michuano hakujawaji kutokea rafu mbaya kama ile ambayo
ilichezwa na golikipa wa Ujerumani i,
Harald Schumacher dhidi ya mlinzi wa Ufaransa, Battison katika dakika ya
65 katika mchezo wa nusu fainali. Matokeo yakiwa ni goli 1-1 kipa huyo wa
Ujerumani alitoka nje ya eneo lake la hatari na kumrukia mlinzi wa kushoto wa
Ufaransa, Battison lakini kipa huyo hakupewa adhabu yoyote na mwamuzi.
Hakuoneshwa kadi ya njano, achilia mbali nyekundu
aliyostahili kupata. Battison alibebwa kwa machela hadi nje ya uwanja ikiwemo
kufanyiwa huduma ya kwanza kwa kuwekewa mashine ya hewa ya oxygen kabla ya
kukimbizwa hospitali. Schumacher ambaye hakustahili kuendelea kuwepo uwanjani
aliokoa penati ya mwisho ya Ufaransa baada ya mchezo kufika katika hatua ya
kupigiana mikwaju ya penalty, na Ujerumani ikatinga fainali ambayo walipoteza
mbele ya Italia waliotwaa taji lao la tatu la michuano na kulingana na Brazil
wakati huo.
Tutaendelea kuwaletea matukio ambayo yamewahi
kutokea na kushangaza watu wengi katika michuano hii mikubwa zaidi ya soka
duniani. Nawe pia ndugu msomaji unaruhusiwa kutoa tukio ambalo unalikumbuka.
0 comments:
Post a Comment