
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
FAINALI za kombe la dunia zimeanza kutimua vumbi
jana nchini Brazil kwa wenyeji kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya
Croatia.
Mabao mawili ya Neymar na moja la Oscar yalitosha
kumpa usingizi Luiz Felipe Scolari pamoja na wabrazil wote waliofurika uwanjani
kuwashuhudia vijana wao wa `Samba`.
Marcelo aliizawaida bao Croatia ya akina Dravko
Logarusic wa Simba sc baada ya kujifunga
katika hekaheka za kuokoa mpira wa krosi.
Michuano hii ni mikubwa zaidi katika ulimwengu wa
soka na inawakutanisha wachezaji wengi wa viwango vya juu duniani.
Mashabiki wa soka dunia wakiwemo Watanzania wanafuatilia
kombe la dunia. Wengine wamebahatika kwenda Brazil na waliowengi wanafuatilia
kwa njia ya luninga.
Siku zote kuwaangalia wengine ni njia ya
kujifunza. Ukiona nchi fulani imefanikiwa katika soka na kucheza fainali za
kombe la dunia, basi ujue wana mipango sahihi ya soka.

Ramadhan Singano anatumia jina kubwa la Lionel Messi wa Barcelona na Argentina
Hili linatakiwa likupe changamoto zaidi na
kutafakari namna ya kujiendeleza ili uwafikie wao. Inaweza isiwe leo wala kesho
kulingana nao, lakini ni muhimu kujifunza.
Uzuri fainali hizi zinaangaliwa na wachezaji wa
mpira, makocha, viongozi na mashabiki.
Tanzania ni taifa linalochechemea katika mpira wa
miguu. Safari imekuwa ndefu na timu yetu imekuwa tia maji tia maji. Kuna
jitihada zinafanyika wala hatutakiwi kuzibeza, lakini haizuii kusema bado
hatuna mipango mizuri katika soka
Jambo moja linalonivutia kwa watanzania wengi ni
kuwa na matumaini na mambo yao, lakini kuna watu wachache wanaharibu mipango.
Uongozi ni tatizo kubwa mno. Mpira wa Tanzania unakosa
viongozi wenye utashi wa kimaendeleo. Wanatumia muda mwingi kufanya mambo
yasiyoweza kutufanikisha na kusahau kujenga mifumo sahihi ya mpira.
Ukiwatazama wachezaji wa Tanzania na ukahojiana
nao, hakika wanaonekana kuwa na matumaini ya kufika Ulaya, lakini wamekosa vitu
vingi mno vya kiufundi. Na hii inatokana na taifa kukosa misingi ya soka la
vijana.
Kombe la dunia limeanza, kuna vipaji vingi. Kuna
wachezaji wenye umri mdogo kama ilivyo kwa wachezaji wa Tanzania katika klabu
za Simba, Yanga, Azam fc, Mbeya City fc na nyinginezo.
Simba na Yanga ndio klabu zenye mvuto zaidi kwa
soka la Tanzania. Azam fc na Mbeya City pia zinafuatia, lakini haziwezi kugusa
hata robo ya Simba na Yanga.
Beki wa Yanga, Kelvin Yondani anatumia jina la Mserbia Nemanja Vidic.
Wachezaji wengi wanapenda sana kucheza Yanga na
Simba. Hakina ni heshima kwa mchezaji kuzichezea timu hizi mbili.
Leo hii nataka kuwakumbusha wachezaji kitu kimoja
tu wakati huu wa fainali za kombe la dunia.
Najua wachezaji wengi wapo likizo na wana muda wa
kutosha kutazama fainali za kombe la dunia. Zinapochezwa ligi za Ulaya, hata
ligi yetu inakuwa inaendelea, hivyo wachezaji wanakuwa kwenye majukumu mazito ,
lakini sasa wengi wana muda wa kutosha.
Nazungumza na ndugu zangu wa kibongo wanaopenda
kujibebesha majina ya wachezaji wakubwa duniani, lakini wanashindwa kuonesha hata
robo ya watu wale.
Imekuwa kawaida kwa wachezaji kujiita majina ya
wachezaji wa Ulaya na wakati mwingine wanabatizwa majina hayo na mashabiki wao,
sina hakika kama wanaangalia aina ya uchezaji au ni mapenzi binafsi tu.

John Raphael Bocco akajichukulia jina la mwafrika mwenzake, Emmanuel Adebayor wa Togo na Tottenham
Nafurahia sana nikisikia mtu anajiita Lionel
Messi, Cristiano Ronaldo au jina lolote kubwa. Wakati fulani wachezaji
wanatumia majina ya wachezaji waliofanya makubwa duniani kwa miaka ya nyuma na
wengine miaka ya sasa kama vile akina Canavaro, Boban, Vidic, na mengineyo.
Ni jambo jema kujiita au kuitwa jina la mtu
mkubwa. Nakumbuka wakati nacheza soka la mchangani nilikuwa najiita Zinedine
Zidane na mashabiki wangu walikuwa wananifahamu kwa jina hilo.
Nilimpenda sana Zidane na kila anapocheza nilikuwa
namfuatilia kwa vitu vingi, lakini nilishindwa kutumia mambo yake kivitendo.
Kinadharia nilijifunza mengi kutoka kwake, ilipofika uwanjani, nilikuwa
nachemka kucheza kama yeye.
Halikuwa tatizo kwangu, lakini nilijifunza vya
kutosha kutoka kwa Zidane ambaye kwasasa ni kocha msaidizi wa Real Madrid.
Wachezaji wa Tanzania huu ni wakati wenu wa kujifunza
kwa wale watu mnaowapenda kwasababu wapo Brazil kwenye fainali za kombe la
dunia na ninyi mna muda wa kutosha sasa. Sijui mnafanya nini, lakini naamini mnatazama
kombe la dunia. Kama haiko hivyo basi hiyo ni ajabu kubwa mno.
Ni jambo jema kujifunza kwa kuiga. Ni muhimu sana kuwaangalia wachezaji wakubwa kwenye luninga. Kumtazama mwingine ambaye ana mafanikio
makubwa kuliko wewe ni njia nzuri ya kujifunza.
Kuwaangalia wachezaji wakubwa kutakufanya ujue
namna mpira unavyochezwa na kukuongezea ubora.
Kama
unacheza nafasi fulani, tumia muda mwingi kuwatazama wachezaji wanaocheza
nafasi yako ili kuchukua vitu muhimu kutoka kwao. Pia angalia kwa makini
maamuzi ya waamuzi ili ujue makosa ya mpira.
Kama wewe ni beki, tumia muda wako kuwatazama mabeki,
kama wewe ni kiungo basi komaa na viungo na kama wewe ni mshambuliaji basi
kazania kuwaangalia washambuliaji, unaweza kutoka na kitu kizuri.
Itumieni michuano ya kombe la dunia kujifunza
mpira kutoka kwa wachezaji wakubwa ili ligi ikianza wale wenye majina ya
wachezaji wakubwa angalau waonekana kuwa na vitu vipya.
Sisemi uwe kama Messi kabisa au Ronaldo au Neymar,
bali uwe angalau na kitu kidogo kumuhusu mchezaji unayempenda na pengine kutumia
jina lake.
Pia wakati huu wa mapumziko, nendeni kwenye makitaba kusoma vitabu vinavyohusu
soka. Kuna vitabu vizuri sana na mojawapo ni kitabu cha “Soccer for Dummies”.
Hiki ni kitabu kizuri na kinaweza kuwasaidia
wengi. Kupata taarifa na maarifa ya juu ya kile ukipendacho ni jambo jema.
Mkirudi kwenye michuano ya ligi kuu onesheni
mliyojifunza, lakini msisite kuomba ushauri kutoka kwa makocha wenu. Ni rahisi
kujua makosa kwa kukaa na mtu anayekutazama muda mwingi.
Mbali na kupata ushauri kutoka kwa makocha wenu,
kumbukeni kufuata ratiba ya mazoezi. Kufanya mazoezi mara 3-4 kwa wiki kutawafanya
muwe bora.
Kila la kheri katika kutazama kombe la dunia
nchini Brazil.
0 comments:
Post a Comment