Aliyekuwa kocha mkuu wa Yanga, Mholanzi Van der Pluijm (wa kwanza kulia) anatarajia kuungana na Mkwasa (wa pili kulia) nchini Saudi Arabia
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
KOCHA msaidizi wa klabu ya Yanga, Mtanzania
Charles Boniface Mkwasa ametimkia Uarabuni kuungana na aliyekuwa bosi wake
msimu uliopita Mholanzi, Hans Van Der Pluijm.
Pluijm baada ya kumaliza mkataba wake wa miezi
sita Yanga, aliamua kuondoka kwenda Saudi Arabia kuifundisha klabu ya ligi kuu
ya Saudi Arabia iitwayo Al Shoalah FC .
Kocha huyo Mholanzi aliondoka kwa makubaliano
maalum na Yanga, huku akieleza kuwa wakati anajiunga na Yanga aliwaambia kuna
dili anasubiria na kama litakwenda sawa ataondoka.
Baada ya mambo kwenda sawa, aliondoka Yanga na
kuagana kwa amani na uongozi wa Yanga pamoja na wanachama.
Pluijm alionekana kumkubali Mkwasa na sasa ameamua
kumtafutia kazi nchini Saudi Arabia na kocha huyo Mtanzania anakwea pipa usiku
huu.
Kabla ya kukwea pipa, Mkwasa amesema tayari
ameshawajulisha viongozi wa Yanga na umetoa Baraka zote na kumpa ushirikiano
mzuri.
“Viongozi wamenipa ushirikiano mzuri kwasababu nao
wangependa nipate uzoefu hususani kwa klabu za nje. Labda nitakaporudi nitaweza
kuisaidia klabu”. Alisema Mkwasa.
Hata hivyo, Mkwasa amegoma kutaja timu anayoenda
kufanya kazi kwasababu mambo hayajakamilika, lakini mambo yakienda sawa
ataanika kila kitu kwa wananchi.
Mkwasa aliongeza kuwa yeye amepata mwaliko baada
ya kutuma wasifu wake (CV), ingawa amekiri kuwa hayo yamejiri kutokana na
jitihada za aliyekuwa kocha wa Yanga, Hans Der Pluijm.
Kocha huyo aliyekuwa na Ruvu Shooting mwanzoni mwa
msimu uliopita aliongeza kuwa Saudia Arabia ipo juu kisoka ukilinganisha na
Tanzania na kizuri zaidi wachezaji wengi wa ulaya wanapochoka huwa wanatafuta
nafasi ya kucheza huko, hivyo itampa changamoto mpya.
Mkwasa alifafanua kuwa mashabiki wa Yanga wasiwe
na wasiwasi kwasababu anaenda kujifunza huko na kuna uwezekano akapangiwa
majukumu tofauti na aliyokuwa nayo sasa hivi.
“Naenda kupata uzoefu ambao naamini nitakapoupata,
naamini utaisaida Yanga na taifa kwa ujumla”. Alihitimisha Mkwasa.
Kila la heri Charles Boniface Mkwasa `Master`
katika maisha mapya ya kazi yako huko Uarabuni.
0 comments:
Post a Comment