Unapiga hivi! sawa?: kocha msaidizi wa Yanga, Charles Mkwasa akiwaelekeza wachezaji wake kwenye moja ya mazoezi ya timu hiyo msimu uliopita.
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
Imechapishwa Juni 15, 2014 saa 8: 31 mchana
KOCHA
msaidizi wa klabu ya Dar Young Africans, Charles Boniface Mkwasa `Master` amewashauri wachezaji wa
Tanzania kutumia michuano ya kombe la dunia inayoendelea nchini Brazil kama
sehemu ya darasa la kupata vitu vipya.
Mkwasa amezungumza na MPENJA BLOG mchana huu na kueleza kuwa kombe la dunia ni michuano
inayowakutanisha wachezaji wa aina zote,
wakongwe na vijana, hivyo wachezaji wa Tanzania wanatakiwa kutumia muda
kuwaangalia na kujifunza na si
kujifurahisha.
“Wachezaji wanaochezaji kombe la dunia wengi ni
`maproo`. Wana vitu vingi kuliko wachezaji wetu. Sisemi wajifunze wawe kama
wao, lakini angalau watoke na vitu
vichache vinavyoweza kuwasaidia katika maisha yao ya soka”. Alisema Mkwasa.
Mkwasa aliongeza kuwa kujifunza kwa kumtazama mtu
aliyekuzidi ni jambo jema kwasababu unaona vitu ambavyo hujawahi kufanya na
hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kujaribu kuvifanyia kazi.
Akizungumzia fainali za mwaka huu za kombe la
dunia, Mkwasa alisema alichokiona mwaka huu ni mchanganyiko mkubwa wa
wachezaji.
“Timu nyingi zimewapa nafasi chipukizi na
wanafanya kazi nzuri. Angalia timu kama Costa Rica, wana vijana wadogo ambao ni
hatari sana. Fundisho kubwa kwetu ni kuwaamini vijana na kuwapa nafasi”.
Alisema Mkwasa.
Kuhusu Hispania, Mkwasa alisema wana nafasi ya
kufanya vizuri katika mechi mbili walizonazo, lakini akaonya kuwa kama
watajiamini wanaweza kutolewa mapema.
“Wamefungwa mabao 5-1 na Uholanzi. Nilichokiona
mimi ni kwamba waliingia kwa kujiamini sana, na kadri walivyofungwa zaidi,
walizidi kujichanganya”. Aliongeza Mkwasa.
Mkwasa kwasasa anasubiri klabu yake ya Yanga ipate kocha mkuu atakayefanya kazi naye katika
msimu wa 2014/2015 wa ligi kuu soka Tanzania bara, ingawa bado haijawekwa wazi
kama ataendelea na kibarua hicho.
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji yupo katika mazungumzo
na kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa stars, Mbrazil Marcio
Maximo, na kuna taarifa kuwa mazungumzo hayo yamefikia hatua nzuri.
Mara wakapomalizana, Maximo atatua nchini na
kuanza rasmi kukinoa kikosi cha Yanga, lakini haijulikani kama Mkwasa
ataendelea kuwa msaidizi wa kocha mpya.
Mkwasa alikuwa msaidizi wa kocha Hans Van der Pluijm msimu uliopita, lakini
Mholanzi huyo alitimkia Uarabuni baada ya kumaliza mkataba wake wa miezi sita
jangwani.
Maximo atakapokuja nchini, mpinzani wake mkuu
atakuwa kocha mkuu wa Simba sc, Mcroatia Dravko Logarusic aliyeongezewa mkataba
wa miaka miwili na klabu ya Simba kufuatia ule wa kwanza wa miezi sita
kumalizika.
0 comments:
Post a Comment