
Imechapishwa Juni 13, 2014 saa 7:08 mchana
BAADA
ya Simba kumkosa kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’ ambaye amesaini mkataba
mpya na timu yake, kocha wa makipa wa Msimbazi, Iddi Pazi, amesema hakuna
jinsi, haraka sana Juma Kaseja anatakiwa kurudi Simba ili acheze kwa raha.
Kabla
ya Yanga kumsainisha Barthez, Simba ilikuwa imepiga hesabu za kumrudisha kipa
wao huyo wa zamani ili apambane na Ivo Mapunda ambaye hana mpinzani katika
kikosi cha timu hiyo.
Kocha
huyo alisema, kuna sababu tatu zinazomfanya Kaseja kuondoka Yanga kwani akibaki
hatoweza kufanya kazi yake kwa furaha na mafanikio.
Alisema
kwanza ushindani wa nafasi kati yake na makipa Deo Munishi ‘Dida’ na Barthez ni
mkubwa. Pili anaonekana hakubaliki kwa mashabiki wa Yanga na tatu ni ujio wa
kocha Marcio Maximo katika kikosi hicho.
Pazi
alisema: “Mahali alipo Kaseja (Yanga), kunaweza kumfanya astaafu kabla ya muda
wake au hata kuendelea kucheza soka kwa mashaka hivyo namtaka afikirie kurudi
Simba ili kutunza heshima na kufanya kazi yake kama ilivyokuwa awali.
“Kaseja
si kipenzi cha mashabiki Yanga na inapokuja wakati wa kazi anaweza kupata
wakati mgumu kutokana na kuzomewa na kumfanya kutojiamini akiwa kwenye kazi
yake.
“Pia
nimesikia Yanga wanamleta Maximo, nafikiri ni hofu kwa Kaseja kwa sababu siku
za nyuma kocha huyo alitofautiana naye wakiwa Taifa Stars, aje Simba ili awe na
amani.”
Pazi
pia amemtaka kipa huyo kufuta ndoto za kustaafu soka wakati huu ili awe kocha
akisema kipa huyo bado ana uwezo wa kucheza.
“Nafikiri
wapenzi wa Simba wanatakiwa kumpa Kaseja nafasi kwenye mioyo yao. Amefanya
mengi na naamini akirudi ataweza kufanya mengi na kumalizia soka lake Simba
akiwa na heshima,” alisisitiza.
CHANZO: MWANASPOTI
0 comments:
Post a Comment