![]() |
Tom Alex Olaba ameanza kunoa kikosi chake mapema ili kufuata mbio za Mbeya City FC waliozitikisha Simba, Yanga na Azam fc msimu uliopita. |
Na Frank Momanyi, Dar es salaam
Imechapishwa Juni 10, 2014, saa 6:17 mchana
KLABU ya Maafande wa Ruvu Shooting yenye maskani
yake Mabatini mkoani pwani imeingia kambini rasmi tayari kwa kujiwinda na
mikikimikiki ya ligi kuu soka Tanzania bara msimu mwaka 2014-2015 unaotarajia
kuanza kushika kasi agosti mwaka huu.
Akizungumza na MPENJA
BLOG , msemaji wa maafande hao, Masau Bwire amesema wameanza kambi hiyo
mapema kwa ajili ya kujiweka fiti kwa msimu ujao, huku lengo hasa likiwa ni
kupata pointi tatu muhimu kwa katika kila mchezo wa ligi kuu.
Masau alisema tayari wamenasa baadhi ya wachezaji
nyota hapa nchini kutoka katika klabu
kama vile Mtibwa sugar pamoja na kagera sugar watakaokisaidia kikosi hicho baada
ya kuvurunda msimu uliopita na kumaliza katika nafasi ya sita ya msimamo wa
ligi.
“Tumeamua kuanza maandalizi kabambe ya kujiandaa
na ligi msimu ujao, na sio maandalizi ya
zima moto, bali ni maandalizi ya nguvu
yatakayoleta mafanikio katika klabu yetu”.
“Kocha Alex Olaba yupo katika hali nzuri ya
kukiimarisha kikosi, na ndio maana tumeingia kambini mapema zaidi kuliko klabu
zingine hapa nchini.
“Lengo hasa likiwa ni kutimiza ndoto zetu za
kutwaa ubingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara msimu ujao”alisema Masau.
![]() |
Ruvu Shooting hawataki tena kupigwa 7-0 na Yanga, ili kukwepa kipondo, haoooo! kambini jana |
Msimu uliopita, Maafande wa Ruvu Shooting
walifanikiwa kumaliza katika nafasi ya sita ya msimamo katika ligi ambayo
ilikuwa na upinzani wa aina yake kutoka kwa klabu kama vile Mbeya City ambayo
ilipanda daraja na kuleta changamoto kubwa na kumaliza mzunguko wa kwanza bila
kupoteza mchezo hata mmoja.
Ruvu Shooting katika michezo 26 ya msimu uliopita,
walifanikiwa kujikusanyia pointi 38 ambapo walishinda mechi 10, sare 8 na kufungwa
mechi 8.
Walifunga magoli 28 na kuruhusu nyavu zao kuguswa
mara 38, hivyo wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa yalikuwa hasi nne (-4).
Wapiga kwata hao wanaona matokeo hayo yalikuwa
mabaya kwao, hivyo hatua ya kwanza ya kuyafuta msimu ujao na kuandika matokeo
mazuri zaidi ni kuingia kambini kuanza maandalizi ya mapema.
0 comments:
Post a Comment