Na Baraka Mbolembole
Imechapishwa Juni 2, 2014, saa 12:12 jioni
... Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars imefanikiwa kutinga hatua ya pili
ya mechi za mtoano baada ya kuiondosha timu ya Zimbabwe, The Warrios kwa jumla ya magoli 3-2. Kwa matokeo hayo, Stars itapambana na timu ya
Taifa ya Msumbiji, Black Mambas na mshindi wa michezo miwili baina yao atafuzu kwa
hatua ya makundi kuwania kufuzu kwa fainali za AFCON 2015, nchini, Morocco.
ZIMBABWE v TANZANIA,
Katika mchezo wa jana, Stars ilimkosa mshambuliaji wake namba moja,
Mbwana Samatta anayesumbuliwa na majeruhi ya nyama za paja, lakini bado kikosi cha kocha, Martin Nooij kilikaribia
kuondoka na ushindi wa kwanza ugenini baada ya kupita kwa miaka mitano. Mara ya
mwisho, Stars kushinda ugenini ni mwaka 2009,
wakati ilipoichapa, Mauritania
katika michezo ya makundi kuwania kufuzu kwa fainali za kombe la dunia, 2010.
Mbele ya watazamaji, 60, 000 katika uwanja wa
National Sports Stadium, Stars ilifuta goli
la kuongoza la wenyeji walioanza kufunga katika dakika ya tatu tu ya mchezo,
ila walijiweka sawa na kumiliki mchezo kuanzia dakika ya 10 hadi waliposawazisha
katika dakika ya 21 kutokana na mpira wa kona uliopigwa na kiungo wa kulia, Saimon Msuva.
Goli la nahodha, Nadir Haroub lilikuja
baada ya mlinzi huyo wa kati kupanda mbele huku akijiamini na kuruka juu kasha kupiga
kichwa cha uhakika. Mara nyingi Stars imekuwa ikikosa ufundi katika kucheza mipira
ya kona, ila goli hilo lilitokana na rekodi yake nzuri ya ufungaji wa mipira ya
kona limefungua njia na kuonesha kuwa bila kujiimarisha katika uchezaji wa mipira
iliyokufa timu inakuwa na nafasi finyu ya kupata ushindi katika michezo ya kimataifa.
SAFU YA ULINZI.
Wachezaji wote walipambana, safu ya ulinzi japo iliruhusu
magoli mawili iliweza kuwa imara na kuwa dhibiti wenyeji wao ambao walifungwa goli
la pili mara tu baada ya kuanza kwa kipindi cha pili. Zimbabwe walifanya mashambulizi
mengi lakini safu ya ulinzi iliyokuwa na Shomari Kapombe, Oscar Joshua, Kelvin
Yondanna Nadir ilifanya kazi kubwa.Goli la kusawazisha la wenyeji lilitokana na
mpira wa kona iliyokwenda moja kwa moja nyavuni lakini hilo haliwezi kutoa sifa
nzuri ya kipa, Deo Munish ambaye alikuwa mchezaji bora wa mechi kwa upande wa
Tanzania.
Nooij ameshuhudia timu yake ikiruhusu goli kwa mara
ya kwanza katika michezo minne aliyoiongoza na goli la kwanza la Zimbabwe
limemkumbusha kitu, kuwa timu nyingi za Tanzania zinafungwa katika dakika za mwanzo,
ila walishughulika na tatizo hilo katika ngwe ya pili na kupata matokeo yaliyoivusha
timu.
SAFU YA KIUNGO.
Stars
ilianza na viungo wanne na hakuna aliyetaraji kama, Erasto Nyoni angekuwepo uwanjani,
Nooij aliwapanga, Mwinyi Kazimoto, Msuva, Amri Kiemba na Nyoni na timu ilionekana
kumiliki mpira uwanjani japo bado wachezaji wa idara hiyo walionekana kuchoka mapema
na wakati mwingine kupiga pasi zisizofika kwa walengwa, Stars ilionekana kunufaika
na wachezaji hao wazoefu ambao waliweza kutulia uwanjani na kuisaidia timu.
Ukimtoa, Msuva safu hiyo ya kiungo ilikuwa na wachezaji wazoefu ambao wamekuwa kikosini
kwa miaka sita na kuendelea hivyo kocha, Nooij ametumia uzoefu wao na kuisaidia
timu kusonga mbele.
Nyoni, alitimiza majukumu yake vizuri japo alionekana
kushambulia wakati fulani, jukumu lake kubwa ilikuwa ni kukaba na kusaidia eneo
la kati na ulinzi wa kushoto, katika siku ambazo mchezaji huyo alionekana kuwa
bora, basi jana alikuwa bora kwakuwa alifanya kazi aliyoagizwa na Walimu wake.
Ugumu wa Stars ulikuwa katikati ya uwanja na hapo kulikuwa na viungo watatu wakabaji
Zimbabwe wanashambulia zaidi kupitia upande wao wa
kushoto na katika mchezo wa kwanza wiki mbili zilizopita, Kapombe alionekana kupata
tabu, ila uwepo wa Msuva uliwasukuma nyuma wenyeji badala ya kusonga mbele.
Stars ilimkosa, Samatta ambaye huwakimbiza wapinzani wake uwanjani, ila walikuwa
na mchezaji hatari uwanjani katika mchezo wa jana. Msuva alitumia vizuri kasi,
aliwasumbua walinzi wa Zimbabwe na kuwafanya washindwe kusogea mbele.
Hakika sasa timu ya Tanzania inaonekana kwenda vizuri
kiuchezaji, nidhamu na taratibu timu inaanza kujiamini hata ikiwa inacheza ugenini.
Msuva alijiamini na hilo ndilo jambo linalopaswa kufanyika kwa timu nzima uwanjani.
Kazimoto, pengine unaweza kuona hakuwa katika ubora wake wa juu ila mipira yake
mirefu ilifanya timu kushambulia kwa kushtukiza ila anapaswa kuwa makini zaidi uwanjani
na kupunguza kupoteza mipira mara kwa mara. Kiemba alicheza katika kiwango kizuri,
huku akicheza kama mchezaji wa kimataifa. Nooij alimpumzisha katika dakika 62 baada
ya kiungo huyo kuanza kucheza rafu.Ilikuwa ni dalili ya kuchoka, alioneshwa kadi
ya njano. Kuingia uwanjani kwa Frank Domayo mahala kwa Kiemba kulileta nguvu mpya
na timu nzima ilicheza kwa nguvu kulinda ushindi wa Dar es Salaam.
SAFU YA MASHAMBULIZI.
John Bocco alifunga
goli pekee katika mchezo wa kwanza wiki mbili zilizopita, safari hii hakupewa hata
nafasi ya kupandisha soksi zake. Walinzi wawili wa Zimbabwe walikuwa wakimtazama
yeye zaidi na hilo lilifanya mechi kuwa ngumu kwa upande wake ila bado, Stars
ilikuwa na ' bunduki' nyingine uwanjani. Thomas Ulimwengu amekuwa mshambuliaji muhimu
sana kwa Stars katika muda wa mwaka mmoja sasa, alifunga goli mara tu baada ya kuanza
kwa kipindi cha pili akitumia makosa ya walinzi wa Zimbabwe ambao hawakuwa makini.
Kufunga magoli mawili ugenini ni kitu ambacho hakijatokea
kwa muda sasa katika kikosi cha Stars lakini sasa timu inaweza kupanga vizuri mashambulizi
na kufunga magoli. Bila, Samatta timu imekuwa imara, niliwahi kuandika kuwa wachezaji
wazoefu wakitumia uzoefu wao watamsaidia Nooij, na ndicho walichofanya.
Msumbiji imekuwa tatizo kubwa kwetu ila hawatuzidi kitu. Walitufunga kutokana
na mbinu zetu ndogo za michezo ya kuamua timu ya kufuzu mwaka 2007 wakati,
Stars ilipokuwa ikihitaji ushindi tu ili kufuzu kwa AFCON, 2008, katika uwanja waTaifa
ila sitegemei makosa yale ya kina Amir Maftaha yatatumaliza tena wakati huu beki
tatu ikishikiliwa na Oscar Joshua.
Msumbiji walikuja Tanzania na kulazimisha sare ya goli
1-1 na Stars ilikwenda ugenini na kupata sare kama hiyo na hivyo kufanya mechi kuamuliwa
kwa sheria ya mikwaju ya penalty. Siamini kama, Samatta anaweza kukosa tena mkwaju
wake kama ilivyokuwa mwaka 2012 wakati walipotutoa kwa mikwaju ya penalty
katika harakati za kufuzu kwa AFCON 2013. Hawa jamaa tukiwaondoa, ‘ Jicho langu
la tatu’ limeona kabisa kuwa kikosi cha Nooij kinaweza kutinga Morocco mwakani mbele
ya Zambia, Niger na Cape Verde. Zambia, tunafungana nao, Cape Verde ni vibonde wetu,
labda hao Niger . Stars imekomaa sasa, inaweza kwenda AFCON mwakani, shukrani kwa walioambatana na timu
Zimbabwe, sapoti yao ilionekana . Makosa yapo, ILA Mwalimu atayafanyia kazi, naamini katika fikra na mtazamo wa Nooij, Msumbiji ndio wanafuata
sasa.
0714 08 43 08
0 comments:
Post a Comment