Dkt. Damas Daniel Ndumbaro, mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa Simba sc |
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Juni 1, 2014, saa 2:41 asubuhi
WAKATI Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa klabu
ya Simba unaotarajia kufanyika juni 29 mwaka huu, Mwanasheria Dkt. Damas Daniel
Ndumbaro akitaja matokeo ya usaili wa wagombea leo hii katika mkutano na
waandishi wa habari jijini Dar es salaam, ametumia nafasi hiyo kujibu mapigo kwa
mgombea aliyeenguliwa kugombea urais, Michael Richard Wambura.
Awali Wambura alipinga maamuzi ya kamati ya
uchaguzi ya Simba juu ya kuengua jina lake na kuweka hoja mbalimbali ikiwemo
uhalali wa kamati yenyewe.
Wambura alitoa hoja nzito ambazo tuliandika na
alisikika kwenye vyombo mbalimbali vya habari, lakini kuna maneno alitamka
yaliyokuwa yakihoji usomi wa mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi huo, Dkt.
Ndumbaro.
Hapo ndipo tatizo limeanzia na kumshitua Ndumbaro
aliyemwaga `upupu` mzito. Haikuwa kazi nyepesi kuyasikiliza maneno mazito
aliyotamka mwanasheria huyo mashuhuri na muhadhiri wa chuo kikuu cha Dar es
salaam tangu mwaka 2003.
Katika
maelezo yake, Ndumbaro amesema , Wambura amekiri kuwa aliipeleka Simba
mahakamani.
“Kuipeleka Simba mahakamani ni sawasawa na kifo,
mtu akishakufa lazima azikwe. Kamati ya uchaguzi ya Simba haijamuua Wambura
kwasababu alishakufa. Mtu akifa lazima azikwe, asipozikwa ataoza huyu. Na
kuzika mtu ni Baraka, ni thawabu”.
Aidha, Ndumbaro alilazimika kusoma aya ya mwisho
ya barua aliyodai kuandikwa na Wambura
wakati akiomba kusamehewe;
“Niwasomee aya ya mwisho ya barua ya kukiri kwa
Wambura , anasema: Pamoja na maelezo hayo, nakiri kukiuka katiba ya klabu yangu
kwa kuipelea klabu yangu mahakamani. Jambo hili halitajirudi tena na niko
tayari kushirikiana na wanachama wenzangu katika kuijenga na kuiendeleza klabu
ya Simba.
“ Ni matumaini yangu kuwa jambo hili litapatiwa
ufumbuzi, naomba msamaha kwa makosa yaliyojitokeza katika uchaguzi wa mwaka 2010. haya si maneno
yangu, ni maneno ya Michael Richard, anakiri kuipeleka Simba mahakamani,
anakiri kukiuka katiba ya Simba na anaomba asemehewe”.
“Sasa tujiulize, nani wa kumsamehe?, kwa mujibu wa
katiba ya Simba ni mkutano mkuu. Anapiga porojo nyingi, muulizeni, ana maamuzi yoyote ya mkutano mkuu yalimsamehe?, huyu
ndiye Michael Richard Wambura”. Alisema Ndumbaro.
Michael Richard Wambura |
Ndumbaro aliendelea kujibu mapigo na kusema kuwa katika
maelezo yake, Wambura anasema hajawahi kusimamishwa, lakini tarehe 5, Mei, 2010
alisimamishwa kwa mujibu wa katiba na tarehe 6, mei, 2010 alipewa barua ya
kusimamishwa na nakala ya maamuzi hayo yalifika kwenye vyombo vya habari na
akasisitiza kuwa nakala yake ipo.
“Imeitukana kamati kwamba kamati hii inakula
rushwa, mpaka rushwa ya ngono, hiyo ni kauli ya bwana Michael dhidi ya kamati”
“Bwana Michael amekiri kuwa ameipeleka Simba
mahakamani, kuipeleka Simba mahakamani ni kifo. Michael amenishambulia mimi
binafsi na kuhoji PhD yangu nimeisomea wapi, kwamba kweli hii PhD ipo?”
“Mimi nimwambie Michael kwamba waliosoma na mimi
wanajua uwezo wangu kitaaluma. Nimekuwa nikifundisha chuo kikuu cha Dar es
salaam tangu mwaka 2003, wanafunzi wangu ambao sehemu kubwa ni waandishi wa
habari kwasababu nafundisha `Media Law`, wanajua uwezo wangu”. Alifungkuka Ndumbaro ambaye ni mwanasheria kitaaluma.
Ndumbaro aliongeza kuwa: “Michael ni mwanafunzi
wangu wa mwaka wa kwanza wa chuo kikuu Huria akisoma shahada ya kwanza ya
sheria. Na mimi ni Muhadhiri wa chuo kikuu Huria, kwa hiyo Michael ni
mwanafunzi wangu. Kama mwanafunzi anapata uwezo wa kuhoji uwezo wa mwalimu
wake, hii ndio naipata kwa Michael kwa mara ya kwanza”.
“Mimi kama mwalimu wake nasahihisha mitihani yake,
najua udhaifu wa Michael Kitaaluma, ila maadili ya ualimu yananizuia nisiseme
udhaifu huo kwenye vyombo vya habari”.
“Kwasababu anasoma pale `Open Univervisty` (chuo
huria), kuna uwezekano kuwa ada inamsumbua, anataka kukusanya ada kutumia jina
la Ndumbaro. Wanaotaka kumchangia wamchangie yeye ili akalipe ada pale open
univesristy kwasababu Ndumbaro amemaliza madarasa yote”. Alisema Ndumbaro.
Alipotafutwa Michael Richard Wambura kujibu mapigo
haya, alisema yeye anajua haki yake iko palepale na hakutendewa haki na kamati
ya uchaguzi wa Simba sc chini ya mwenyekiti wake Ndumbaro.
Hata hivyo alisema atajibu hoja za Ndumbaro hapo
kesho baada ya kukaa chini na kuchambua hoja hizo za Ndumbaro.
Kesho Michael Richard Wambura ambaye rufaa yake
ipo TFF, atakuwa na mkutano na waandishi wa habari na anatarajiwa kujibu mapigo
kwa Ndumbaro.
`Ya Bunge
maalum la katiba yamegeukia upande wa Simba sc`. Tusubiri kuona mwisho
wa sinema hii tamu! Huu ndio mpira wa Bongo
0 comments:
Post a Comment