Simba SC siku nyingi hamjabeba ndoo, jipandeni |
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
TEL: 0712461976
TAYARI mchakato wa uchaguzi katika klabu ya Simba
sc umeshaanza na tayari mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi, Damas
Ndumbaro ametangaza kuwa juni 29 mwaka huu uchaguzi utafanyika
Wapo watu wengi wanaotamani kuiongoza klabu ya
Simba ambayo kwasasa ipo katika hali ngumu kwa soka la uwanjani.
Kumaliza nafasi ya nne nyuma ya Mbeya City, Yanga
na Azam fc ni jambo linalowaumiza wana Simba wote.
Ni msimu wa pili mfufulizo Simba wanakosa nafasi
ya kushiriki michuano ya kimataifa. Kwa ukongwe wake ni jambo la fedheha kubwa
japokuwa mpira uko hivyo.
Hatuwezi kuwakosoa Simba kwa matokeo waliyokuwa
wanapata kwasababu mpira wa miguu huwa unabadilika, lakini makosa yanapotokea
kwasababu ya watu fulani kutowajibika, hapo lazima ukosoaji uhusike.
Kwa mfano wachezaji kushindwa kucheza vizuri kwasababu
hawajalipwa posho na mishahara, unashindwaje kuukosoa uongozi kwa kushindwa
kuwajibika?
Kumekuwapo na mivutano ya muda mrefu baina ya
mwenyekiti wa Simba, sasa Rais, Ismail Aden Rage na baadhi ya wajumbe wake wa kamati ya utendaji
pamoja na baadhi ya wanachama.
Sinema nyingi zimeonekana na zimeandikwa, kila mtu
anafahamu yaliyokuwa yanatokea Simba sc.
Mwenyekiti wa Simba sc, Ismail Aden Rage anaondoka |
Jana aliyekuwa kiungo wa Simba sc msimu uliopita,
Henry Joseph Shindika wakati akihojiana na mtandao huu alikiri wazi kuwa maisha
ya wachezaji wa kitanzania ni magumu sana.
Joseph alisema watanzania tunajijua maisha yetu
wenyewe. Kama si baba, basi ni kaka au ndugu, kwahiyo unapokuwa unapata kipato
kuna watu wengi nyuma yako wanaohitaji msaada.
Kwahiyo utakuta mchezaji ana familia, anasomesha
wadogo zake na anategemewa na wazazi wake kutokana na mshahara anaopata katika
klabu.
Inapotokea hapewi mshahara mambo mengi yanakwama,
hivyo kisaikolojia anaathirika na kushindwa kucheza vizuri na ndio maana unaona
wachezaji hawana morali.
Maneno ya Joseph yana pointi kubwa ndani yake kuwa
mazingira ya wachezaji wengi wa kitanzania kutegemewa na familia zao yanasababisha
mshahara na posho kuwa kitu cha kwanza.
Kwa maana hiyo uongozi ukishindwa katika kipengele
hiki, matatizo mengi ya uwanjani yataonekana.
Kipindi cha Rage, matatizo ya kuchelewesha posho
na mishahara kwa wachezaji yameripotiwa mara nyingi na mpaka yeye mwenyeweanakiri
hilo.
Uongozi kwa soka letu ndio kila kitu. Sasa safari
ya Rage imefikia ukingoni na yatari uchaguzi utafanyika juni 29 mwaka huu
ambapo Rais mpya , makamu wa Rais na wajumbe wapya wa kamati ya utendaji
watapatikana.
Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa Simba sc, Damas
Ndumbaro alisema jana kuwa kamati yake haitakuwa na huruma hata kidogo kwa wale
wote watakaokiuka kanuni za uchaguzi.
Na akawaahidi wanasimba kuwa uchaguzi wa mwaka huu
utazingatia misingi ya haki, kanuni na sheria kwasababu kamati yake ina watu
makini, waadilifu na wenye nia ya kuisaidia Simba kupata viongozi wa kweli.
Haya ni maneno kutoka kamati ya uchaguzi, lakini
bado wenye mamlaka makubwa ya kuamua nani waingie kwenye uongozi ni wanachama
hai wa Simba sc.
Wanachama wa Simba mara nyingi mmetuita waandishi
wa habari na kusema mengi juu ya uongozi wa Rage.
Wengi wenu hamkuupenda uongozi wa Rage na
kuthubutu kusema Simba imekuwa hapa ilipo kwasababu ya mwenyekiti huyo. Sasa
anaondoka na hatagombea tena.
Mambo kadhaa mnayotakiwa kuzingatia ni pamoja na
kutambua kuwa klabu yenu inahitaji kiongozi mpya kwa kila kitu, zaidi awe na
mawazo chanya kwa ajili ya kuiendeleza klabu.
Rais wenu awe mpenzi wa Simba, aipende Simba na atumie
muda wake kuisaidia Simba sc.
Awe kiongozi mwenye mtazamo wa mbali ili katika
kipindi chake cha miaka miwili ya uongozi, tuione Simba mpya.
Tunajua mna hamu ya kurudisha heshima yenu, na kwa
kuanza, lazima mhakikishe juni 29 mnachagua mtu mwenye nia na sera nzuri kwa
klabu ya Simba.
Simba na Yanga zimekuwa kitega uchumi kwa watu fulani.
Kuna kiongozi mmoja wa soka aliwahi kusema tukiwa katika mazungumzo ya kwaida
tu kuwa hakuna hela rahisi kama kwenye mpira.
Alimaanisha kwenye mpira kuna mwanya mkubwa wa
kuchuma pesa na ukajenga nyumba, ukaendesha gari na kufanya mambo mengine bila
kutumia nguvu.
Simba ni klabu kubwa yenye rasilimali. Hivyo kuna
watu wana nia ya kuomba uongozi ili wajinufaishe wenyewe.
Wataomba wengi , lakini watakuwa na nia tofauti.
Ni ngumu sana kumjua mtu mwenye nia nzuri kwa kumuangalia machoni.
Kidogo unaweza kujiridhisha kuwa fulani hafai kama
aliwahi kuwa kiongozi kwasababu unajaribu kukumbuka mazuri yake na mabaya yake,
lakini kwa mtu mpya kabisa ni ngumu sana.
Kama baadhi ya watu waliowahi kuwa viongozi
watarudi kwenye uchaguzi huu, basi wanachama kaeni chini mtathimini kwa kina
kama wanaweza kuja na mambo mapya.
Kila kitu kipo juu yenu, mtakayemchagua ni ninyi
na mtakaokuja kujuta ni ninyi. Wanachama wa Simba, kuweni makini kipindi hiki
na msiridhishwe na siasa nyepesi. Mpira ni vitendo na si maneno.
Kwa bahati mbaya watanzania wengi tunaingiza siasa
hasa kwenye masuala ya msingi. Ni rahisi mtu kutamka kuwa nitaijengea klabu
uwanja, lakini ikifika utekelezaji, maneno ya siasa yanatumika.
Kila la heri Simba kuelekea katika uchaguzi wenu
juni 29 mwaka huu, kazi imebaki kwenu kwa mujibu wa katiba ya klabu yenu.
0 comments:
Post a Comment